• HABARI MPYA

    Friday, January 23, 2009

    KANUNI ZA LIGI KUU BARA HIZI HAPA


    Beki wa kulia, Shadrack Nsajigwa (kushoto) wa Yanga akijaribu kumtoka kiungo wa Mtibwa Sugar, Uhuru Suleiman.

    UTANGULIZI
    TFF imezifanyia marekebisho kadhaa baadhi ya Kanuni za Ligi Kuu ili kuondokana na migogoro isiyokuwa ya lazima. Mabadiliko haya Lengo lake kuu ni kuwa na Ligi iliyo bora zaidi, ambayo itaweza kuleta ushindani kwa timu shiriki na pia kutoa burudani zaidi kwa watazamaji, pamoja na kuchochea wadhamini zaidi kujitokeza kwa ajili ya kudhamini ligi na timu shiriki.
    Ligi iliyo bora, itawezesha kupata wachezaji bora watakaounda timu bora ya Taifa itakayoweza kufanya vizuri katika medani ya kimataifa na pia tutaweza kupata klabu zitakazotuwakilisha vyema katika mashindano ya kimataifa kwa ngazi ya klabu. Mafanikio haya yataweza kukuza na kuendeleza kiwango cha soka katika nchi yetu na pia kuijengea heshima Tanzania katika ulimwengu wa soka.
    TFF inafahamu na inaamini kuwa mpira wa miguu ni mchezo wenye nguvu, unaopendwa na watu wengi duniani na unaoweza kuvutia watu wengi kuwekeza iwapo kanuni, taratibu na sheria za mchezo huu zitafuatwa na kuheshimiwa na pia kanuni za ‘fair play’ zitazingatiwa na wachezaji, makocha, waamuzi, viongozi, washabiki, na wengine wote ambao kwa njia moja au nyingine wanahusika na mchezo wa soka.
    TFF inaagiza kilabu, makocha, na waamuzi kuzisoma kwa makini kanuni hizi na kuhakikisha zinaeleweka na kufuatwa kwa faida ya mchezo wa mpira wa miguu. TFF inapenda kuwakumbusha watu wote kuwa soka kama ilivyo michezo mingine yote inalindwa na sheria pamoja na kanuni. Bila sheria michezo itakuwa ni vurugu tupu. TFF inaziomba kilabu kuhakikisha kuwa kanuni hizi pia zinaeleweka vizuri kwa wachezaji na washabiki wake, kwani itasaidia kuwafanya wafahamu kanuni na taratibu za mpira wa miguu vizuri zaidi na kwa kuzifahamu kanuni zaidi, zitawafanya wawe wachezaji bora zaidi na wataepuka kuadhibiwa kwa makosa ambayo yanaweza kuepukika.
    Kanuni na sheria huwekwa kwa ajili ya kuufanya mchezo uwe na ladha katika kuucheza na pia uwe na ladha katika kuuangalia na hivyo kuufanya uwe na burudani zaidi. Tukitumia nguvu na ‘spirit’ ya soka inavyotakiwa, tutaweza kujenga jamii na dunia bora yenye afya zaidi, upendo, amani, furaha na usawa.
    TFF siku zote itahakikisha mchezo wa soka unakuwa na heshima kwa kusimamia kwa uadilifu kanuni na sheria za mchezo huu, kutoa adhabu inapobidi, kuelimisha na kuhakikisha siku zote mshindi anapatikana uwanjani kwa kufuata kanuni na taratibu za mchezo na siyo kwa kutumia njia chafu zisizokubalika.

    MICHEZO NI FURAHA
    TANZANIA FOOTBALL FEDERATION
    YALIYOMO


    Na Kanuni Ukurasa
    SURA YA KWANZA
    Kuundwa, Matumizi na Tafsiri

    1. Kuundwa 7
    2. Matumizi na Tafsiri 7

    SURA YA PILI
    Daraja, Aina na Namna ya Uendeshaji Ligi
    3. Daraja la Ligi 8
    4. Namna ya Uendeshaji wa Ligi Kuu 8
    5. Uwanja wa Nyumbani na Ugenini 9

    6. Mshindi wa Ligi 9

    7. Msimu wa Ratiba ya Ligi 10

    SURA YA TATU
    Taratibu Za Mchezo

    8. Taratibu za Mchezo 11

    9. Kuahirisha Mchezo 16

    10. Waamuzi 17

    SURA YA NNE
    Huduma ya Kwanza na Bima

    11. Huduma ya Kwanza 18

    12. Bima 18

    SURA YA TANO
    Ada ya Ushiriki Na Usimamizi Wa Ligi

    13. Ada ya Ushiriki 19

    14. Usimamizi wa Ligi 19

    SURA YA SITA

    15. Rufani na Utaratibu Wake 19

    16. Utaratibu wa Kukata Rufani 20

    17. Ada ya Rufaa 20

    SURA YA SABA

    18. Mgawanyo wa Mapato 21

    19. Gharama za Mchezo 22

    SURA YA NANE

    20. Kujitoa Katika Ligi 23

    21. Kutofika Kituoni/Uwanjani 24

    22. Kuvuruga Mchezo 25

    23. Kupanga Matokeo 26


    SURA YA TISA
    Udhibiti wa Mienendo na Adhabu kwa Wachezaji, Waamuzi na Viongozi


    24. Uchezaji wa Kiungwana (Fair Play) 27

    25. Udhibiti wa Wachezaji 31

    26. Udhibiti na Adhabu kwa Waamuzi 34

    27. Udhibiti wa Kamishna 33

    28. Udhibiti wa Waalimu 34

    29. Udhibiti wa Viongozi 35

    30. Viwango na Utaratibu wa Adhabu kwa Wachezaji 37

    31. Adhabu kwa Klabu 38

    SURA YA KUMI
    Usajili Na Uhamisho Wa Wachezaji

    32. Kipindi cha Usajili 39

    33. Hadhi ya Wachezaji 39
    34. Kupata Upya Hadhi ya Ridhaa 40

    35 Kuacha Shughuli 40

    36. Usajili 40

    37. Vipindi vya Usajili 41

    38. Pasi ya Wachezaji 42

    39. Maombi ya Usajili 42

    40. Hati ya Uhamisho ya Kimataifa 43

    41. Kuazimwa Kwa Mkopo Wachezaji wa Kulipwa 43

    42. Wachezaji Wasiosajiliwa 44

    43. Masharti Maalum Yanayohusu Mikataba kati ya Wachezaji wa Kulipwa na Klabu 44

    44. Usajili na Uhamisho wa Wachezaji 45

    45. Uthibitisho wa Usajili 46

    46. Majina ya Wachezaji 46

    47. Idadi ya Wachezaji 46

    48. Kilabu/Wachezaji Wanaositisha Mikataba 46

    49. Wachezaji Waliopandishwa 47

    50. Wachezaji Huru 47

    51. Wachezaji wa Kuhamishwa 48

    52. Wachezaji Kutoka Nje ya Nchi 48

    53. Ngazi za Uthibitisho wa Usajili 48

    54. Kutengua Uthibitisho wa Usajili 48

    55. Katazo 49

    56. Uhamisho wa Mchezaji 49

    57. Uhamisho Kwenda Zanzibar 50


    SURA YA KUMI NA MOJA
    Adhabu Zihusuzo Usajili Na Uhamisho

    58. Adhabu Zihusuzo Usajili na Uhamisho 51

    59. Uhamisho Nje ya Nchi 52


    SURA YA KUMI NA MBILI
    Mengineyo
    60. Mwalimu wa Timu 53

    61. Daktari wa Timu 54

    62. Timu za Pili na Watoto 54

    63. Udhamini 56

    64. Ufafanuzi 56

    65. Tafsiri 56

    66. Marekebisho ya Kanuni 57

    67. Kufuta Kanuni 57

    68. Mambo Yasiyomo Kwenye Kanuni Hizi 57


    NYONGEZA
    Jedwali La Kwanza


    57 (5) Ada za Usajili na Uhamisho wa Wachezaji 58

    58 (B) Mgawanyo wa Ada za Usajili na Uhamisho wa 58
    Wachezaji Kutoka Tanzania Bara Kwenda Tanzania Zanzibar


    KANUNI ZA LIGI KUU

    SURA YA KWANZA
    KUUNDWA, MATUMIZI NA TAFSIRI

    KANUNI YA 1
    KUUNDWA

    Kanuni hizi zimeundwa chini ya Ibara ya 76 ya katiba ya TFF ya mwaka 2004 na zitatumika Tanzania Bara.

    KANUNI YA PILI 2
    MATUMIZI NA TAFSIRI

    Katika Kanuni hizi isipokuwa pale ambapo imeainishwa vinginevyo:-

    “CECAFA” tafsiri yake ni: Council of East and Central Africa Football Associations” ikiwa na maana ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu la Nchi za Afrika Mashariki na Kati.

    “TFF” tafsiri yake ni Tanzania Football Federation”, ikiwa na maana ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania.

    “FIFA” tafsiri yake ni “Federation Internaltionale de Football Association” ikiwa na maana ya Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu.
    “FRAT” tafsiri yake ni “Football Referees Association of Tanzania”, ikiwa na maana ya Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania.

    “Kamati ya Utendaji” maana yake ni Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania.”

    “Klabu” maana yake ni klabu cha mpira wa miguu.

    “Mpira” maana yake ni Mpira wa Miguu.

    “TAFCA” tafsiri yake ni “Tanzania Football Coaches Association” ikiwa na maana ya Chama cha Walimu wa Mpira wa Miguu Tanzania.

    “TASMA” tafsiri yake ni Tanzania Sports Medicine Association ikiwa na maana ya Chama cha Madaktari wa Tiba kwa Wanamichezo Tanzania.

    “Timu” maana yake ni Timu ya Mpira wa Miguu
    ‘Sputanza’ tafsiri yake chama cha wachezaji wa soka Tanzania

    SURA YA PILI
    DARAJA, AINA NA NAMNA YA UENDESHAJI LIGI

    KANUNI YA 3
    DARAJA LA LIGI

    Kanuni hizi ni kwa ajili ya Ligi Kuu msimu wa 2008/9.

    KANUNI YA 4
    NAMNA YA UENDESHAJI WA LIGI KUU YA VODACOM

    Ligi Kuu itashirikisha timu kumi na mbili (12) tu kumi (10) Zilizobaki toka msimu uliopita na timu mbili (2) zilizopanda daraja.

    TFF ilitekeleza makubaliano yake na FIFA ya kupunguza idadi ya timu za Ligi kuu toka 16 na kufikia 12 ambayo yamekamilika katika msimu wa 2008/09. Vilevile timu zinatakiwa kuwa na mikataba na wachezaji na makocha iliyosajiliwa TFF, na kuwa na timu za vijana.

    Hivyo makubaliano na FIFA yametekelezwa kwa utaratibu ufuatao :
    • Ligi Kuu msimu huu itashusha timu tatu (3);
    • Vilabu vinatakiwa kusajili timu za vijana TFF kabla ya Ligi kuu kuanza
    • Timu zitacheza Ligi ya mikondo miwili nyumbani na ugenini ;
    • Timu tatu (3) za mwisho katika msimamo wa Ligi zitashuka daraja.


    KANUNI YA 5
    UWANJA WA NYUMBANI NA UGENINI

    (1) Uwanja wa nyumbani ni ule ulio katika mji ambao timu mojawapo ina makao yake na uwanja wa ugenini ni ule ambao timu pinzani imekaribishwa kucheza.

    (2) Endapo timu yoyote haina uwanja wa nyumbani unaofaa kwa mashindano ya Ligi, timu husika inaweza kuchagua kwa idhini ya TFF, uwanja mwingine wowote, hata nje ya mji huo au Mkoa ili mradi Uwanja huo uwe jirani na mkoa wa timu husika ndani ya Tanzania Bara na uwe na sifa zinazokubalika.

    KANUNI YA 6
    MSHINDI WA LIGI
    (1) Mshindi katika mchezo wowote wa ligi atapatikana kwa kufunga magoli mengi zaidi ya timu pinzani.

    (2) Mshindi atapata pointi tatu (3)

    (3) Endapo timu zitatoka sare ya aina yoyote, kila timu itapata point moja.

    (4) Timu itakayoshindwa itakosa pointi.

    (5) Mshindi katika ligi ni timu iliyopata pointi nyingi zaidi ya timu zote zilizoshiriki katika Ligi hiyo.

    (6) Ikiwa timu mbili zitalingana kwa pointi baada ya michezo mshindi atapatikana kwa tofauti bora ya magoli ya kufungwa na kufunga, kama tofauti hiyo haitoi mshindi, mshindi atakuwa ni mwenye magoli mengi ya kufunga, kama pia magoli ya kufunga hayatoi mshindi; basi mshindi atakuwa ni yule atakayekuwa na pointi nyingi kwenye michezo miwili iliyohusisha timu hizi mbili wakati, na kama pia michezo hiyo hautoi mshindi, mshindi atakuwa yule aliyefunga magoli mengi zaidi katika mchezo wa ugenini uliozihusisha timu hizi mbili, iwapo bado haitoi mshindi, mshindi atakuwa aliyefunga magoli mengi ya ugenini katika msimu mzima, iwapo bado haitoi mshindi timu hizi zitacheza mchezo mmoja katika uwanja utakaochaguliwa na TFF, na taratibu zote za kupata mshindi zitafuatwa kama mchezo wa Fainali.
    (7) Mshindi wa kwanza wa Ligi atakuwa bingwa wa Ligi kuu ya Tanzania Bara kwa mwaka 2008/9 na atapewa kikombe cha ubingwa.

