• HABARI MPYA

    Saturday, December 20, 2025

    MCHEZAJI WA ZAMANI WA SIMBA, MNENGE SULUJA AFARIKI DUNIA GEITA

    Mnenge Suluja wakati anacheza
    Toto Africans mwaka 1995
    WINGA machachari wa zamani wa Simba SC, Mnenge Suluja Junior (51) amefariki Dunia usiku wa jana mkoani Geita.
    Kwa mujibu wa mchezaji mwenzake wa zamani wa Simba SC, Athumani Chama marehemu alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya vidonda vya tumbo.
    Chama amesema umauti umemkuta nyumbani kwake, Geita siku nne baada ya kurejea kutoka Mwanza ambako alikuwa amelazwa kwa wiki moja kwa matibabu hospitali ya Bugando.
    Mwili wa marehemu utasafirishwa kesho mchana kwenda nyumbani kwao, Sengerema kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika Jumatatu mchana kijiji cha Nyantakubwa.
    Hadi umauti unamkuta, Suluja ambaye kisoka aliibukia Pamba ya Mwanza kabla ya kusajiliwa Simba SC mwaka 1997 — alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Wilaya ya Geita (GEDFA).
    Mbali na Pamba na Simba SC, Mnenge pia alichezea timu za Malindi ya Zanzibar, Kariakoo United ya Lindi na Pallson ya Arusha pamoja na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars akianzia timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Vijana Stars, sasa Ngorongoro Heroes.
    Mnenge pia amewahi kucheza soka ya kulipwa Falme za Kiarabu (UAE) pamoja na wachezaji wengine wa Tanzania akina Iddi Moshi, Athumani Chama, Mohamed Hussein 'Mmachinga' kwenye Kombe la Mafuta 'Adma Cup'. 
    Mnenge alizaliwa Septemba 10, mwaka 1974, Temeke, Dar es Salaam ambako baba yake alikuwa Mwandishi wa Habari za mahakamani wa magazeti mbalimbali.
    Mnenge alipata elimu yake ya Msingi katika shule ya Nyakato, kabla ya kujiunga na Sekondari ya Makoko Seminari ya Musoma mkoani Mara hadi Kidato cha Pili akahamia sekondari ya Buswelu iliyopo Ilemela, Mwanza ambako alimalizia Kidato cha Nne.
    Baada ya hapo akajikita kwenye soka akianzia OAU maarufu kama 'Watoto wa Mchopa', Toto Africans na Pamba zote za Mwanza, kabla ya kwenda Malindi SC ya Zanzibar, Falme za Kiarabu (UAE) kucheza Kombe la Mafuta, Simba, Kariakoo United na Pallson.
    Mnenge ambaye ameacha mke, Anastacia na watoto wawili wote wa kiume, Juma aliyezaliwa mwaka 1998 na Mnenge Suluja Junior aliyezaliwa mwaka 2007 - timu yake ya mwisho kuchezea ni Geita Gold ambayo aliichezea kuanzia katika Ligi ya Mkoa hadi kuipandisha Daraja la Kwanza, kabla ya kustaafu.
    Mungu ampumzishe kwa amani. Amin.
    Mnenge Suluja (kushoto) akiwa na Wyclif Ketto (katikati) Said Maulid 'SMG' (kulia) wakati wanacheza Simba SC mwaka 2000
    Mnenge Suluja wa pili kutoka kushoto walioketi katika kikosi cha Pamba SC mwaka 1997
    Mnenge Suluja wa tatu kutoka kushoto waliopiga magoti akiwa na kikosi cha OAU maarufu kama 'Watoto wa Mchopa' mwaka 1994
    Mnenge Suluja wa sita kutoka kulia waliosimama akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 mwaka 1999


    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MCHEZAJI WA ZAMANI WA SIMBA, MNENGE SULUJA AFARIKI DUNIA GEITA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top