• HABARI MPYA

    Wednesday, July 02, 2014

    MAXIMO AWATUMA YANGA KUFUATA WABRAZIL WENGINE, KIONGOZI JANGWANI AKWEPA PIPA LEO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIONGOZI mmoja wa Yanga SC amepanda ndege leo kwenda Brazil kwa ajili ya kuwaona wachezaji kadhaa aliolekezwa na kocha Marcio Maximo, ili mmoja wao arejee naye nchini.
    Maximo amewapa Yanga SC mawasiliano na wachezaji kadhaa wa Kibrazil wanaocheza nchini humo, ili wakawaone na wakiridhika nao waje nao nchini.
    BIN ZUBEIRY inafahamu Yanga SC inataka kuongeza Mbrazil mmoja tu baada ya kiungo Andrey Coutinho aliyesaini Mkataba wa miaka miwili wiki hii.
    Andrey Coutinho amesaini miaka miwili Yanga SC na sasa klabu hiyo inataka kusajili Mbrazil mwingine

    Na mpango uliopo Yanga SC ni kuachana na Mganda Hamisi Kiiza iwapo itafanikiwa kumpata Mbrazil huyo, kwa kuwa idadi ya wachezaji wa kigeni katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwisho watano.
    Tayari Yanga SC inao beki Mbuyu Twite, kiungo Haruna Niyonzima kutoka Rwanda, Coutinho wa Brazil, Kiiza na Emmanuel Okwi wote wa Uganda- maana yake ili kuongeza mchezaji mwingine wa kigeni itatakiwa kupunguza mmoja na Diego wa Kampala yuko kwenye hatari hiyo.
    Yanga SC imekwishaanza mazoezi rasmi chini ya makocha wake wapya, Wabrazil Marcio Maximo na Msaidizi wake, Leonardo Neiva, asubuhi ikijifua katika fukwe za Coco na jioni Uwanja wa Chuo cha Bandari, Tandika mjini Dar es Salaam.
    Yanga SC itashiriki Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Kagame mwezi ujao mjini Kigali, Rwanda na ikirudi itafungua pazia la msimu wa Ligi Kuu kwa kumenyana na mabingwa Azam FC katika mechi ya Ngao ya Jamii mwezi ujao.
    Mapema mwakani, Yanga SC iliyomaliza nafasi ya pili msimu uliopita katika Ligi Kuu, itashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAXIMO AWATUMA YANGA KUFUATA WABRAZIL WENGINE, KIONGOZI JANGWANI AKWEPA PIPA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top