    (8) Mshindi wa kwanza wa LIGI KUU atawakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya Kilabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati.

    (9) Mshindi wa kwanza wa LIGI KUU ataiwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya Kilabu Bingwa Afrika (Champions League).

    KANUNI YA 7
    MSIMU WA RATIBA YA LIGI
    1. Kamati ya Utendaji ya TFF itatangaza tarehe za kuanza na kumalizika kwa msimu wa Ligi Kuu.
    2. Ratiba ya Ligi itaandaliwa na kutolewa na TFF kabla ya Ligi kuanza.
    3. Ratiba ya Ligi ikishatolewa haitabadilishwa isipokuwa kama kuna dharura au sababu nzito na za msingi.
    SURA YA TATU
    TARATIBU ZA MCHEZO
    KANUNI YA 8

    (1) Kutakuwa na mkutano wa kitaalamu wa maandalizi kabla ya mchezo (pre-match meeting) ambao utafanyika kabla ya mchezo. Mkutano huu utafanyika saa 4.00 asubuhi siku ya mchezo. Kwa sababu maalum, mkutano huu unaweza kupangiwa muda, siku na mahali pengine kama itakavyopendekezwa na Chama cha Mpira cha Mkoa na kuidhinishwa na TFF. Timu zinazocheza siku hiyo pamoja na waamuzi na kamisaa wanatakiwa kuhudhuria.

    (2) Timu yoyote itakayochelewa kufika kwenye Mkutano wa kitaalamu wa maandalizi ‘Pre match meeting’ au itakayoleta watu wasiohusika au wasiokuwa na vitambulisho itatozwa faini ya TShs 100,000/= na timu itakayoshindwa kufika kwa sababu zisizo za msingi itatozwa faini ya TShs 200,000/=.
    (i) Taarifa ya ukiukwaji wa vipengele hivi itawasilishwa na Kamisaa na Msimamizi wa Kituo.
    (ii) Faini zote zitalipwa mara tu baada ya mchezo kumalizika kwa kukata kwenye mapato ya timu. Endapo mapato ya timu ya mchezo huo hayatoshi watakatwa kwenye mchezo unaofuata.
    (3) (a) Wafuatao ndio wanaotakiwa kufika kwenye mkutano wa maandalizi na vitambulisho vyao
    vilivyotolewa na TFF, asiyekuwa na kitambulisho hicho hatoruhusiwa kuhudhuria kikao:-
    (i) Mwalimu wa Timu
    (ii) Mtunza vifaa wa Timu
    (iii) Nahodha wa Timu na;
    (iv) Daktari wa Timu.

    (b) Kila timu inatakiwa kufika na vitu vifuatavyo:-
    (i) Jezi za wachezaji wa ndani zenye namba kubwa zinazosomeka zinazoanzia na nambari 1 hadi 30 ikiwa ni pamoja na jezi mbili za walinda milango. Endapo rangi za sare za timu zote mbili zitafanana, timu ngeni italazimika kubadilisha sare yake.

    (4) Jezi ya mlinda mlango isifanane rangi na jezi za wachezaji wa ndani lakini inaweza kufanana na jezi ya mlinda mlango wa timu pinzani.

    (5) Mchezaji atakayevaa jezi isiyokuwa na nambari mgongoni hataruhusiwa kucheza.

    (6) Viwanja vyote vitakavyotumika kwa michezo yote vitaidhinishwa na TFF.

    (7) TFF ina madaraka ya mwisho ya kuhamisha mchezo au kubadilisha kituo cha mchezo kwa sababu inazoona zinafaa kwa mchezo au mashindano husika.

    (8) Manahodha wa timu zinazoshindana wanatakiwa kuvaa vitambulisho vya rangi tofauti na jezi zao kwenye mikono ya jezi zao.

    (9) Kila mchezaji ni lazima avae “shin- guards” kwenye miguu yote miwili.

    (10) Wachezaji wanaruhusiwa kushangilia goli kwa wastani. Ushangiliaji wa kupitiliza, kiasi cha kupoteza muda au kufanya ishara yoyote isiyokuwa ya kiuanamichezo au ya kashfa au matusi kwa timu pinzani au watazamaji hairuhusiwi. Mchezaji/wachezaji watakaofanya vitendo hivyo wataadhibiwa kwa kufungiwa michezo isiyozidi mitatu au faini ya laki moja au vyote kwa pamoja. Mchezaji atakayevua jezi kushangilia ataonyeshwa kadi ya njano.

    (11) Michezo yote ya ligi itachezwa kwa vipindi viwili vya jumla ya dakika tisini (90) kila kipindi kikiwa na dakika arobaini na tano (45) na mapumziko ya dakika zisizopungua tano (5) na zisizozidi kumi (15) kati ya vipindi hivyo.

    (12) Timu zinatakiwa kufika kiwanjani si chini ya dakika (60) kabla ya wakati uliopangwa kuanza mchezo. Michezo inayoonyeshwa moja kwa moja na Luninga muda utapangwa kulingana na muda wa muda wa mchezo wa siku hiyo.

    (13) Timu itakayochelewa kufika kwa mujibu wa masharti ya Kanuni ya 8 Kifungu cha 12; itatozwa faini ya sh. 300,000/=.

    (14) Timu zitakaguliwa kwenye vyumba vyao vya kuvalia na endapo rangi za sare za timu zote zitafanana timu ambayo haikufika kwenye kikao cha maandalizi italazimika kubadili jezi.
    (i) Kila kilabu itasajili TFF rangi ya jezi zake kwa mechi za nyumbani na ugenini kabla ya kuanza msimu wa Ligi. Kilabu itakayokiuka itatozwa faini ya Tshs. 300,000/=

    (ii) Vyumba vya kuvalia wachezaji vitapangwa kulingana na ratiba inavyosomeka, kwa timu ya nyumbani na ugenini. Sehemu ya kufanyia mazoezi na benchi la wachezaji wa akiba itakuwa upande ule ule wa vyumba vya kuvalia. Kilabu itakayokiuka itatozwa faini ya Tshs 300,000/=.

    (iii) Ni marufuku kwa viongozi kuingia uwanjani kinyume na taratibu za mchezo kabla, wakati au baada ya mchezo. Timu itakayokiuka kipengele hiki itatozwa faini ya sh. 300,000/=.

    (iv) Ni marufuku kwa na mashabiki kuingia uwanjani kabla, wakati au baada ya mchezo. wakati au baada ya mchezo. Timu itakayokiuka kipengele hiki itatozwa faini ya sh. 300,000/=.
    (15) Timu zitakaguliwa na mgeni rasmi kiwanjani kwa kupeana naye mikono na kwa heshima zote zinazostahili. Timu itakayokiuka itatozwa faini ya Tshs. 300,000/=.

    (16) Wakati wa mapumziko, timu zitalazimika kwenda kupumzika kwenye vyumba vyao vya kuvalia. Timu zinalazimika kupitia kwenye milango na siyo vinginevyo. Timu itakayokiuka itatozwa faini ya Tshs. 300,000/=.

    (17) Timu yoyote hairuhusiwi kuruka ukuta na uzio wa ndani ya Uwanja. Endapo itafanya hivyo itatozwa faini ya sh. 500,000/=.

    (18) Pamoja na adhabu iliyoainishwa katika Kanuni ya 8 (14, 15, 16 na 17) TFF inaweza kutoa adhabu ikiwemo ya Timu husika kupoteza mchezo na kumfungia mchezaji, kiongozi, au shabiki yeyote wa timu husika kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu.

    (19) Mwalimu mkuu au mwalimu msaidizi wa timu anatakiwa kuwasilisha kwa Kamishina wakati wa kukaguliwa orodha iliyo na wachezaji 18 na viongozi watano ambao wameorodheshwa katika fomu maalumu iliyoandaliwa na TFF kwa madhumuni hayo. Formu hiyo italazimika kujazwa kwa unadhifu na ukamilifu.

    (20) Timu itatumia wachezaji walioorodheshwa katika fomu hiyo tu. Mchezaji ambaye hakuoorodheshwa hatahesabika kama mchezaji wa siku hiyo.

    (21) Wachezaji wote watatambulika kwa kutumia vitambulisho vyao vilivyoidhinishwa na TFF; katika mashindano hayo. Mchezaji yeyote ambaye hatakuwa na kitambulisho kutokana na sababu zisizokuwa na msingi atapiga picha akiwa na Mwamuzi na Kamisaa wa mchezo huo kwa gharama za kilabu kama ushahidi utakaopambanua utambulisho wake.

    (22) Iwapo itathibitika bila kujali kukatwa au kutokatwa Rufaa, kupitia taarifa za mchezo za Kamisaa ama kwa njia yoyote kuwa timu imechezesha mchezaji/wachezaji ambao si halali au ni batili kiusajili (non qualified) timu hiyo itapoteza mchezo na ushindi kupewa timu pinzani.
    (23) Timu ambayo itawasilisha fomu isiyo kamili itachukuliwa kuwa haijawasilisha fomu hiyo.

    (24) Endapo timu imeshindwa kuwasilisha fomu iliyotajwa katika Kanuni ya 8 (20) itakuwa imekiuka Kanuni hiyo na timu husika itatozwa faini ya Sh. 100,000/= ambazo zitalipwa kutokana na mchezo au michezo ya timu husika.

    (25) Wanaoruhusiwa kukaa kwenye benchi la wachezaji wa akiba ni wachezaji saba (7) wa akiba na viongozi watano (5) ambao ni mwalimu Mkuu, mwalimu Msaidizi, Daktari, Mchua misuli na Mtunza vifaa wa Timu.

    (26) Mwamuzi atalazimika kutoanzisha mchezo hadi masharti ya Kanuni ndogo ya (25) ya Kanuni hii yametekelezwa.

    (27) Endapo hata baada ya Mwamuzi kuitaka timu itekeleze masharti ya Kanuni ya 8 (25) timu husika ikashindwa kufanya hivyo; basi timu hiyo itatozwa faini ya sh. 500,000/=. Mwamuzi ataomba msaada wa wanausalama kuwaondoa wasiohusika kabla ya kuanzisha mchezo.

    (28) Mwamuzi na Kamishna wa mchezo wanatakiwa kutoa taarifa zao za maandishi kwa TFF, endapo hali iliyoelezwa katika Kanuni ndogo ya (27) ya Kanuni hii itatokea.

    (29) Chama cha Mpira cha ngazi husika kitapeleka kiwanjani mipira miwili au zaidi yenye sifa zinazokubalika kisheria itakayotumika kwa ajili ya mchezo. Kila timu inatakiwa kufika kiwanjani angalau na mpira mmoja wenye sifa hizo hizo.

    (30) Ni marufuku kwa timu yoyote kukataa kuchezea mpira wowote uliochaguliwa na mwamuzi.

    (31) Mwamuzi ataanzisha mchezo iwapo tu kama kuna mipira miwili au zaidi yenye sifa zinazokubalika kisheria.

    (32) Endapo timu yoyote itakataa kuchezea mpira wowote uliochaguliwa na mwamuzi na kusababisha mchezo huo kuvunjika, timu hiyo itapoteza mchezo huo na timu pinzani itapata ushindi wa pointi tatu na magoli matatu.
    (33) Endapo timu yoyote itakataa kuchezea mpira wowote uliochaguliwa na mwamuzi na kusababisha mchezo huo kuchelewa kuanza na baadaye mchezo ukalazimika kuvunjwa kabla ya dakika tisini (90) kwisha kwa sababu ya giza timu iliyosababisha mchezo kuvunjika itapigwa faini ya 500,000/=, itapoteza mchezo huo na timu pinzani itapata ushindi wa pointi tatu (3) na magoli mawili (2).

    (34) Mwamuzi ataanzisha mchezo iwapo kila timu ina wachezaji 11. Endapo timu yoyote haitimizi wachezaji 11, mchezo unaweza kuanzishwa ikiwa tu wachezaji wa kila timu hawapungui saba (7) mmoja wao akiwa mlinda mlango. Lakini Kanuni hii haitahusu timu iliyosalia na wachezaji pungufu ya saba kutokana na baadhi yao kuumia au kutolewa nje na mwamuzi wa mchezo.

    (35) Timu inaruhusiwa kubadilisha wachezaji watatu (3) tu wa akiba kutoka kwenye orodha ya wachezaji saba (7) wa akiba.

    (36) Timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu pamoja na waamuzi, endapo watapewa na mdhamini, jezi na suti za michezo, timu pamoja na waamuzi wanatakiwa wahakikishe wanavaa vifaa hivi kwenye michezo yote ya Ligi Kuu.

