• HABARI MPYA

    Monday, August 03, 2015

    SHILOLE ANAPOSHINDANA NA SERIKALI INAKUWA KITU FLAN AMAZING

    Unapowauliza watu wengi wenye hekima zao pale wanapokuwa na kesi mahakamani, jibu la huwa ni moja tu: “Shauri hili lipo mahakamani, siwezi kulizungumzia kwa sasa.” …Na pale hukumu inapotolewa kinyume na matarajio yao, basi watakuambia “Tunaandaa utaratibu wa kukata rufaa”.
    Hivi ndivyo nilivyomtarajia msanii Shilole awe hivyo pale alipofungiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kosa la kucheza uchi, ikiwa ni mara yake ya pili kufanya hivyo.
    Kwangu mimi nilikuwa namuona Shilole kama msanii mpiganaji, aliyepambana kutoka chini hadi kuwa mmoja mastaa wanaozungumzika kwenye ‘game’ .
    Msanii aliyeweza kusaka upenyo wa fursa baada ya kuona nafasi ya kupasua kwenye filamu ni finyu, akapenya kwenye muziki, nyimbo zikasumbua kwenye media, show zikikamiminika, mialiko ya nje ya nchi ikabisha hodi kwa kasi.
    Lakini pamoja na upambanaji wake, usasa ulimsumbua Shilole, uvaaji uliokiuka maadili ya kitanzania ikawa ni sehemu ya taratibu zake za kazi, uchezaji uliojaa ukakasi nao pia ukawa ni moja ya ‘silaha’ zake kubwa kwenye kuboresha soko lake.
    BASATA ilishamwita Shilole na kumpa karipio kali, mwenye akaomba radhi kwa maandishi, pengine bila yeye kujua kuwa ile ni kadi yake ya njano, bibie huyo akaendelea na ‘swaga’ zake ya kuuanika mwili wake. 
    Shilole akawa na onyesho nchini Ubelgiji, akafanya yasiyostahili jukwaani, BASATA wakamwita tena na kwa mara nyingine akaomba radhi kwa njia ya maandishi, baada ya hapo hukumu ikafuata …Shilole akafungiwa kufanya maonyesho ya muziki kwa mwaka mmoja ndani na nje ya nchi.
    Na hapo ndipo nilipotegemea busara za Shilole, atambue kuwa Basata si taasisi ya mtu binafsi, BASATA ni chombo rasmi cha serikali, kinachofanya kazi kwa niaba ya serikali na hivyo tamko lolote la BASATA ni sawa na tamko la serikali.
    Wakati mashindano ya Miss Tanzania yakifungiwa na BASATA mwaka jana, Kamati ya Miss Tanzania ikawa mpole, wala haijapimana ubavu na BASATA na kuanza kusukumiana lawama kupitia vyombo vya habari.
    Kufungiwa kwa mashindano ya Miss Tanzania, kuliathiri vibarua vya zaidi ya watu 1000 ambao pengine kwa namna moja au nyingine, maisha yao na ya wanaowategemea yaliathirika kwa kiasi kikubwa.
    Shilole anapobishana na BASATA na kuwasuta kwenye mahojiano yake kupitia mitandao ya kijamii, anapaswa kwanza ajiulize yeye na mashindano ya Miss Tanzania nani mkubwa?
    Miss Tanzania ilikuwa na udhamini wa mamilioni kutoka kinywaji cha Redd’s kupitia Tanzania Breweries lakini BASATA haikujali hilo, sheria ikachukua mkondo wake …BASATA haikujali uhusiano wake mzuri na Tanzania Breweries ambayo inadhamini tuzo zake za Tanzania Music Awards kupitia Kilimanjaro Lager, ikatoa hukumu bila kupepesa macho.
    Shilole inabidi ajiulize yeye ni nani mpaka apimane ubavu na chombo cha serikali, anategemea adhabu yake itasitishwa kwa njia hiyo? Je yuko juu ya sheria kiasi kwamba hastahili kuguswa? Anadhani BASATA wanafanya kazi kwa mashinikizo ya mitandao ya kijamii?
    Nilipigwa na butwaa pale Shilole alipokuwa akiswashutumu BASATA kwa kusema:  “Mnataka nikaishi wapi? nina watoto wawili wanaosoma boarding, kila mwaka ninatakiwa nilipe milioni 5 kwa kila mmoja, nina watoto 3 yatima ninaowalea na kuwasomesha kupitia muziki huu huu ninaofanya ambao watu wengine, ninalipa kodi ya nyumba Milioni 7 kwa mwaka, mlitaka nikauze unga au niwe changudoa?”
    Kwa maneno hayo ni wazi kuwa Shilole anapimana ubavu na BASATA, mbaya zaidi kuna wakati alikwenda mbali zaidi kwa kusema “Tutachukua hatua kwa hatua” …Nimwambie tu Shilole kuwa unapokuwa mkosaji halafu ukataka kupimana ubavu na serikali ni kitu flan amazing, sio amazing ile ya kuvutia kama wanavyoitumia watoto wa mjini, hapana ni amazing ya kuharibu – Inashangaza, inastaajabisha, inaduwaza!
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SHILOLE ANAPOSHINDANA NA SERIKALI INAKUWA KITU FLAN AMAZING Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top