• HABARI MPYA

    Sunday, August 02, 2015

    CECAFA ACHENI KIBURI, YARUDISHENI MASHINDANO JANUARI, HAYANA FAIDA

    HATIMAYE bingwa mpya wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame anatarajiwa kupatikana jioni ya leo kwa mchezo wa fainali kati ya wenyeji Azam FC na Gor Gor Mahia ya Kenya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Mchezo huo utatanguliwa na mechi ya kusaka mshindi wa tatu kati ya KCCA ya Uganda na Khartoum N ya Sudan, itakayoanza Saa 8:00 mchana.
    Imeshuhudiwa katika michuano ya mwaka huu, mabingwa watetezi, El Merreikh ya Sudan wakishindwa kuja kwa sababu wapo katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Na hata washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Sudan, El Hilal nao hawakuja kwa sababu wapo kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika- badala yake ndio wamekuja washindi wa tatu na wa nne, Al Shandy na Khartoum.
    Hakuna ubishi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, klabu hizo mbili za Sudan zipo juu zaidi kisoka na hata kwa uwezo wa kujiendesha, tena kisasa kabisa.
    Kwa miaka ya karibuni imekuwa kawaida kwa timu stahiki kutojitokeza katika Kombe la Kagame kutokana na sababu za kawaida sana.
    Kwa mfano mwaka jana, Yanga SC walitakiwa kusafiri hadi Rwanda, lakini wakagoma kwa sababu ndiyo kwanza walikuwa wanaanza maandalizi ya msimu mpya.
    Miaka ya nyuma, mashindano haya wakati huo yakijulikana kama Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati tu hakuna timu iliyostahili ilikuwa inakosekana.
    Mashindano haya wakati huo yalikuwa yafanyika Januari ya kila mwaka na yalikuwa yanafana mno.
    Timu nyingi zilichangamkia fursa ya kushiriki michuano hiyo, kwa sababu baada ya hapo zilikuwa zinaingia moja kwa moja kwenye michuano mikubwa ya Afrika- Kombe la Washindi, Kombe la CAF na Klabu Bingwa Afrika.
    Kwa sasa Kombe la CAF limeunganishwa na Kombe la Washindi na kuwa Kombe la Shirikisho ndiyo hilo limefanya tuwakose El Hilal na Klabu Bingwa sasa imekuwa Ligi ya Mabingwa, ambayo nayo imefanya tuwakose Merreikh.
    Michuano hii ilianza taratibu kutoka katika muda wake mwafaka wa kufanyika, kutokana tu na sababu za ukosefu wa fedha za maandalizi.
    Ilisogezwa mbele kidogo kidogo hadi sasa kalenda yake imekuwa Julai na Agosti.
    Julai na Agosti ni kipindi ambacho michuano ya CAF inafikia kwenye hatua ya makundi- lakini kwa sababu Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limejikatia tamaa, halioni umuhimu tena wa michuano hiyo ya bara zima.
    Sasa ni dhahiri sisi wa CECAFA ndiyo tunashika mkia kisoka katika bara letu, hata nchi ndogo ndogo zilizokuwa duni kisoka miaka michache iliyopita kama Madagascar, Lesotho, Swaziland na Shelisheli za kusini (COSAFA) sasa zinatufundisha mengi. 
    Hii ni kwa sababu, pamoja na mapungufu yetu yote, lakini pia hatuna mipango.
    Mfano mdogo ni hii michuano ya Kagame, badala ya kuifanya Januari ili timu zetu zipate maandalizi ya kuingia kwenye michuano ya Afrika, tunaifanya Julai na Agosti.
    Kipindi hicho ni ambacho baadhi ya Ligi za ukanda wetu zinatoka kumalizika na ligi nyingine zinaelekea kuanza, unaweza kuona kabisa timu nyingi huingia katika mashindano haya zikiwa haziko tayari.
    Mashindano haya yakirudi kufanyika Januari, dhahiri yatarejesha msisimko wake na hakutakuwa na udhuru wa timu kutokuja kushiriki.
    Hata ile dhamira ya kualika timu kubwa za ukanda mwingine kuja kutongezea changamoto inaweza kufanikiwa kwa sababu hicho ni kipindi ambacho hakuna mashindano ya CAF.
    Lazima turejeshe enzi zile bingwa mtetezi anapokewa kwenye kituo cha mashindano akiwa na Kombe lake. Turejeshe enzi ambazo mashindano yanashirikisha mabingwa watupu wa ukanda wetu.
    Turejeshe thamani ya mashindano kwamba si ya kila timu kushiriki, yawe mashindano ya mabingwa wa ukanda wetu.
    Novemba na Desemba tunafanya Challenge (Kombe la Mataifa ya CECAFA), Januari mapema tu ndani ya wiki mbili za mwanzo tunakamilisha Kagame- baada ya hapo, klabu zetu ziende kwenye michuano ya Afrika zikiwa vizuri.
    Lakini ajabu CECAFA wameshindwa kuelewa dhana hii na wameendelea kulazimisha Kombe la Kagame lifanyike Julai na Agosti, ndiyo maana watu sasa wanayaita mashindano haya Bonanza tu, kwa sababu hawaoni umuhimu wake.
    Wakati umefika sasa viongozi wa CECAFA wakubali kushaurika na mashindano wayarudishe Januari. Tukutane Taifa. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CECAFA ACHENI KIBURI, YARUDISHENI MASHINDANO JANUARI, HAYANA FAIDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top