    (37) Iwapo kutakuwa na mdhamini wa ligi Kuu, Nembo ya mdhamini itawekwa kifuani.Wadhamini wengine wote nembo zao zitawekwa mgongoni na mikononi.Timu itakayokuwa na jezi zake italazimika kuweka nembo ya mdhamini katika jezi hizo kwa kufuata utaratibu huo na hairuhusiwi kuweka matangazo ya kampuni nyingine ambayo ina ushindani wa moja kwa moja kibiashara na mdhamini wa Ligi kuu.

    (38) Kila Kilabu kinalazimika kuheshimu Mikataba ya udhamini inayowekwa na TFF. Timu itakayoshindwa kutekeleza kipengele namba 36 na 37 cha kanuni hizi itatozwa faini isiyopungua 1,500,000/= kwa kila mchezo na pia inaweza kuchukuliwa hatua nyingine zaidi ikiwemo kuondolewa kwenye mashindano na/au kufungiwa.

    (39) Mwamuzi ambaye hatovaa jezi na suti ya michezo yenye nembo ya mdhamini ataondolewa katika orodha ya waamuzi wanaochezesha ligi kuu.

    (40) Kilabu chochote kinachotaka kuingia mkataba na mdhamini kinalazimika kuwasilisha rasimu ya mkataba huo kwa TFF kabla ya kutia sahihi.

    (41) Timu itakayokosa kufika uwanjani na kusababisha mchezo kutofanyika baada ya kushiriki kikao cha maandalizi ya mchezo, itatozwa faini ya shilingi 5,000,000/=, kulipa fidia ya uharibifu wowote unaoweza kijitokeza na viongozi waliosababisha watachukuliwa hatua zaidi za kinidhamu.
    KANUNI YA 9
    KUAHIRISHA MCHEZO

    Mchezo unaweza kuahirishwa kutokana na sababu yoyote kati ya zifuatazo:-
    (a) Endapo timu ina wachezaji watano au zaidi katika timu ya Taifa;

    (b) Endapo timu inashiriki katika mashindano ya Kimataifa na ina muda usiozidi siku sita kufikia mchezo wa Kimataifa;

    (c) Sababu yoyote ya dharura nzito na yenye msingi itakayokubaliwa na TFF.

    (d) Mchezo wowote ulioahirishwa utapangwa tena katika tarehe itakayoamuliwa na TFF isipokuwa kama ni dharura ya mvua au dharura yoyote nyingine basi mchezo huo utachezwa siku inayofuata iwapo ratiba inaruhusu.

    (e) Iwapo mchezo ulishaanza na kuvunjika kwa sababu ya mvua au dharura yoyote nyingine; magoli yaliyofungwa katika mchezo huo yataendelea kuwekwa katika idadi ya magoli yaliyofungwa na wachezaji binafsi lakini si katika idadi ya magoli ya timu. Kadhalika kadi walizoonyeshwa wachezaji katika mchezo ulioahirishwa au uliovunjika zitaendelea kuhesabika.

    (f) Taarifa ya maombi ya kuahirisha mchezo ni lazima itolewe kwa maandishi si chini ya siku 14 kabla ya siku ya mchezo, isipokuwa kwa sababu zilizo nje ya uwezo wa binadamu.

    KANUNI YA 10
    WAAMUZI

    1. Katika mchezo wowote Uamuzi wa Mwamuzi wa mchezo ni wa mwisho.

    2. Kila Mwamuzi atawasilisha TFF ngazi husika mara tu baada ya mchezo taarifa ya mchezo aliouchezesha iliyojazwa katika fomu maalum katika muda usiozidi saa 24.

    3. Taarifa ya Mwamuzi iliyotajwa katika Kanuni ya 10 (2) inatakiwa ijazwe kwa unadhifu na ukamilifu.

    4. Mwamuzi atakayeshindwa kutoa taarifa sahihi ya mchezo kwa mujibu wa Kanuni ya 10 (2) ataondolewa katika orodha ya waamuzi wanaochezesha Ligi kuu na/au atafungiwa kwa muda usiozidi miezi kumi na mbili (12).

    5. Waamuzi wa mchezo watapangwa na TFF na klabu chochote hakiruhusiwi kumkataa mwamuzi yeyote.

    6. Waamuzi watakaochezesha Ligi ni wale wa Daraja la FIFA na Daraja la kwanza waliofaulu “Physical Test” na kuteuliwa kuchezesha ngazi ya Ligi Kuu.

    7. Kutafanyika “Physical Test” kila mwaka kabla ya Ligi kuanza ikiambatana na mtihani wa kuandika na mahojiano.

    SURA YA NNE
    KANUNI YA 11
    HUDUMA YA KWANZA NA BIMA

    Chama cha Mpira ngazi husika ni lazima kihakikishe kuwa katika mchezo wowote wa Ligi Kuu panakuwepo huduma ya kwanza na gari la wagojwa, kadhalika kihakikishe katika kila mchezo kunakuwepo na Daktari.

    KANUNI YA 12
    BIMA

    (1) Viongozi na wachezaji wote lazima wawekewe bima na vilabu vyao. Kilabu kitakachokiuka Kanuni hii hakitashirikishwa katika michuano yoyote inayosimamiwa na TFF.

    (2) Chama cha Walimu wa Mpira wa Miguu (TAFCA) kihakikishe kwamba wanachama wake wanawekewa Bima na Vilabu husika.

    (3) Chama cha Madaktari wa Michezo Tanzania (TASMA) kihakikishe kwamba wanachama wake wanawekewa Bima na Vilabu husika.

    SURA YA TANO
    KANUNI YA 13
    ADA YA USHIRIKI NA USIMAMIZI WA LIGI

    1. Ada ya ushiriki wa Ligi Kuu ni TShs 300,000/=.

    2. Kutakuwa na fomu za maombi ya kushiriki kwenye Ligi, tarehe ya mwisho kuthibitisha itatangazwa na TFF. Maombi hayo yataambatana na ada ya ushiriki, maombi yasiyo ambatana na ada hayatapokelewa. Klabu itakayoshindwa kuthibitisha kushiriki hadi kufikia tarehe ya mwisho ya kufanya hivyo itakuwa imejiondoa yenyewe kwenye Ligi na kujishusha daraja.

    KANUNI YA 14
    USIMAMIZI WA LIGI

    1. Ligi kuu itasimamiwa na Kamati ya utendaji ya TFF ambayo inaweza ikakasimu madaraka ya usimamizi kwa Kamati ya Mashindano.

    SURA YA SITA
    KANUNI YA 15
    RUFANI NA UTARATIBU WAKE

    Rufaa zote zinazohusiana na Ligi Kuu zitasikilizwa na:
    (1) Kamati ya nidhamu ya TFF:- Iwapo mrufani au mrufaniwa hataridhika na maamuzi ya kamati ya Nidhamu, atakata rufaa kwa Kamati ya rufaa ya TFF.

    (2) Kamati za nidhamu na rufaa zitasikiliza rufaa zote zinazohusu mashindano haya na ufundi.

    (3) Ni marufuku kupeleka malalamiko yoyote dhidi ya TFF kwa masuala yahusuyo soka katika mahakama za sheria. Klabu au mtu yeyote atakayepeleka malalamiko yake katika mahakama za sheria atachukuliwa hatua kali ikiwamo kufutwa kabisa kujishughulisha na mchezo wa soka.
    KANUNI YA 16
    UTARATIBU WA KUKATA RUFANI

    (a) Rufani ya kupinga matokeo ya mchezo iwasilishwe kwa maandishi kwa Kamishna wa mchezo au ofisi ya TFF sio zaidi ya masaa 24 baada ya mchezo kumalizika na iwe imeambatanishwa na ada ya rufaa.

    (b) Kamishna wa mchezo atawasilisha kwenye Sekretarieti ya TFF sio zaidi ya saa ishirini na nne (24) tangu kupokea rufaa hiyo.

    (c) Kamati husika itaketi kusikiliza na kuitolea uamuzi Rufaa hiyo baada ya kupata vielelezo husika na wajumbe wa Kamati hiyo kukamilika. Mkata rufaa atawasilisha vielelezo kuhusu rufaa yake, rufaa isiyokuwa na vielelezo na ambayo haijalipiwa ada itatupwa.

    (d) Muda wa kukata rufaa kwenye Kamati ya Rufaa iwapo mrufani au mrufaniwa hajaridhika na mamuzi ya Kamati ya Nidhamu ni si zaidi ya siku tano za kazi.

    (e) Rufani yoyote itakayowasilishwa baada ya muda uliowekwa chini ya kanuni hii, haitasikilizwa na ada ya rufaa haitarudishwa kwa mrufani.

    KANUNI YA 17
    ADA ZA RUFAA

    (a) Rufaa yoyote itakayokatwa kwa Kamati ya Nidhamu inatakiwa ilipiwe ada ya TShs 300,000/= na

    (b) Kamati ya Rufaa ni TShs 500,000/=

    SURA YA SABA
    KANUNI YA 18
    MGAWANYO WA MAPATO

    1. Kila timu itajihudumia yenyewe, timu zilizocheza zitagawana asilimia 50 ya mapato ya mchezo.
    2. Mgawanyo wa mapato ya mchezo utakuwa kama ifuatavyo:-
    Jichangie Jumla ya pato xxxx
    Toa: Nauli na Posho ya waamuzi na kamisaa xxxx
    Gharama za Tiketi xxxx
    -------
    Baki ya Pato xxxx
    10% Gharama za mchezo; xxxx
    (Isizidi 5,000,000/=)
    15% TFF (T); xxxx
    10% FDF; xxxx
    10% Uwanja; xxxx
    1% B.M.T; xxxx
    4% FAT (M) xxxx
    25% Klabu ngeni xxxx
    25% klabu mwenyeji xxxx

    3. Endapo timu moja itahamia uwanja wa Mkoa mwingine mbali ya ule wa nyumbani sehemu ya mapato ya 4% ya Chama cha Mpira cha Mkoa itagawanywa kama ifuatavyo:
    (a) Mkoa unaotoka timu husika utapata nusu ya 4%
    (b) Mkoa utakaohusika na uwanja utapata nusu ya 4%

    4. Msimamizi wa Kituo atawasilisha taarifa ya mapato na fedha za mchezo husika kwa TFF katika muda usiozidi masaa 24. Kiongozi au Msimamizi atakayeshindwa kuwasilisha atachukuliwa hatua kwa mujibu wa Kanuni za TFF. Bila kuathiri kanuni hizi Chama cha Mpira ngazi husika kinaweza kuanzisha mfuko/mchango wowote kwa maendeleo ya mpira wa miguu.

    5. ( i) Gharama za Waamuzi na kamisaa ni nauli ya kutoka kwenye Kituo alichotokea,
    usafiri wa treni Daraja la Pili, Basi au Meli.
    (ii) Usafiri wa ndani wa Waamuzi kwa ujumla wao Sh. 10,000/= na kamisaa 10,000/=.
    (iii) Chakula na malazi 30,000/= kwa kila mwamuzi na kamisaa.
    (iv) Mwamuzi wa mezani atalipwa Sh. 30,000/=.
    (v) Kamisaa atalipwa posho ya mchezo Sh. 90,000/=
    (vi) Mwamuzi na wasaidizi wawili (2) watalipwa posho ya mchezo Sh. 80,000/= kwa kila mmoja.
    (vii) Posho hizi zitalipwa kutoka katika mapato ya mchezo.

    KANUNI YA 19
    GHARAMA ZA MCHEZO
    1. Asilimia 10% ya gharama za mchezo itatumika kulipia gharama zifuatazo:-
    (i) Gharama za msimamizi wa kituo.
    (a) Msimamizi kutoka nje ya kituo atalipwa gharama za kula na kulala 30,000/= na nauli kutoka kituo chake na kurudi.
    (ii) Malipo ya ulinzi, ball boys, huduma ya kwanza, vinywaji, wasimamizi, wauzaji na wachanaji tiketi, matangazo na stationery.
    (iii) Malipo ya TAFCA na FRAT 10,000/= kila kimoja.

    2. Mtiririko wa gharama hizo utaonyeshwa kwenye Fomu ya Mapato, msimamizi wa kituo tawajibika
    na usimamizi wa gharama za mchezo.
    3. Malipo yatalipwa kwa hundi kama Kanuni za fedha zinavyosema isipokuwa Waamuzi na
    Makamisaa.

    4. Iwapo gharama halisi ni pungufu ya 10% zilizokatwa kama gharama za mchezo, fedha zitakazobaki zitagawanywa nusu kwa nusu kati ya vilabu na TFF, yaani TFF itachukua 50% na vilabu vitagawana 50% nyingine. Mgawanyo wa fedha hizi unatakiwa uandikwe kwenye fomu ya gharama za mchezo isainiwe na msimamizi wa kituo kwa niaba ya TFF na wawakilishi wa vilabu kwa niaba ya vilabu vyao.

    SURA YA NANE
    KANUNI YA 20
    KUJITOA KATIKA LIGI

    (1) Endapo Kilabu chochote kina nia ya kujitoa katika Ligi kwa sababu zozote zile za msingi ni lazima itoe taarifa ya maandishi kwa TFF kikieleza sababu zinazokilazimisha kilabu hicho kijitoe, siku thelathini kabla ya ligi kuanza.

