• HABARI MPYA

    Monday, January 26, 2009

    PHIRI AWALILIA HENRY JOSEPH, EMEH

    Patrick Phiri, kocha wa Simba

    KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Phiri, amekiri kuwa kuondoka kwa mshambuliaji wake wa kulipwa, Emeh Izechukwu na kiungo Henry Joseph, ni pengo katika kikosi cha timu hiyo.
    Wachezaji hao wanaondoka nchini huku Simba ikiwa inakabiliwa na kibarua kigumu cha kuwafukuza mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, walio kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo inayoendelea.
    Akizungumza kwa njia ya simu jana, Phiri ambaye ni raia wa Zambia, alisema hata hivyo kuwa wawili hao watakuwapo katika mechi ya Jumatano dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons, itakayopigwa katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
    Henry na Emeh wamepata nafasi ya kwenda kufanya majaribio ya soka la kulipwa katika klabu ya Ligi Daraja la Kwanza nchini Norway ya Molde FK.
    Wachezaji hao wamepata nafasi hiyo baada ya kufanyiwa mpango na wakala mmoja nchini ambaye anatambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), aliyewahi pia kuwatafutia nafasi kama hiyo wachezaji Uhuru Seleman anayeichezea Mtibwa Sugar kwa sasa na Seleiman Ndikumana wa Burundi.
    Akizungumzia maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi Kuu, Phiri alisema anaifanyia kazi safu ya ulinzi ya timu hiyo inayoonekana kuwa na udhaifu ili kuondoa dosari ambazo zimekuwa zikijitokeza katika mechi zilizopita.
    Alisema kwa sasa hana wasiwasi wowote na safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kutokana na uwezo wa kupachika mabao walioonyesha washambuliaji wake katika mechi zilizopita.
    Tangu Phiri ajiunge na Simba, tayari ameweza kuipatia ushindi katika mechi mbili mfululizo, ikiwa ni ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Villa Squad na Polisi Morogoro ambayo ilifungwa mabao 3-2.
    Keshokutwa Simba inakutana na Prisons, huku ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha bao 1-0 ilichokipata katika mchezo wa raundi ya kwanza ya ligi hiyo, uliofanyika katika Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya.
    Mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, Simba, ambayo ilikuwa ikinolewa na kocha kutoka Bulgaria, Krasmir Bezinski, ilishindwa kutamba katika baadhi ya mechi zake na kujikuta ikipoteza michezo mitano.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PHIRI AWALILIA HENRY JOSEPH, EMEH Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top