• HABARI MPYA

    Wednesday, July 02, 2014

    BILA KUMALIZA TOFAUTI ZAO, ITAKUWA KAZI SANA SIMBA KURUDI KWENYE MSTARI

    MWISHONI mwa wiki Simba SC ilifanya uchaguzi wake mkuu katika bwalo la Maofisa wa Polisi, Oyster Bay, Dar es Salaam na kupata viongozi wapya.
    Evans Elieza Aveva alichaguliwa kuwa Rais wa klabu hiyo, wakati Geoffrey Hiriki Nyange ‘Kaburu’ akachaguliwa kuwa Makamu wa Rais.
    Iddi Kajuna, Said Tulliy, Collins Frisch, Ally Suru na Jasmine Badour walichaguliwa kama Wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
    Zoezi la mchakato mzima wa uchaguzi huo unaofuatia uongozi wa Alhaj Ismail Aden Rage kumaliza muda wake, liligubikwa na mgogoro ulioigawa klabu hiyo pande mbili.

    Upande wa kwanza ambao ndiyo ulikuwa na watu wengi ni ule uliomuunga mkono Aveva na kundi lake la Friends Of Simba, wakati upande mwingine ni uliomuunga mkono mgombea aliyeenguliwa, Michael Richard Wambura.
    Wambura alienguliwa mara mbili, kwanza akidaiwa si mwanachama halali wa klabu hiyo, kwa sababu aliwahi kuipeleka klabu hiyo mahakamani na FIFA inakataza masuala ya soka kupelekwa mahakama za dola.
    Kwa kosa hilo, Wambura akakata rufaa Kamati ya Rufani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambako alishinda na kurejeshwa kwenye mbio.
    Akitaja hukumu yake, Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani ya TFF, Wakili Julius Lugaziya alisema kwamba amemrejesha Wambura kwa sababau, Simba wenyewe walikwishamrejesha na kumuingiza hadi kwenye Kamati ya Utendeaji.
    Lugaziya alisema, baada ya kosa alilolifanya Wambura kuipeleka klabu mahakamani, lakini aliendelea kuhudhuria mikutano, kulipia ada zake za uanachama hata akateuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji.
    Wambura akafanya kosa lingine, wakati anazungumza namna alivyoyapokea maamuzi ya Kamati ya Rufani, akajikuta anazungumza maneno ambayo mbele ya Kamati ya Uchaguzi ya Simba SC yalitafsiriwa kuwa ya kikampeni, wakati muda wa zoezi hilo ulikuwa haujafika.
    Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Dk Damas Daniel Ndumbaro ikamuengua tena Wambura kwa kosa la kufanya kampeni kabla ya muda, hivyo amekiuka kanuni za uchaguzi.
    Wambura akakata tena Rufaa TFF, kwa bahati mbaya kwake, akakwama na kuwa ameondolewa moja kwa moja kwenye uchaguzi.
    Wafuasi wake wakafungua kesi mahakama ya dola, wakitaka uchaguzi uzuiliwe, lakini kwa kuwa hawakujipanga vizuri na hawakuwa na hoja, wakakwama na uchaguzi ukafanyika Jumapili.
    Wazi kundi ambalo lilimuunga mkono Aveva ndilo limeibuka mshindi baada ya sakata zima hili- lakini ukienda ndani zaidi, unaweza kustaajabu kwa nini wana Simba wawe maadui wao kwa wao?
    Inafahamika Simba SC kama timu, mahasimu wao ni Yanga SC- hao ndiyo wa kushindana nao na kuwekeana chuki labda, ingawa katika soka ya dunia ya leo nayo hiyo si sawa sana.
    Dunia ya leo upinzani wa soka unaishia uwanjani, watu wakikutana kwenye vilinge vingine wanaendelea kufurahia pamoja.
    Ndiyo maana, mtu wa Yanga anaoa wa Simba, na kwa pamoja tunategemeana katika mahitaji mbalimbali. Baba anazaa mtoto ni timu tofauti na yake, lakini hata akijiita Simba au Yanga tofuti na baba yake, lakini atabaki kuwa mtoto wa fulani tu. Hatuna uadui siku hizi kwenye mpira, unakwenda uwanjani, timu yako inafungwa 5-0 unarudi nyumbani taratibu na ukifika wa kwanza wa kukutania mwanao, au mkeo.
    Hiyo maana yake sasa mpira ni furaha na si uadui na ni ushamba mkubwa kuifikisha dhana ya upinzani wa mpira kwenye uadui.
    Hivyo basi, wana Simba SC lazima wajue kwamba kuendelea kuwa na matabaka miongoni mwao ni kuharibu taswira ya klabu yao.
    Kila kitu kilichosimama imara lazima kiwe na msingi wake ujenzi- basi itakuwa vyema Evans Elieza Aveva awe msingi wa kurejea kwa umoja na amani ndani ya klabu hiyo.
    Kweli, Wambura alikosea, lakini kuendelea kupambana naye na kutaka kumkomoa, au kumuadhibu kwa makosa aliyoyafanya kutakuza uhasama.
    Na hakuna sababu ya kukuza uhasama baina ya wana Simba, ikiwa tunaweza kujiridhisha kwamba michezo ni furaha na si chuki.
    Wambura mbishi, wengi wetu tunamjua. Kuomba radhi ni jambo gumu kwake hata kama kweli naye anajua amekosea, bali ataendelea kupambana tu kwa njia nyingine.
    Basi kama ni hivyo, na kwa kuwa uchaguzi umefanyika kwa amani na viongozi wapya wameptikana, vyema wana Simba wakazika tofauti zao na kurudisha umoja katika klabu yao.
    Umoja ni raha, tena kwa namna zote na haswa ikizingatiwa kaulimbiu ya Simba SC ni Nguvu Moja- basi Aveva alitazame kwa kina hilo hivi sasa yeye kama kiongozi mkuu wa klabu. 
    Naamini, kama Simba SC na Yanga SC hawatazika tofauti zao, basi itakuwa kazi sana kurudi kwenye mstari. Ramadhani njema. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BILA KUMALIZA TOFAUTI ZAO, ITAKUWA KAZI SANA SIMBA KURUDI KWENYE MSTARI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top