    (2) Endapo TFF imekubali kujitoa kwa kilabu chochote, klabu kingine ambacho awali kilikuwemo katika Daraja hilo lakini kiliteremka kwa mujibu wa msimamo wa Ligi, kitarudishwa kuziba pengo. Kilabu hicho ni kile kilicho katika nafasi ya juu kuliko vilabu vingine vyote vilivyoteremka Daraja katika msimu huo.

    (3) Kilabu kilichojitoa kitateremka Daraja.

    (4) Kilabu chochote kitakachojitoa katika Ligi baada ya Ligi kuanza au kushindwa kucheza michezo miwili katika msimu mmoja wa Ligi kitakabiliwa na adhabu zifuatazo:
    (a) Kitateremka daraja na kufungiwa kucheza Ligi kwa misimu 2. Kamati ya Utendaji ya TFF pia inaweza kukichukulia hatua zaidi klabu hicho/viongozi au wachezaji iwapo itathibitika kuwa kimejitoa kwa madhumuni ya kuhujumu msimamo wa Ligi au hujuma nyingine yoyote.

    (b) Iwapo klabu zitakazojitoa au kushindwa kumaliza Ligi kwa sababu yoyote ile zitakuwa ni zaidi ya tatu (3) kama kanuni za Ligi za timu kushuka daraja zinavyosema; timu zote hizo zitashuka daraja na na timu zaidi zitapanda kutoka daraja la kwanza ili kujaza nafasi na idadi ya timu za Ligi kuu kuendelea kuwa 12.

    (c) Matokeo ya michezo yote iliyowahi kuchezwa yatafutwa lakini kitakuwepo kwenye orodha ya msimamo wa ligi.

    (d) Magoli yaliyofungwa na wachezaji wa timu iliyojitoa katika ligi yatafutwa na hivyo wachezaji wake hawataweza kushindana katika ufungaji bora hata kama walifunga magoli mengi lakini magoli yaliyofungwa na wachezaji wa timu pinzani dhidi ya timu iliyojitoa kwenye ligi hayatafutwa na hivyo yataendelea kuonekana katika idadi ya magoli yaliyofungwa na wachezaji hao lakini hayataonekana katika idadi ya magoli yaliyofungwa na klabu zao

    ANUNI YA 21
    KUTOFIKA KITUONI

    Timu yoyote itakayokosa kufika kituoni na kusababisha mchezo usifanyike itakabiliwa na adhabu zifuatazo:
    (a) Itapoteza ushindi na timu pinzani itapata ushindi wa pointi tatu na magoli matatu;

    (b) Itatozwa faini ya TShs 3,000,000/= ambazo kati ya hizo Tshs 1,500,000/= itaenda TFF na TShs 1,500,000/= itaenda kwa timu pinzani.

    (c) Itapoteza haki ya kuchukua sehemu yake ya mapato ya mchezo huo.

    (d) Kiongozi yeyote atakayebainika .kuwa alishiriki, alishawishi au alikuwa chanzo cha mgomo huo atafungiwa kwa kipindi cha miezi kumi na miwili.

    (e) Inaweza ikakabiliwa na adhabu zaidi kama ambavyo Kamati ya Utendaji itaona inafaa.

    (f) Timu yoyote iliyopewa adhabu ya faini chini ya aya ya (b) ya Kanuni hii haitaruhusiwa kucheza mchezo unaofuata hadi itakapotekeleza adhabu hiyo. Endapo ni mchezo wa mwisho wa msimu, timu hiyo haitaruhusiwa kucheza katika msimu unaofuata mpaka itekeleze adhabu hiyo.


    KANUNI YA 22
    KUVURUGA MCHEZO

    1. Timu itakayosababisha mchezo kuvurugika kwa namna yoyote ile na hatimaye kuvunjwa, itapoteza mchezo huo hata kama ilikuwa inaongoza kwa magoli na timu pinzani itapewa ushindi wa pointi tatu na magoli matatu, iwapo timu pinzani inaongoza kwa magoli zaidi ya mawili, itabakia na idadi ya magoli hayo iliyokwishafunga.

    2. Magoli yaliyofungwa na wachezaji wa timu iliyosababisha mchezo kuvunjika yatafutwa lakini magoli yaliyofungwa na timu pinzani hayatofutwa na yataendelea kuonekana katika idadi ya magoli yaliyofungwa na wachezaji wa timu hiyo wakati wa kutafuta mfungaji bora.

    3. Endapo itatokea vurugu ya aina yoyote ile na kusababisha mchezo kusimama, mwamuzi atasubiri kwa dakika zisizozidi kumi na tano, na endapo hali ya vurugu bado inaendelea mwamuzi atavunja mchezo na kuwasilisha taarifa ya mchezo kwa kamati ya Usimamizi ya ngazi husika.

    4. Timu iliyosababisha vurugu itapoteza mapato yote ya mchezo.

    5. Timu iliyosababisha kuvurugika kwa mchezo italipa faini ya TShs 500,000/=.

    6. Faini hiyo italipwa kabla ya mchezo unaofuatia.

    7. TFF inaweza ikatoa adhabu nyingine zaidi iwapo itaona kuna haja ya kufanya hivyo, mathalani iwapo itathibitika kuwa timu imevuruga mchezo kwa makusudi kwa madhumuni ya kuikosesha timu pinzani ushindi mkubwa zaidi.

    KANUNI YA 23
    KUPANGA MATOKEO

    1. Endapo timu zozote zitabainika kuwa zimepanga kwa namna yoyote ile matokeo ya mchezo wowote waliocheza kwa madhumuni yoyote yale zitachukuliwa hatua zifuatazo:-

    2. Matokeo ya mchezo huo yatafutwa; na kila timu itatozwa faini ya shilingi millioni tano (5,000,000/=)

    3. Zitateremshwa hadi ligi ya wilaya;

    4. Viongozi wa timu hizo waliohusika na njama za kupanga matokeo watafungiwa kwa kipindi cha miaka mitano;

    5. Iwapo timu husika itashindwa kulipa faini basi timu hiyo haitapangwa katika mchezo wa ligi msimu unaofuata..

    SURA YA TISA
    UDHIBITI WA MIENENDO NA ADHABU KWA WACHEZAJI, WAAMUZI NA VIONGOZI

    KANUNI YA 24
    UCHEZAJI WA KIUNGWANA (FAIR PLAY)

    Wachezaji wanatakiwa kuzingatia kanuni za mchezo wa kiungwana ‘fair play’ ndani na nje ya uwanja wa mchezo. Kanuni 10 za FIFA za mchezo wa kiungwana ni kama ifuatavyo:

    i. Cheza Kiungwana – Ushindi hauwezi kuwa na thamani iwapo umepatikana katika njia isiyo halali au kwa udanganyifu. Kudanganya ni rahisi lakini haileti raha ya ushindi. Kucheza kiungwana inahitaji moyo na tabia njema. Pia hufurahisha zaidi. Mchezo wa kiungwana siku zote una malipo yake hata kama utapoteza mchezo. Kucheza kiungwana kunakujengea heshima wakati kudanganya kunaleta aibu. Kumbuka kuwa mpira wa miguu ni mchezo na mchezo wowote hauwezi kuwa na maana kama hautochezwa kiungwana kwa kuzingatia kanuni na taratibu ili mshindi halali aweze kupatikana.

    ii. Cheza kwa nia ya kutafuta ushindi lakini pia kuwa tayari kukubali kushindwa – Kushinda ndiyo lengo la kushiriki katika mchezo wowote ule. Siku zote usijiandae kushindwa. Iwapo huchezi kwa nia ya kushinda utakuwa unawadanganya wapinzani wako, unawadhulumu watazamaji na pia unjifanya mwenyewe kuwa ni mjinga. Usikate tamaa hata siku moja unapombana na wapinzani wenye nguvu zaidi lakini pia usidharau hata siku moja unapombana na wapinzani dhaifu. Ni kumkosea adabu mpinzani unapocheza chini ya kiwango chako. Cheza kwa nia ya kutafuta ushindi hadi dakika ya mwisho lakini kumbuka hakuna anayeshinda wakati wote. Siku nyingine utashinda na siku nyingine utashindwa. Jifunze kukubali kushindwa. Usitafute visingizio unapofungwa. Sababu za kweli siku zote zitadhihirika. Wapongezi washindi bila kinyongo. Usilaumu waamuzi wala mtu mwingine yoyote. Jizatiti kufanya vizuri zaidi wakati mwingine. Walioshindwa na kukubali wanapata heshima zaidi kuliko washindi wanaolazimisha.

    iii. Heshimu sheria za mchezo – Michezo yote inalindwa na sheria. Bila sheria itakuwa ni vurugu tupu. Sheria za mpira wa miguu ni nyepesi na rahisi kujifunza. Hakikisha unajifunza; itakusaidia kuufahamu mpira wa miguu vizuri zaidi. Kuufahamu mchezo zaidi itakufanya uwe mchezaji bora zaidi. Pia ni muhimu kufahamu madhumuni ya sheria zilizowekwa. Zimekusudiwa kuufanya mchezo uwe na ladha katika kuucheza na pia uwe na ladha katika kuuangalia. Kwa kufuata sheria, mchezo wa mpira wa miguu utakuwa na burudani zaidi.

    iv. Heshimu wapinzani, wachezaji wenzako, waamuzi, viongozi na watazamaji – Mchezo wa kiungwana unamaanisha kuheshimu wapinzani. Bila ya wapinzani kutakuwa hakuna mchezo. Kila mmoja ana haki sawa, ikiwemo haki ya kuheshimiwa. Wachezaji wa timu moja ni wenza. Tengeneza timu ambayo kila mmoja kwenye timu atakuwa na haki sawa. Waamuzi wapo kuhakikisha nidhamu na mchezo wa kiungwana unadumishwa. Siku zote kubali maamuzi yao bila ya ulalamishi, na wasaidie waweze kuwafanya washiriki wote waufurahie zaidi mchezo. Viongozi pia ni sehemu ya mchezo na wanatakiwa wapewe heshima wanayostahili. Watazamaji wanaufanya mchezo uwe na msisimko. Wanahitaji kuuona mchezo ukichezwa kiungwana kwa kuzingatia kanuni, lakini pia wanatakiwa kuwa waungwana na kujiheshimu.

    v. Dumisha Maslahi ya mchezo wa mpira wa miguu – Mpira wa miguu ndiyo mchezo unaoongoza duniani. Lakini siku zote unahitaji msaada wa kila mmoja kuufanya uendelee kuwa mchezo wenye kupendwa zaidi. Fikiria maslahi ya mpira kabla ya maslahi yako mwenyewe. Fikiria ni vipi vitendo vyako vinaweza vikaupaka matope mchezo wa mpira wa miguu. Zungumzia mambo mazuri ya mchezo wa mpira wa miguu. Shawishi watu wengine kuuangalia na kuucheza kiungwana. Wasaidie wengine kupata brudani ya kutosha katika mchezo wa mpira wa miguu kama unayoipata wewe. Kuwa balozi wa mchezo wa mpira.

    vi. Waheshimu wale wanaolinda heshima ya mchezo wa mpira wa miguu – Jina zuri la mchezo wa mpira wa miguu limeendelea kudumu kwa sababu idadi kubwa ya watu wenye kuupenda mchzo huu ni wakweli na waungwana. Wakati mwingine mtu hufanya jambo kubwa ambalo linastahili tulitambue. Watu kama hawa wanastahili kutuzwa na mambo mema waliyofanya yatangazwe. Hii itashawishi wengine kuiga mifano yao. Saidia kuendeleza mpira wa miguu kwa kuyatangaza mazuri yake.

    vii. Kataa rushwa, madawa, ubaguzi, fujo, kamari na mambo mengine ya hatari kwa mchezo wetu – Umaarufu mkubwa wa mchezo wa mpira wa miguu wakati mwingine huufanya uwe rahisi kuathiriwa na mambo mabaya ya nje. Jichunge na vishawishi vitakavyokufanya ushawishike kushiriki kwenye kudanganya au kutumia madawa yaliyokatazwa. Madawa yaliyokatzwa hayana nafasi katika soka, mchezo mwingine wowote na jamii kwa jumla. Sema hapana kwa madawa ya kulevya. Saidia kuupiga teke ubaguzi kwenye soka. Wachukulie wachezaji wote na wengineo kuwa ni sawa bila kujali dini zao, kabila, jinsia au utaifa wao. Usivumilie hata kidogo kamari katika michezo unayoshiriki. Inaporomosha kiwango chako cha uchezaji na inasababisha hali ya mgongano wa maslahi. Thibitisha kuwa soka haihitaji fujo, hata kutoka kwa washabiki wako wenyewe. Soka ni mchezo na michezo huleta amani.

    viii. Wasaidie wengine kupambana na mashinikizo ya upokeaji rushwa – Wakati mwingine unaweza kusikia wachezaji wenzako au watu wengine unaowafahamu wanashawishiwa wadanganye kwa njia moja au nyingine au washiriki ktika vitendo visivyokubalika katika mchezo wa soka. Wanahitaji msaada wako. Usisite kusimama upande wao. Wape nguvu ya kukataa vishawishi. Wakumbushe wajibu wao kwa wenzao na kwa mchezo wenyewe. Tengeneza umoja wenye mshikamano, kama ngome ngumu kabisa kwenye mchezo wa soka.

    ix. Wabainishe wale wanaojaribu kuuchafua mchezo wetu – Usione aibu kusimama dhidi ya yoyote yule ambaye una hakika anashawishi wengine kudanganya au kushiriki katika vitendo vingine visivyokubalika. Ni vyema kuwafichua waovu wote ili waweze kuondolewa kabla ya kuleta madhara. Ni uovu kushirikiana na watu waovu. Usiseme tu hapana, wafichue wanaotaka kuichafua soka kabla hawajafanikiwa kuwashawishi wengine.

    x. Tumia soka kujenga dunia bora zaidi – Soka ina nguvu ya ajabu ambayo inaweza kutumika kuifanya dunia hii ikawa sehemu bora zaidi ya kuishi. Tumia nguvu hii kudumisha amani, usawa, afya na elimu kwa wote. Ifanye soka iwe bora zaidi, ipeleke kwa jamii na utakuwa unajenga dunia bora zaidi.


