FAINALI za Kombe la Mataifa ya Afrika(AFCON) zitakuwa zikifanyika kila baada ya miaka minne, huku Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likitambulisha michuano mipya, Ligi ya Mataifa ya Afrika.
Hayo yamesemwa na Rais wa CAF, Patrice Motsepe katika mkutano na Waandishi wa Habari leo ukumbi wa mikutano Uwanja wa Prince Moulay Abdellah Jijini Rabat nchini Morocco siku moja kabla ya kuanza kwa Fainali za 35 za AFCON kesho.
Hiyo italiweka Bara hilo sambamba na kalenda ya kimataifa, kwani CAF lilisema linafanya hatua hiyo kwa maslahi ya ustawi wa wachezaji na kwamba litahakikisha mapato zaidi kwa mchezo huo barani.
"Huu ni uamuzi bora kwa soka ya Afrika," alisema Dk. Motsepe raia wa Afrika Kusini.
AFCON ijayo itaendelea kama ilivyopangwa mwaka wa 2027, ambayo imepangwa kuandaliwa kwa pamoja na Kenya, Tanzania na Uganda, ikifuatiwa na mashindano mengine mwaka unaofuata, Motsepe alisema, akizialika nchi zinazotarajiwa kuwa wenyeji kutoa zabuni.
Baada ya Fainali za 2028, mashindano hayo ya timu 24 yatafanyika kila baada ya miaka minne, na kumalizia zaidi ya nusu karne ya mashindano ya kila baada ya miaka miwili.
Badala yake, Ligi ya Mataifa ya Afrika itaanzishwa kila mwaka kuanzia 2029, ambayo Dk. Motsepe alisema itachezwa katika madirisha ya Septemba, Oktoba na Novemba kwa mechi za timu za kitaifa.
Huku mashirikisho mengine barani Asia, Ulaya na Amerika Kusini yakiandaa ubingwa wao wa bara kila baada ya miaka minne, Afrika ilishikilia kuandaa ubingwa wake kila baada ya miaka miwili, ikisema kwamba mapato yanayotokana na mashindano hayo yalikuwa karibu 80% ya bajeti yake.
"Nilikuwa na tatizo hapo awali kuhusu kubadilisha Kombe la Mataifa kuwa kila baada ya miaka minne lakini mara tu nilipopitia takwimu niliona tutapata pesa zaidi [kwa kalenda mpya]," rais wa CAF alisema.
Rais wa FIFA Gianni Infantino hapo awali ameshinikiza uongozi wa CAF kubadilisha mzunguko wake, na muda wa AFCON umekuwa ukizua utata kwa muda mrefu kwa sababu kwa kawaida umekuwa ukiandaliwa katikati ya msimu wa Ulaya, na kulazimisha vilabu kuwaachilia wachezaji wao wa Kiafrika.
Mvutano huu wa uaminifu ulipaswa kutatuliwa kwa kuhamisha Kombe la Mataifa hadi katikati ya mwaka kuanzia 2019 lakini mashindano ya baadaye nchini Cameroon mwaka 2022 na Ivory Coast mwaka 2024 yaliandaliwa tena mwanzoni mwa mwaka.
"Ni kwa maslahi ya timu, vilabu na wachezaji," Dk. Motsepe aliongeza.
"Siwezi kuwa na wachezaji wanaoondoka katika klabu zao barani Ulaya katikati ya msimu. Ni makosa.
"Tuna wajibu kwa wachezaji. Tunajua jinsi inavyowakatisha tamaa wachezaji wanaposema wanahitajika lakini pia wanahitajika kwa ajili ya nchi.
"Si haki kwa wachezaji. Tunatatua tatizo hili kwa ajili yetu barani Afrika na kwa ajili ya wachezaji wetu wa Afrika," alisema.
Katika hatua nyingine, Dk. Motsepe ametangaza ongezeko la zawadi ya Bingwa wa AFCON mwaka huu kutoka Dola za Kimarekani Milioni 7 hadi Milioni 10.
Dk. Motsepe pia amesema CAF itatoa Dola Milioni 1 kwa kila Shirikisho la Soka la nchi mwanachama wake kama sehemu ya mpango wake kusaidia na kuendeleza mchezo huo barani.



.png)
0 comments:
Post a Comment