    Pamoja na kanuni za Fair Play za FIFA, kadhalika wachezaji wanatakiwa kuzingatia yafuatayo:
    a) Nidhamu – kudumisha tabia njema nje ya uwanja na wakati wote wa mchezo kwa kucheza bila ya kuwaumiza au kuhatarisha usalama wa wachezaji wa timu pinzani.

    b) Mchezo wa kiungwana – Kutodanganya kuumia au kufanyiwa rafu, kutotumia mbinu zisizo za kiungwana mchezoni au kujiingiza katika vitendo visivyokuwa vya kiunamichezo kama vile kutukana kwa maneno, ishara au kujihusisha na vitendo vyovyote vya kibaguzi.

    c) Kutorejeshea – kutorejeshea ‘retaliation’ iwapo mchezaji atafanyiwa rafu au kukashifiwa.

    d) Malalamiko – Ni nahodha pekee ambaye anaruhusiwa kuzungumza na waamuzi. Iwapo patatokea malamiko yoyote wakati wa mchezo wachezaji wengine wote wanatakiwa wawe hatua zisizopungua kumi kutoka kwa mwamuzi.

    e) Kumheshimu Kocha – Mchezaji wakati wote anatakiwa atii maagizo ya kocha wake. Mchezaji anatakiwa akubali kubadilishwa uwanjani na kuadhibiwa kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu au visivyokuwa vya kiuanamichezo.

    f) Kumheshimu nahodha – Mchezaji anatakiwa amheshimu na atii maagizo ya nahodha wake nje na ndani ya uwanja hususan katika masuala yahusuyo timu na tabia njema kwa jumla.

    g) Kuheshimu wachezaji – Mchezaji anatakiwa awaheshimu wachezaji wenzake na awatie hamasa nje na nadani ya uwanja. Mchezaji anatakiwa asimkashifu mchezaji mwenzake mwenye kufanya makosa.

    h) Kuheshimu wapinzani – Mchezaji anatakiwa awape wachezaji wa timu pinzani heshima yao, awe tayari kutoa msaada kwa mchezaji aliyeumia na kushikana mikono kabla na baada ya mchezo.

    i) Kuheshimu waamuzi – Mchezaji anatakiwa wakati wote kuheshimu maamuzi ya waamuzi na kutozozana nao au kutumia lugha ya matusi au kashfa dhidi yao.

    j) Kujiheshimu mwenyewe – Mchezaji anatakiwa ajiheshimu mwenyewe na ajitunze na asitumie madawa yaliyokatazwa.

    KANUNI YA 25
    UDHIBITI WA WACHEZAJI
    (1) TFF itadhibiti mienendo ya wachezaji kwa kuchukua hatua kama ifuatavyo:-
    (a) Mchezaji atakayetolewa nje kwa kadi nyekundu baada kupata kadi mbili za njano katika mchezo wa ligi hataruhusiwa kucheza mchezo mmoja unaofuata wa timu yake.

    (b) Mchezaji atakayetolewa nje kwa kadi nyekundu ya mojakwamoja (straight red) atakosa michezo miwili.

    (c) Mchezaji atakayeonywa kwa kadi ya njano katika michezo mitatu hataruhusiwa kucheza mchezo mmoja unaofuata.

    (d) Kilabu zinatakiwa zitunze kumbukumbu za wachezaji wake waliyoonyeshwa kadi. Kilabu itakayomchezesha mchezaji mwenye kadi 3 za njano au kadi nyekundu itapoteza mchezo na timu pinzani itapewa ushindi wa pointi 3 na magoli 3, halikadhalika mchezaji antakiwa atunze kumbukumbu zake za kadi na iwapo atacheza akiwa anatakiwa kutocheza kwa ajili ya kadi tatu za njano au kadi nyekundu timu yake itapoteza mchezo.

    (e) Mchezaji yeyote atakayempiga mchezaji mwenzake au kiongozi yeyote kabla, wakati au baada ya mchezo aatafungiwa kucheza mpira kwa kipindi cha miezi 3 – 12 au atafungiwa kucheza idadi ya michezo ambayo kamati ya utendaji itaona inafaa au atalipa faini kama itakavyopangwa na kamati ya utendaji au vyote kwa pamoja.

    (f) Mchezaji yeyote atakayefanya jambo lolote kati ya haya yafuatayo ataadhibiwa kwa kufungiwa kwa kipindi kisichopungua miezi 3 – 12, kufungiwa kucheza michezo kadhaa, kupigwa faini kwa mujibu wa kanuni ya 31, au vyote kwa pamoja:
    (i) Kukataa kujiunga na Timu ya Taifa kwa visingizio vyovyote vile.

    (ii) Kupigana kabla au mara tu baada ya mchezo kumalizika.

    (iii) Kumshambulia mwamuzi au kiongozi yoyote kwa namna yoyote ile, iwe kwa matusi au kwa kumgusa.

    (iv) Kufanya kitendo chochote cha aibu, kama vile kukojoa kiwanjani, kutoa matusi au kuonyesha ishara yoyote inayoashiria matusi;

    (v) Kusababisha kuvurugika kwa amani kiwanjani kabla au baada ya mchezo;

    (vi) Kufanya vitendo vyenye kuonyesha imani za ushirikina au uchawi hadharani; na

    (vii) Kufanya kitendo chochote kinyume cha maadili ya mchezo wa mpira.

    (viii) Timu yoyote itakayomchezesha mchezaji aliye chini ya adhabu kwa mujibu wa Kanuni hii itapoteza mchezo huo na timu pinzani itapewa ushindi.

    (ix) Mchezaji yoyote atakayetakiwa kufanya vipimo vya dawa za kulevya au kuongeza nguvu, anawajibika kufanya hivyo, endapo atakataa kufanya hivyo atafungiwa kwa kipindi cha miezi kumi na mbili (12).

    KANUNI YA 26
    UDHIBITI NA ADHABU KWA WAAMUZI

    1. Mwamuzi yeyote atakayefanya jambo lolote kati ya haya yafuatayo ataadhibiwa kama
    ilivyoainishwa katika Kanuni hii:-
    (a) Akishindwa kumudu mchezo kwa uzembe, woga au kutozingatia sheria kiasi cha kuvuruga mchezo, kuhatarisha amani, atafungiwa kwa kipindi kisichopungua miezi sita (6) na kisichozidi miezi kumi na miwili (12).

    (b) Akichelewa kwa zaidi ya saa ishirini na nne (24) kutuma taarifa ya mchezo bila sababu za msingi ataadhibiwa kwa mujibu wa kanuni ya 10 kipengele cha 4.

    (c) Akibainika kuwa anadai hongo au amepokea hongo /au akitoa taarifa yenye mazingira ya hongo atafungiwa maisha.

    (d) Akibainika kuwa ameshawishi kupangiwa mchezo atafungiwa kwa kipindi kati ya miezi 3 – 12.
    (e) Akishindwa kufika au akichelewa kufika bila sababu ya msingi au kutotoa taarifa, kwenye kituo cha mchezo alichopangiwa kiasi cha kusababisha ratiba ya waamuzi kurekebishwa au mchezo kuahirishwa, ataondolewa kwenye orodha ya waamuzi na atafungiwa kwa kipindi kati ya miezi 3 - 12.

    (f) Akishindwa kutoa taarifa ya kutofika kwake kwenye kituo alichopangiwa kwa sababu ya dharura yoyote aliyoipata, na hivyo kusababisha mabadiliko yanayostahili kushindwa kufanyika, atafungiwa kwa kipindi kisichozidi miezi sita.

    (g) Akifanya kitendo chochote ambacho ni kinyume cha maadili ya taaluma ya uamuzi atafungiwa maisha.

    (h) Mwamuzi atakayemaliza mchezo kabla ya wakati bila ya sababu za msingi atafungiwa kati ya miezi 6 – 12.

    (i) Mwamuzi atakaebainika kushirikiana na Kamisaa kuandika taarifa ili kuficha ukweli ataondolewa katika orodha ya waamuzi wa Ligi Kuu na atafungiwa kwa kipindi kisichopungua miezi 24.

    KANUNI YA 27
    UDHIBITI WA KAMISHINA

    (a) Kamishna atakayeshindwa kutoa taarifa ya mchezo au akitoa taarifa ya uongo, ataondolewa kwenye orodha ya makamishna wa michezo na atafungiwa kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja.

    (b) Kamishna atakayeshindwa kutoa taarifa katika muda wa saa 24 ataondolewa katika orodha ya makamishna wa michezo na/au atafungiwa kwa kipindi kisichopungua miezi sita (6).

    (c) Kamishna atakayebainika kukataa kupokea Rufaa kwa sababu zisizokuwa za msingi kwa njia yoyote ile, atafungiwa kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja.

    (d) Akibainika kuwa anashawishi kupangiwa mchezo atafungiwa kwa kipindi kati ya miezi mitatu (3) hadi kumi na mbili (12).

    (e) Kamisaa atakaye bainika kushirikiana na mwamuzi kuandika taarifa ili kuficha ukweli ataondolewa katika orodha ya Makamisaa na atafungiwa kwa kipindi kisichopungua miezi 24.

    (f) Kamisaa atayebainika kuendesha kikao cha matayarisho na viongozi wa timu wasiohusika (kanuni 8(3)) ataondolewa kwenye orodha ya makamisaa.

    KANUNI YA 28
    UDHIBITI WA WAALIMU

    Mwalimu yeyote atakayefanya jambo lolote kati ya haya yafuatayo ataadhibiwa kwa mujibu wa Kanuni hii:-
    (a) Akimshambulia mwamuzi, mchezaji au kiongozi yeyote, kwa maneno au vitendo, kabla, wakati au baada ya mchezo, atatozwa faini isiyopungua shilingi laki tano (500,000/-) na/au kufungiwa kwa kipindi kati ya miezi 3 – 12, bila ya kujali adhabu yoyote iliyotolewa na mwamuzi kiwanjani.

    (b) Akitoa kauli au ishara inayoashiria au kushawishi shari kabla, wakati au baada ya mchezo atatozwa faini isiyopungua laki tano (500,000/=) na/au kufungiwa kwa kipindi cha kati ya miezi mitatu (3) hadi kumi na mbili (12).

    (c) Akijishirikisha na vitendo vyovyote vile vinavyoashiria imani za uchawi au ushirikina atatozwa faini isiyozidi shilingi laki tatu (300,000/=) na/au kufungiwa kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu.

    (d) Akibainika kujihusisha na vitendo vya kutoa hongo kwa Waamuzi au wachezaji wa timu pinzani atafungiwa kufundisha mpira maisha.

    (e) Akibainika kugushi sahihi ya mchezaji au kufanya tendo lolote kwa lengo la kukamilisha zoezi la usajili kwa udanganyifu atafutwa katika ordha ya waalimu, leseni yake itatwaliwa na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

    (f) Pamoja na adhabu zilizoanishwa kwenye Kanuni hii, TFF inaweza kuongeza au kupunguza adhabu zilizotajwa kama kuna haja ya kufanya hivyo au kutoa adhabu ya faini ya kiwango ambacho TFF inaona itafaa.

    (g) Mwalimu atakayebainika kusababisha timu kutofika uwanjani na kukosa mchezo, baada ya kuhudhuria kikao cha maandalizi, atatozwa faini ya shilingi 1,000,000/= na kufungiwa kwa kipindi kisichopungua miezi kumi na mbili (12).

    KANUNI YA 29
    UDHIBITI WA VIONGOZI

    1. Kiongozi yeyote atakayefanya jambo lolote kati ya haya yafuatayo, Ataadhibiwa kwa mujibu wa
    Kanuni hii:-
    (a) Akibainika kujihusisha na vitendo vya kushawishi au kutoa hongo kwa Waamuzi au wachezaji wa timu pinzani atafungiwa maisha;

    (b) Akimshambulia Mwamuzi, mchezaji au kiongozi mwingine yoyote, kwa maneno au vitendo, kabla, wakati au baada ya mchezo atafungiwa kwa kipindi kisichozidi miezi sita.

    (c) Akifanya kitendo chochote kinachoashiria imani ya uchawi atafungiwa kwa kipindi cha miezi sita.

    (d) Akifanya kitendo chochote kinyume cha maadili ya mchezo atafungiwa kwa kipindi kisichopungua miezi sita.

    (e) Akishindwa kutoa taarifa zinazohitajika TFF kwa kipindi cha siku 30 atafungiwa kwa kipindi kisichozidi miezi sita.

    (f) Akitoa taarifa ya uongo kiasi cha kupotosha maamuzi ya TFF atafungiwa kwa kipindi kisichopungua miezi kumi na miwili.

    (g) Akitoa matamshi au ishara za matusi dhidi ya mashabiki, akitoa matamshi, ishara za matusi yenye nia ya kumdhalilisha kiongozi mbele ya jamii awe wa TFF, KILABU au TAIFA atatozwa faini ya Sh. Milioni moja (1,000,000/=) na/au kufungiwa kwa kipindi kisichopungua miezi sita (6).

    (h) Kiongozi au Kilabu itawajibika kufuata na kutii maamuzi au maagizo ya TFF. Atakayeshindwa kutii maamuzi au maagizo hayo atafungiwa kwa kipindi kisichopungua miezi sita (6) na au kutozwa faini ya Sh. Milioni moja (1,000,000/=) au vyote kwa pamoja. Kama Kilabu itashindwa kutekeleza itaondolewa kwenye mashindano na kushushwa Daraja.

    (i) Ni marufuku kwa kiongozi wa Kilabu kushutumu au kutoa matamshi yenye lengo la kumkashifu au kumdhalilisha kiongozi wa TFF/Chama cha Mpira cha ngazi husika kwenye vyombo vya habari.

    (j) Hairuhusiwi kwa kiongozi au Kilabu kutoa matamshi au kuzungumzia jambo lolote linalohusu TFF kwenye vyombo vya habari bila ya kuwasiliana.

    (k) Kiongozi atakayekwenda kinyume na Kanuni ya 29 (i na j) atakabiliwa na adhabu zilizoainishwa kwenye Kanuni ya 29 (h) ya Kanuni hii.

    (l) Kiongozi akibainika kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mchezo kwa kujisingizia cheo kisicho kuwa chake atatozwa faini ya shilingi 200,000/= na /au kufungiwa kwa kipindi kisichopungua miezi 6.

    (m) Pamoja na adhabu zilizoanishwa kwenye Kanuni hii TFF inaweza kutoa adhabu nyingine kwa kuongeza au kupunguza ikiona kuna ulazima.

    (n) Uongozi ukibainika kugushi sahihi ya mchezaji au kufanya tendo lolote kwa lengo la kukamilisha zoezi la usajili kwa udanganyifu, Katibu Mkuu. Atafungiwa kwa kipindi kisichopungua miaka mitano na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake

    (o) Kiongozi atakayebainika kusababisha timu kutofika uwanjani na kukosa mchezo, baada ya kuhudhuria kikao cha maandalizi, atatozwa faini ya shilingi 1,000,000/= na kufungiwa kwa kipindi kisichopungua miezi kumi na mbili (12).

    KANUNI YA 30
    VIWANGO NA UTARATIBU WA ADHABU KWA WACHEZAJI

    (1) Kilabu chochote kinaweza kutoa adhabu yoyote inayostahili dhidi ya mchezaji wake yeyote.

    (2) Adhabu zote zitakazotolewa na vilabu ni lazima zithibitishwe na TFF kabla adhabu hiyo haijaanza kutekelezwa.

    (3) Kilabu hakitakuwa na mamlaka ya kumfungia mchezaji kwa kipindi kinachozidi msimu wa ligi husika au kwa mchezaji mwenye mkataba, zaidi ya kipindi cha mkataba wake na klabu.

    (4) Kilabu hakitakuwa na mamlaka ya kumfungia mchezaji yoyote nje ya nchi.

    (5) TFF, pamoja na kuthibitisha adhabu yoyote iliyotolewa na klabu, kufuta, kupunguza au kuongeza adhabu hiyo ikiwa ni pamoja na kumfungia mchezaji huyo nje ya Nchi.

    (6) Kabla Kilabu chochote hakijatoa adhabu yoyote ni lazima mchezaji anayehusika apewe nafasi ya kujitetea.

    (7) Kilabu chochote kitakachotoa adhabu kwa mchezaji wake na kutuma taarifa hiyo TFF ili adhabu hiyo ithibitishwe, kitalazimika kutuma TFF vielelezo vyote vinavyohusika ikiwa ni pamoja na Muhtasari wa Kikao kilichotoa adhabu hiyo.

    (8) Endapo mchezaji yeyote anaamini ameonewa kutokana na adhabu aliyopewa na kilabu chake na ikathibitishwa na TFF, anarushusiwa kukata rufani, kupinga adhabu hiyo, kwa TFF.

    KANUNI YA 31
    ADHABU KWA KLABU

    (1) Kilabu kina wajibu na jukumu la kuhakikisha kuwa wachezaji, viongozi, wanachama na wapenzi wake wanajiheshimu na hawajihusishi na vitendo vyovyote vya utovu wa nidhamu kama vile matusi, vitisho, vurugu, vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina na vitendo vyovyote vingine visivyokuwa vya kimichezo kwenye viwanja vya michezo. Kilabu ambacho washabiki wake watafanya vitendo hivyo kitatozwa faini ya TShs 300,000/=. Mshabiki atakayekamatwa akifanya vitendo hivyo atachukuliwa hatua za kisheria na atakayepatikana na hatia atafungiwa kuingia uwanjani kwa kipindi kisichopungua miezi 3 na kisichozidi miezi 12.

    (2) Kilabu kitapoteza mchezo ambao utavunjika kutokana na vurugu za washabiki wake.

    (3) Kilabu pia zitawajibika kulipa gharama za matibabu na kulipa gharama za mali zilizoharibika kwa waathirika wa vurugu za washabiki wake zitakazofanyika kabla, wakati au baada ya mchezo.

    (4) Kilabu zinatakiwa zihakikishe viongozi wa kilabu husika waliosimamishwa na TFF kwa sababu moja au nyingine kujishughulisha na uongozi wa klabu wanatii adhabu zao. TFF itachukua hatua itakayoona inafaa ikiwemo kuisimamisha klabu kushiriki katika ligi iwapo klabu hiyo itaruhusu viongozi wake waliosimamishwa kujishughulisha na masuala ya uongozi ndani ya kipindi cha adhabu.

    (5) Kilabu kitakashindwa kuleta timu uwanjani baada ya kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mchezo itatozwa faini ya shilingi milioni tano (5,000,000/=) na, kiongozi aliyeshiriki kutoleta timu uwanjani atafungiwa kwa kipindi kisichopungua miezi kumi na mbili (12), kutojishirikisha na masuala yote ya mpira wa miguu na atatozwa faini ya shilingi milioni moja (1,000,000/=).

    SURA YA KUMI
    HADHI USAJILI NA UHAMISHO WA WACHEZAJI

    KANUNI YA 32
    KIPINDI CHA USAJILI
    (1) Usajili wa wachezaji ni suala la kiufundi kama ilivyo kanuni ya 8 (3). Mwalimu Mkuu wa timu atawajibika kutambua wachezaji wanaotakiwa kusajiliwa. Katibu Mkuu atafanya masuala ya utawala, atakamilisha zoezi la usajili wa wachezaji na kuwasilisha mikataba na fomu ya majina TFF kwa wakati.

    (2) Kutangaza wachezaji wanaoachwa, uhamisho na usajili wa wachezaji utafanywa na waalimu wa vilabu katika kipindi kitakachotangazwa na TFF.

    (3) Kutakuwa na vipindi vingine viwili vya usajili, kipindi cha kwanza kitakuwa baada ya kumalizika Ligi na kipindi cha pili kitakuwa katikati ya msimu wa Ligi Kuu ya 2008/9. Tarehe za usajili wa vipindi vyote viwili zitatangazwa na TFF. (kanuni Na 37 )

    KANUNI YA 33
    HADHI YA WACHEZAJI

    WACHEZAJI WA RIDHAA NA WA
    KULIPWA

    (1) Wachezaji wanaoshiriki katika Soka Rasmi ni wa Ridhaa au wa kulipwa.

    (2) Mchezaji wa Kulipwa ni mchezaji mwenye mkataba wa maandishi na Klabu na analipwa zaidi ya gharama halisi anazoingia kutokana na shughuli zake za soka. Wachezaji wengine wote wanahesabiwa kuwa ni wa Ridhaa.

    KANUNI YA 34
    KUPATA UPYA HADHI YA RIDHAA

    1 Mchezaji aliyesajiliwa kama Mchezaji wa Kulipwa hawezi kusajiliwa tena kama wa Ridhaa mpaka zipite angalau siku 30 baada ya mechi ya mwisho aliyoecheza kama wa kulipwa.

    2. Hakuna fidia inayolipwa kwa kupata upya hadhi ya Ridhaa. Iwapo mchezaji anasajiliwa upya kama wa kulipwa katika kipindi cha miezi 30 ya kurudishiwa hadhi ya Ridhaa, Klabu yake mpya italipa Fidia ya Mafunzo kwa mujibu wa Ibara ya 20 ya kanuni ya FIFA.

    KANUNI YA 35
    KUACHA SHUGHULI

    1. Wachezaji wa Kulipwa wanaomaliza muda wao wa mkataba na wachezaji wa Ridhaa wanaomaliza muda wao, watabaki kuwa wamesajiliwa katika Chama cha Mpira cha Nchi ambacho Klabu yao waliochezea mwisho kwa kipindi cha miezi 30.

    2. Kipindi hiki kinaanza siku ambayo mchezaji atachezea Klabu mara ya mwisho katika mechi Rasmi.

    KANUNI YA 36
    USAJILI

    1. Mchezaji lazima asajiliwe na Chama cha Soka ili kuchezea klabu kama mchezaji wa Kulipwa au wa Ridhaa kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya 2 ya kanuni za FIFA. Ni wale wachezaji waliosajiliwa tu ndio wanaostahili kushiriki katika Soka rasmi. Kwa kujisajili, ina maana mchezaji anakubali kufuata Sheria na Kanuni za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA). Mashirikisho na Vyama vya Soka.

    2. Mchezaji anaweza kusajiliwa na kilabu moja tu kwa wakati huo.

    3. Wachezaji wanaweza kusajiliwa katika kilabu hadi tatu kwa kipindi cha tarehe 01 Julai hadi 30 Juni cha mwaka unaofuata. Katika kipindi hicho, mchezaji anastahili kuchezea Mechi Rasmi katika kilabu mbili tu.


    KANUNI YA 37
    VIPINDI VYA USAJILI

    1. Wachezaji wanaweza kusajili tu kati moja ya vipindi viwili vya Usajili vya mwaka vilivyopangwa na Chama cha Soka kinachohusika. Jambo la pekee katika Sheria hii, mchezaji wa kulipwa ambaye Mkataba wake umekwisha kabla ya Kipindi cha Usajili anaweza kusajiliwa nje ya Kipindi cha Usajili. Vyama vya Soka vinaruhusiwa kusajili wachezaji hao wa kulipwa alimradi tu uzingativu unaotolewa kwa kuaminika kimichezo kwa mashindano yanayohusika. Iwapo kuna sababu za msingi za kuvunjika kwa mkataba, FIFA inaweza kuchukua hatua za muda ili kuepuka ukiukaji na kwa mujibu wa Ibara ya 22 ya kanuni za FIFA.

    2. Kipindi cha kwanza cha Usajili kitaanza baada ya kukamilika kwa msimu na kwa kawaida hukamilika kabla Msimu Mpya haujaanza. Kipindi hiki hakizidi majuma kumi na mawili. Kipindi cha Pili cha Usajili kwa kawaida kitatokea katikati ya Msimu na hakitazidi majuma manne. Vipindi Viwili vya Usajili kwa Msimu vitaarifiwa FIFA angalau miezi 12 kabla ya kuanza kutumika. FIFA itaamua tarehe kwa Chama chochote cha Soka kitakachoshindwa kuwasilisha kwa wakati.

    3. Wachezaji watasajiliwa tu itokeapo hali ya upekee kama ilivyotabiriwa na Ibara ya 6, aya ya 1. Iwapo maombi ya Kilabu yatawasilishwa kwa wakati kwa Chama kinachohusika wakati wa Kipindi cha Usajili.

    4. Masharti yanayohusu Vipindi vya Usajili hayatumiki kwa mashindano ambayo Wachezaji wa Ridhaa tu wanashiriki. Kwa mashindano ya aina hiyo, Chama kinachohusika kitabainisha vipindi ambapo wachezaji watasajiliwa, alimradi uzingativu utawekwa kwa kuaminika kwa mashindano yanayohusika.

    KANUNI YA 38
    PASI YA WACHEZAJI

    Chama kinachosajili kinawajibika kukipa Kilabu alikosajiliwa mchezaji pasi ya mchezaji yenye taarifa zinazohusika za mchezaji. Pasi ya Mchezaji itaonyesha kilabu alikosajiliwa tangu simu wake wa miezi 12 ya kwanza. Iwapo mwisho wa miezi 12 inaishia kati ya Misimu, mchezaji ataoroedheshwa katika pasi ya mchezaji kwa klabu aliyokuwa amesajiliwa katika Msimu uliofuata kumalizika kwa miezi yake 12.
    KANUNI YA 39
    MAOMBI YA USAJILI

    Maombi ya Usajili wa Mchezaji wa Kulipwa lazima yawasilishwe pamoja na nakala ya mkataba wa mchezaji. Ni ridhaa ya chombo cha uamuzi kinachohusika kuzingatia marekebisho au nyongeza yoyote ya mikataba ambayo hayakuwasilishwa ipasavyo kwa chombo hicho.

    KANUNI YA 40
    HATI YA UHAMISHO YA KIMATAIFA

    1. Wachezaji waliosajiliwa katika Chama kimoja cha Soka wanaweza kusajiliwa tu na Chama kipya mara chama hicho kipya kitakapopokea Hati ya Uhamisho ya Kimataifa (ambayo humu itajulikana kuwa: ITC) kutoka Chama cha Soka cha zamani. ITC itatolewa bure na bila ya masharti yoyote au ukomo wa muda. Masharti yoyote yatakayokwenda kinyume na hayo ni batili. Chama cha Soka kitakachotoa ITC kitapeleka nakala FIFA. Utaratibu wa kiutawala wa kutoa ITC umo katika Kiambatanisho cha 3 cha Kanuni hizi.

    2. ITC haihitajiki kwa mchezaji mwenye umri wa chini ya miaka 12

    KANUNI YA 41
    KUAZIMWA KWA MKOPO WACHEZAJI WA KULIPWA

    1. Mchezaji wa kulipwa anaweza kuazimwa kwa mkopo kwa kilabu nyingine kwa msingi wa makubaliano ya maandishi kati yake na klabu zinazohusika. Uazimwaji huo kwa mkopo utafuata sheria zilezile zinazotumika katika uhamisho wa wachezaji, yakiwemo masharti ya fidia ya mafunzo na utaratibu wa mshikamano.

    2 Kufuatana na Ibara ya 5, aya ya 3, ya kanuni za FIFA kipindi cha chini cha kuazima kwa mkopo mchezaji kitakuwa muda kati ya Vipindi Viwili vya Usajili.

    3. Kilabu itakayompokea mchezaji kwa msingi wa kuazimwa kwa mkopo haina haki ya kumhamishia katika klabu nyingine bila ya idhini ya maandishi ya kilabu iliyomwachia mchezaji kwa mkopo na ya mchezaji anayehusika.

    KANUNI YA 42
    WACHEZAJI WASIOSAJILIWA

    Iwapo mchezaji asiyesajiliwa na Chama cha Soka anacheza mechi rasmi yoyote ya Kilabu, mchezaji huyo atahesabiwa kucheza kinyume cha sheria. Bila ya kuathiri hatua yoyote inayotakiwa kurekebisha athari inayosabishwa na kucheza huko, vikwazo vinaweza kuwekwa kwa mchezaji na/au kilabu. Haki ya kuweka vikwazo hivyo kimsingi iko mikononi mwa Chama cha Soka husika au mtayarishaji wa Mashindano yanayohusika.

    KANUNI YA 43
    MASHARTI MAALUMU YANAYOHUSU MIKATABA KATI YA
    WACHEZAJI WA KULIPWA NA KILABU

    1. Iwapo wakala anahusika katika mapatano ya mkataba, naye atatajwa katika Mkataba.

    2. Muda wa chini wa Mkataba utakuwa kuanzia tarehe ya kuanza kutumika hadi mwisho wa msimu, wakati ambapo muda wa juu wa Mkataba utakuwa miaka mitano. Mikataba ya muda mwingine wowote itakubaliwa tu kama inalingana na Sheria za nchini. Wachezaji chini ya umri wa miaka 18 haruhusiwi kuingia mkataba wa mchezaji wa kulipwa kwa kipindi kinachozidi miaka mitatu. Sharti lolote linalotaja kipindi kirefu zaidi halitatambuliwa.

    3. Kilabu inayotarajia kuingia mkataba na mchezaji wa kulipwa haina budi kuiarifu klabu yake ya sasa kwa maandishi kabla ya kufanya makubaliano na mchezaji huyo wa kulipwa. Mchezaji wa kulipwa atakuwa huru tu kuingia mkataba na klabu nyingine iwapo mkataba wake na Kilabu yake ya sasa umekwisha au utakwisha baada ya miezi sita. Uvunjaji wowote wa sharti hili utastahili vikwazo vinavyofaa.

    4. Uhalali wa Mkataba hautahesabiwa mpaka kuwe na matokeo mazuri ya upimaji afya na/au kutolewa kwa kibali cha kufanya kazi.

    8. Iwapo Mchezaji wa Kulipwa ataingia katika mkataba zaidi ya mmoja unaohusu kipindi kimoja masharti yaliyowekwa katika Sura ya IV ya kanuni za FIFA yatatumika.

    KANUNI YA 44
    USAJILI NA UHAMISHO WA WACHEZAJI

    1. Fomu mama ya usajili wa wachezaji itatolewa na TFF katika kipindi kitakachotangazwa.

    2. Kutakuwa na Kitabu (Pasi) cha usajili wa mchezaji chenye nembo ya TFF na namba maalum kitakachotolewa na TFF, ambacho kitatumika kwa minajili ya kumhamisha mchezaji (kanuni 38)

    3. Kila mchezaji atakuwa na kitambulisho atakachoonyesha wakati wa mchezo.

    4. Mchezaji ana uhuru wa kujisajili na Kilabu kingine katika msimu mmoja iwapo kutakuwa na maelewano kati ya klabu chake na kile kinachotaka kumsajili.

    5. Kilabu kinawajibika kuingia mkataba na mchezaji wa kuichezea lakini mkataba huo ni lazima uthibitishwe na TFF. Ada ya kuthibitisha mkataba ni Sh. 10,000/=. (kanuni Na 43 (2)

    6. Mchezaji ambaye ameingia mkataba wa zaidi ya msimu mmoja hatoruhusiwa kujisajili na klabu kingine kabla ya klabu yake mpya kuafikiana na klabu yake ya zamani. (kanuni Na 43 (3).

    7. Mchezaji anawajibika kusaini Mkataba na Kilabu ili aweze kuidhinishwa na TFF kuchezea kilabu yake. Jina lake litaorodheshwa kwenye Fomu ya Majina (Fomu Mama).

    KANUNI YA 45
    UTHIBITISHO WA USAJILI

    Mchezaji yeyote hataruhusiwa kuchezea kilabu chochote katika michezo ya Ligi hadi usajili wake umethibitishwa na TFF. TFF itatoa siku 14 kuwasilisha malalamiko au pingamizi kimaandishi juu ya usajili tangu kutangazwa majina ya wachezaji wanaombwa kusajiliwa na klabu husika, baada ya hapo uthibitisho utakaotolewa na TFF ndiyo utakuwa wa mwisho. TFF haitapokea rufaa yeyote inayohusu usajili kwa mchezaji ambaye hakuwekewa pingamizi mwanzoni isipokuwa iwapo klabu imefanya udanganyifu wa jina la mchezaji.

    KANUNI YA 46
    MAJINA YA WACHEZAJI

    Mchezaji atalazimika kujaza majina yake kamili matatu katika kitabu cha usajili.


    KANUNI YA 47
    IDADI YA WACHEZAJI

    Kila Kilabu kitaruhusiwa kusajili wachezaji wasiozidi thelathini (30) na wasiopungua kumi na wanane (18).

    KANUNI YA 48
    KILABU / WACHEZAJI WANAOSITISHA AU KUMALIZA MIKATABA

    Kila Kilabu kitalazimika kuwasilisha TFF kwa maandishi, majina ya wachezaji watakaositisha mikataba yao/kuwa huru katika usajili wa msimu wa Ligi/dirisha dogo unaofuata katika muda wa Uhamisho utakaotangazwa na TFF na kitalazimika kumpa taarifa ya maandishi mchezaji/wachezaji husika.

    KANUNI YA 49
    WACHEZAJI WALIOPANDISHWA

    1. Kila Kilabu kitaruhusiwa kusajili wachezaji wa timu yake ya pili (B) ambao walithibitishwa na TFF katika msimu uliopita.

    2. Mchezaji yeyote wa timu ya pili ambaye hakusajiliwa na kuthibitishwa na TFF katika msimu uliopita hataruhusiwa kusajiliwa katika timu ya kwanza (A) kama mchezaji aliyepandishwa au huru.

    3. kilabu kitaruhusiwa kupandisha wachezaji wake chipukizi ambao hawajawahi kucheza Ligi yoyote waliotimiza sharti la kanuni ya 49 (1), ili kuziba mapengo wakati Ligi inaendelea. Kilabu kitafanya hivyo endapo hakijatimiza wachezaji 30 au kwa kuzingatia Kanuni Na 56 (1).

    KANUNI YA 50
    WACHEZAJI HURU

    1. Mchezaji yeyote ambaye hakusajiliwa na klabu yoyote ya Daraja lolote katika msimu uliopita atakua huru, hahitaji uhamisho bali atalipiwa ada ya usajili TFF.

    2. Mchezaji yeyote ambaye kilabu yake imesitisha mkataba wake/au mkataba wake umemalizika, atakua mchezaji huru na hivyo hatalipiwa ada ya uhamisho isipokuwa ada ya usajili TFF.

    3. Mchezaji aliyerudi nyumbani baada ya kumaliza mkataba wake nje hatokuwa huru, hadi atakapokamilisha taratibu za uhamisho wa Kimataifa.

    KANUNI YA 51
    WACHEZAJI WA KUHAMISHWA.

    Mchezaji yoyote ambae hajamaliza Mkataba au Mkataba wake haujasitishwa na Kilabu yake, atakapojisajili na Kilabu kingine ni lazima ahamishwe kuanzia ngazi ya Kilabu, Wilaya, Mkoa na TFF.

    KANUNI YA 52
    WACHEZAJI KUTOKA NJE YA NCHI

    Kilabu kinaruhusiwa kusajili wachezaji wa ngazi ya kimataifa (wachezaji wa timu za taifa/Ligi Kuu) kutoka nje ya nchi wasiozidi kumi. Kilabu hicho kinaruhusiwa kuchezesha wachezaji sita (6) wa kigeni katika mchezo mmoja. Wachezaji hao ni lazima wakamilishe taratibu za uhamisho wa kimataifa.

    KANUNI YA 53
    NGAZI ZA UTHIBITISHO WA USAJILI

    TFF itathibitisha usajili wa wchezaji wote wa kilabu za ligi kuu.

    KANUNI YA 54
    KUTENGUA UTHIBITISHO WA USAJILI

    Uthibitisho wa usajili wa wachezaji wa klabu za ligi kuu unaweza kutenguliwa na Kamati ya Utendaji ya TFF endapo itathibitika kuwa usajili huo umekiuka masharti ya Kanuni hizi.

    KANUNI YA 55
    KATAZO

    Haitaruhusiwa kwa mchezaji yeyote kutia saini mikataba ya vilabu zaidi ya kimoja kwa wakati mmoja. Mchezaji atakayesaini mikataba ya timu mbili tofauti kwa wakati mmoja, ataadhibiwa kwa mujibu wa kanuni ya 43 (5).

    KANUNI YA 56
    UHAMISHO WA MCHEZAJI

    Bila ya kuathiri kanuni za uhamisho na usajili wa wachezaji:-
    1. Kilabu kinaweza kumhamisha mchezaji kutoka kilabu kimoja hadi kingine, kwa madhumuni ya kumsajili, baada ya ligi kumalizika na/au katika kipindi cha usajili wa katikati ya msimu. Kilabu kinachotaka kumsajili mchezaji aliyesajiliwa na kilabu kingine au mwenye mkataba na kilabu kingine, kitalazimika kuafikiana na kilabu chake kabla ya kumsajili mchezaji huyo. Hata hivyo kilabu ambacho kitaruhusiwa kusajili mchezaji katikati ya msimu ni kile tu ambacho hakijatimiza wachezaji 30 au kile ambacho kimempa mchezaji wake ITC ya kwenda kucheza soka nje ya nchi, au kile ambacho mchezaji wake amehamia kilabu kingine cha ndani kwa mujibu wa Kanuni hii.

    2. Endapo kiongozi wa Kilabu anachohama mchezaji amekataa au amekwepa kuidhinisha uhamisho wa mchezaji asiye na mkataba na kilabu hicho na ambaye anayetaka kukihama kilabu chake baada ya msimu wa Ligi kwisha; Katibu wa Chama cha Mpira ngazi ya Wilaya husika ataidhinisha uhamisho huo baada ya mchezaji aliyeomba kuhama kumthibitishia kwa maandishi kuwa amehamia Kilabu hicho kipya lakini Katibu wa Kilabu chake cha zamani hataki au anakwepa kuidhinisha uhamisho wake.

    3. Nakala za barua ya uthibitisho wa mchezaji kwa Katibu wa Chama cha mpira ngazi ya Wilaya husika ni lazima zitumwe pia kwa Katibu wa Chama cha mpira cha Mkoa husika na kwa Katibu Mkuu wa TFF.

    4. Pamoja na kupokea nakala ya barua ya uthibitisho kwa mujibu wa Aya ya (3) ya Kanuni hii, TFF inaweza kumwita mchezaji huyo na kumhoji kuhusiana na uthibitisho alioutoa kwa Vyama vya mpira vya wilaya na mkoa na uamuzi wa TFF utakuwa wa mwisho.

    5. Ada za uhamisho wa mchezaji mmoja kutoka Kilabu kimoja hadi kingine kwa madaraja mbalimbali na mgawanyo wake kwa mamlaka zinazohusika zitakuwa kama inavyoonekana kwenye jedwali la kwanza lililopo kwenye nyongeza ya Kanuni hizi. Ada hizi ni kima cha chini cha ada za uhamisho wa wachezaji kutoka klabu moja kwenda nyingine lakini klabu yenye mkataba na mchezaji ina haki ya kudai malipo zaidi kwa ajili ya uhamisho toka kwa klabu kinachomtaka mchezaji wake. Ada za uhamisho kwa mamlaka zingine hata kwa wachezaji wenye mikataba zitabaki kama zilivyo.

    KANUNI YA 57
    UHAMISHO KWENDA TANZANIA ZANZIBAR

    Pamoja na kufuata utaratibu mzima wa uhamisho wa mchezaji kama ulivyoainishwa katika Kanuni ya 56, ada za uhamisho wa wachezaji wa Tanzania Bara kwenda Tanzania Visiwani itakuwa ni itakuwa ni kwa mujibu wa makubaliano baina ya timu zinazohusika kulingana na masharti yaliyomo ndani ya mkataba wa mchezaji husika na kilabu chake.

    SURA YA 11
    ADHABU ZIHUSUZO USAJILI NA UHAMISHO

    KANUNI YA 58
    ADHABU ZIHUSUZO USAJILI NA UHAMISHO

    1. Mchezaji yeyote atakayebadili jina lake halisi kwa madhumuni ya kudanganya ili asajiliwe kinyume cha masharti ya Kanuni hizi atafungiwa kucheza mpira ndani na nje ya nchi kwa kipindi kisichopungua miezi kumi na miwili kuanzia tarehe ya kubainika.

    2. Kilabu iliyomchezesha mchezaji aliyebadili jina kwa nia ya kudanganya kitalipa faini ya TShs 100,000/= kwa kila mchezo ambao mchezaji huyo alicheza lakini matokeo ya uwanjani hayatobadilika.

    3. Kilabu kitakachothibitika kumchezesha mchezaji ambaye hajasajiliwa na klabu hiyo kitapoteza michezo yote ambayo mchezaji huyo alicheza bila ya kujali kukatwa au kutokatwa rufaa.

    4. Kitabu cha usajili cha mchezaji kilichochafuka, kufutwafutwa au kunyofolewa kiasi cha kuleta mashaka hakitakubaliwa.

    5. Kilabu chochote kitakachowasilisha Usajili wake baada ya tarehe itakayotangazwa na TFF kitakabiliwa na faini ya TShs 500,000/=.

    6. Endapo TFF itatoa muda wa nyongeza wa kurejesha Mikataba ya wachezaji na bado kilabu kikashindwa kuwasilisha mikataba kwa muda huo; kilabu hicho kitahesabika kuwa kimejiondoa chenyewe kwenye Ligi na kitashuka daraja.

    7. Kiongozi yeyote wa TFF atakayeweka saini inayotofautiana na saini yake halisi kwenye kitabu cha usajili kwa madhumuni yoyote yale, atafungiwa kuongoza mchezo wa mpira kwa kipindi cha miaka mitano.

    8. Kiongozi yeyote wa FA au Kilabu atakayetoa taarifa za uongo na kupotosha Kamati ya Utendaji ya FA ngazi husika katika maamuzi yake, kuhusiana na usajili, atakabiliwa na adhabu ya kufungiwa kwa kipindi kisichopungua miezi sita.

    9. Kiongozi yeyote wa TFF au Kilabu atakayekataa au atakayekwepa bila sababu ya msingi, kusaini kitabu cha Usajili kwa madhumuni ya uhamisho atakabiliwa na adhabu ya kufungiwa kwa kipindi kisichopungua miezi sita.


    KANUNI YA 59
    UHAMISHO NJE YA NCHI

    1. Mchezaji yeyote anaruhusiwa kuhamia Kilabu kingine nje ya Nchi baada ya kupata kibali cha Kimataifa (ITC).

    2. Kabla TFF haijatoa kibali, mchezaji analazimika kupata idhini ya Kilabu chake cha hapa Nchini.

    3. Maombi ya kibali cha TFF na idhini yeyote itakayotolewa na Kilabu ni lazima vifanywe kwa maandishi.

    4. Kilabu kinachotaka kumhamisha mchezaji na kilabu kinachohusika na mchezaji huyo vitakubaliana kuhusu gharama za uhamisho.

    5. Endapo itatokea kutokubaliana kati ya pande hizo mbili kutokana na sababu yoyote ile TFF itaingilia kati na kutoa uamuzi kwa kuzingatia sheria na kanuni za TFF, CAF na FIFA.

    6. TFF itatambua kumalizika au kuvunjika kwa mkataba wa mchezaji na klabu yake ya nje baada ya kupata ITC kutoka kwa Chama cha Soka cha Nchi alipokuwa akicheza.

    7. Barua ya uthibitisho kutoka kwa Chama cha Soka cha nje ni lazima iwe na Nembo ya Chama husika, jina kamili, cheo na saini ya afisa mhusika katika Chama hicho.

    9. Uhamisho wa kimataifa unaombwa na kutolewa kwa chama cha cha mpira cha kitaifa pekee kwa niaba ya kilabu, na si kwa mchezaji au kiongozi wa kilabu.


    SURA YA 12
    MENGINEYO
    KANUNI YA 60
    MWALIMU WA TIMU

    1. Kila Kilabu kinapaswa kuajiri mwalimu wa timu mwenye ujuzi wa kutosha na anayetambuliwa na TAFCA, na mkataba wake kusajiliwa TFF.

    2. Mwalimu wa klabu ya Ligi kuu anatakiwa awe na Stashahada au cheti cha ngazi pevu ya ufundishaji.

    3. Mwalimu toka nje atathibitishwa kwanza na TFF kabla ya kuingia mkataba na kilabu na kupewa kibali cha kuishi na kufanya kazi nchini.

    4. Mwalimu atatakiwa kuwa na Leseni ya Daraja la A toka TFF kuweza kufundisha kilabu cha ligi kuu.

    5. Mwalimu wa timu ndiye mkuu wa shughuli zote za timu kuanzia usajili wa wachezaji, uandaaji wa timu, usimamiaji katika mashindano na kadhalika.

    KANUNI YA 61
    DAKTARI WA TIMU

    Kila Kilabu kinapaswa kuajiri Daktari wa timu mwenye ujuzi wa kutosha na anayetambuliwa na TASMA na kuthibitishwa na TFF.

    KANUNI YA 62
    TIMU ZA PILI NA WATOTO

    1. Kila Kilabu kinatakiwa kuunda na kudumisha timu za pili au za watoto ikiwa ni Sharti la kushiriki Ligi na kwa manufaa ya Kilabu na kwa maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu kwa ujumla. Endapo Kilabu itashindwa kutimiza sharti hili itaondolewa katika Ligi na kushushwa daraja.

    2. Kila Kilabu kitaruhusiwa kusajili wachezaji wa timu za watoto wasiyopungua 18 na wasiyozidi 25 wenye umri usiyozidi miaka 20.

    3. Kilabu zinatakiwa ziwe zimekamilisha usajili wa timu za watoto ifikapo tarehe 15/8/2008.

    4. Wachezaji wa timu za watoto wanaweza kutumika katika mashindano ya Ligi Kuu.

    5. Usajili na uhamisho wa timu za watoto utazingatia kanuni za Ligi Kuu.

    6. Waraka maalumu utatolewa kuhusiana na usajili wa wachezaji wa timu za watoto ambao utasomeka pamoja na kanuni hizi.

    KANUNI YA 63
    UDHAMINI

    TFF itajitahidi kutafuta mdhamini/wadhamini wa Ligi Kuu, kila Kilabu kitalazimika kuheshimu na kuzingatia kikamilifu masharti yote yanayotakiwa kutekelezwa na Kilabu chenyewe, timu yake, wachezaji wake au Viongozi wake. yaliyomo ndani ya Mkataba /Mikataba hiyo kama itakavyoelezwa na TFF. Timu itakayoshindwa kutekeleza masharti haya kama itakavyoelezwa na TFF itatozwa faini isiyopungua Tshs. 1,500,000/= na pia inaweza kuchukuliwa hatua nyingine ikiwemo kuondolewa kwenye mashindano na /au kufungiwa.

    KANUNI YA 64
    UFAFANUZI

    Kwa minajili ya kufafanua Kanuni hizi TFF itakuwa inatoa WARAKA kila inapoonekana inafaaa kufanya hivyo kwa lengo la kuleta ufanisi katika utekelezaji wa Kanuni hizi.

    KANUNI YA 65
    TAFSIRI

    Kikao cha juu kuliko vyote kwa ajili ya tafsiri ya Kanuni hizi kitakuwa kamati ya utendaji ya TFF na uamuzi wake utakuwa wa mwisho.

    KANUNI YA 66
    MAREKEBISHO YA KANUNI

    Kamati ya utendaji ya TFF inaweza kurekebisha Kanuni hizi kila inapotokea haja na sababu za kufanya hivyo.

    KANUNI YA 67
    KUFUTA KANUNI

    Kanuni hizi zinaweza kufutwa na Kamati ya Utendaji ya TFF pekee.

    KANUNI YA 68
    MAMBO YASIYOMO KWENYE KANUNI HIZI

    Mambo yote yasiyokuwemo kwenye Kanuni hizi yataamuliwa na Kamati ya Utendaji ya TFF kwa kuzingatia Kanuni za FIFA na CAF.

    Kanuni hizi zimepitishwa kwa Azimio la Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana Dar es salaam tarehe 25 Julai, 2008.


    _________________ ______________________
    Frederick Mwakalebela TAREHE
    KATIBU MKUU


    NYONGEZA
    JEDWALI LA KWANZA
    (KANUNI YA 56 (5)
    FOMU YA MGAWANYO WA MAPATO
    KANUNI YA 18 (1), (2), (3), (4) NA (5)

    KIASI JINA SAHIHI
    Toa jichangie shs. 200/= kila tiketi
    (i) Kilabu ngeni shs. 70/= kila tiketi
    (ii) Klabu mwenyeji shs. 70/= kila tiketi
    (iii) FA (M) shs. 60/= kila tiketi
    Toa: Posho ya kujikimu, usafiri wa ndani kwa waamuzi na kamisaa
    Usafiri wa ndani kwa waamuzi wote shs. 10,000/= na kwa kamisaa shs. 10,000/=.
    Posho ya mwamuzi wa akiba shs. 30,000/=
    Gharama za tiketi
    Baki ya pato
    10% Gharama za mchezo: (Rejea fomu ya gharama za mchezo)
    (Isizidi 5,000,000/=)
    15% TFF (T)
    10% FDF
    10% Uwanja
    1% BMT
    4% FA (M)
    25 klabu ngeni
    25% Klabu mwenyeji
    JUMLA



    JEDWALI LA PILI
    (KANUNI YA 57 (B))

    FOMU YA MGAWANYO WA GHARAMA ZA MCHEZO LIGI KUU YA VODACOM 2008/9

    KANUNI YA 19 (1), (2) NA (3)

    KIASI JINA SAHIHI
    Gharama za msimamizi wa kituo
    (j) Msimamizi mkazi atalipwa posho 90,000/= na nauli ya
    ndani 10,000/=
    (ii) Msimamizi kutoka nje ya kituo atalipwa posho shs.
    90,000/=, nauli ya ndani 10,000/= gharama za kula na
    kulala shs. 30,000/= na nauli kutoka kituo chake na
    kurudi
    (iii) Malipo ya ulinzi, ball boys, huduma ya kwanza, vinywaji,
    wasimamizi, wauzaji na wachanaji tiketi, matangazo,
    stationery.
    (iv) Malipo ya TAFCA 10,000/=
    (v) Malipo ya FRAT 10,000/=
    (vi) Baki ya pato iwapo gharama za mchezo ni pungufu 10%
    Klabu ngeni 25%
    Klabu mwenyeji 25%
    TFF 50%
    JUMLA




    ADA ZA USAJILI NA UHAMISHO WA WACHEZAJI

    Ada Za Uhamisho Za Wachezaji Kutoka Daraja Lolote Kwenda Ligi Kuu Itakuwa Kama Ifuatavyo;



    KLABU TFF FA (M) FA (W) JUMLA
    55,000.00 25,000.00 20,000.00



    MGAWANYO WA ADA ZA USAJILI NA UHAMISHO WA WACHEZAJI KUTOKA TANZANIA BARA KWENDA VISIWANI.



    KLABU TFF FA (M) FA (W) JUMLA
    300,000.00 120,000.00 80,000.00
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KANUNI ZA LIGI KUU BARA HIZI HAPA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top