• HABARI MPYA

    Saturday, October 31, 2009

    MGOSI AIUA YANGA, SIMBA POINTI 30...


    BAO pekee la Mussa Hassan Mgosi, leo katika dakika ya 26, liliiwezesha Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga, mbele ya mashabiki zaidi ya 60,000 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Mgosi alifunga bao hilo baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Yanga na kuunganisha vyema krosi ya Mganda, Emanuel Okwi, ambaye jana alikuwa mwiba mchungu kwa ngome ya Yanga.
    Kwa ushindi huo, mbali na kulipa kisasi cha kufungwa 1-0, Oktoba 26, mwaka jana kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi msimu uliopita, Simba pia imezidi kujiimarisha kileleni, ikifikisha pointi 30 baada ya kucheza mechi 10, yaani imeshinda mechi zake zote.
    Kocha wa Simba, Patrick Phiri, alijivunia washambuliaji wake wenye kasi kina Okwi, Mrwanda na Mgosi, waliowapa wakati mgumu mabeki wa Yanga.
    Yanga jana ilionekana kuathiriwa na mfumo wake iliotumia, kujaza viungo wengi na kucheza na mshambuliaji mmoja tu, wakati wapinzani wao walikuwa wakishambulia kupitia pembezoni mwa uwanja.
    Kocha Kosta Papic, ambaye alipowasili nchini alisema kutokana na mfumo wake wa kushambulia timu yoyote anayoiongoza haiwezi kutoka uwanjani bila kufunga bao, jana alishuhudia mwamuzi Orden Mbaga akipuliza kipyenga cha kuhitimisha mchezo huo, Yanga ikiwa haijaziona nyavu za Simba.
    Kipigo hicho kwa Yanga kinawafanya sasa wazidiwe pointi 12 na wapinzani wao hao wa jadi kwenye Ligi Kuu, jambo ambalo sasa litawafanya wasubiri miujiza ili kutetea ubingwa wao.
    Simba itaumana na Mtibwa Sugar katika mchezo wake wa kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi, wakati Yanga itamaliza na Prisons yenye ari mpya baada ya kupata kocha mpya, Oscar Dan Korosso.
    Simba: Juma Kaseja, Salum Kanoni, Juma Jabu, Kelvin Yondani, Joseph Owino, Mohamed Banka, Danny Mrwandea, Hillary Echesa, Mussa Mgosi, Emanuel Okwi/David Naftali na Ramadhan Chombo/Uhuru Suleiman.
    Yanga; Obren Curkovic, Nsajigwa Shdrack, Amir Maftah, Mohamed Bakari, Wisdom Ndhlovu, Athumani Iddi, Mrisho Ngassa, Nurdin Bakari, Boniphace Ambani/Jerry Tegete, Abdi Kassim/Mike Barasa na Kiggi Makassy/Moses Odhiambo.


    Phiri amzidi hesabu Papic

    MOJA kati ya vitu vilivyoiponza Yanga leo kufungwa 1-0 na Simba, ni mfumo wake wa uchezaji, kujaza viungo wengi uwanjani na kucheza na mshambuliaji mmoja tu, Boniphace Ambani, ambaye msimu huu ameonekana kupoteza makali.
    Kosta Papic, kocha wa Yanga, alikwenda kulala jana akijutia mfumo wake huo, kwani mwenzake, Phiri kwa kujaza washambuliaji watatu mbele, Mussa Mgosi, Emanuel Okwi na Danny Mrwanda, kulimpa faida ya ushindi na kufanya mashambulizi mengi pia.
    Papic alishindwa hata kutumia mwanya wa Simba kumpoteza mshambuliaji wake Danny Mrwanda, aliyepewa kadi nyekundu dakika ya 52, kwa kumtolea maneno machafu mwamuzi Orden Mbaga akiwa tayari ana kadi ya njano, hivyo kutolewa nje kwa nyekundu.
    Papic aliingiza kiungo mwingine uwanjani, Moses Odhiambo, akiwaacha kwenye benchi washambuliaji Jerry Tegete na Mike Barasa.
    Mambo yalibadilika kidogo wakati Papic alipowaingiza Tegete na Barasa dakika nane za mwishoni, lakini wakati huo tayari Phiri alikuwa amekwishawaelekeza wachezaji wake kucheza kwa kulinda bao hilo.
    Hakika Yanga walitafuta kila njia ya kutafuta bao, tangu Mussa Mgosi alipowatungua dakika ya…, lakini kutokana na kukosa washambuliaji mbele, kila mchezaji aliyepata alitaka kuutengeneza.
    Si kama Yanga ilizidiwa mchezo na Simba jana, bali maarifa ya uwanjani na hicho ndicho pekee ambacho kitampa jeuri Phiri.


    Kaseja ni kiboko ya Yanga

    PAMOJA na ukweli kwamba safu ya ulinzi ya Simba ni madhubuti, lakini pia kipa Juma Kaseja ni shujaa wa kweli langoni, baada ya leo kuokoa michomo mingi ya wazi, ambayo mbele ya kipa ‘wasiwasi’, Yanga ingeweza kuvuna zaidi ya mabao matatu.
    Kaseja aliwakatisha tamaa kabisa Yanga, kutokana na kucheza kwa umakini wa hali ya juu, akiokoa michomo ya hatari na kuituliza timu yake kila ilipoanza kupoteana.
    Kwa kuweza kudaka vyema na kuifanya Simba ishinde 1-0, Kaseja amedumisha rekodi yake ya kusimama kwenye lango la timu hiyo tangu ajiunge nayo mwaka 2002 kwenye mechi zote za Ligi ikicheza na Yanga bila ya kupoteza mchezo.
    Yanga waliweza kupata ushindi mbele ya Simba, Kaseja akiwa langoni mara moja tu, Aprili 20, mwaka 2003, katika mchezo wa kirafiki ulioandaliwa na kampun ya Dika Sharp.
    Siku hiyo Yanga ilishinda mabao 3-0, wafungaji wakiwa ni Kudra Omary dakika ya 30, Heri Morris dakika ya 32 na Salum Athumani dakika ya 47.
    Zaidi ya hapo, Kaseja amedaka tangu mwaka 2002, kabla ya msimu uliopita kuhamia Yanga kwa mkataba wa msimu mmoja, lakini mara zote hizo amekuwa akishangilia ushindi na wachezaji wenzake wa Simba.
    Hata alipokuwa Yanga msimu uliopita, Kaseja aliiongoza kulazimisha sare ya 2-2 na Yanga katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu, baada ya awali Obren Curkovic kudaka vyema na kuifanya Yanga ishinde 1-0.
    Alipokuwa Yanga msimu uliopita, Simba haikuweza kufua dafu kwa Watoto wa Jangwani, lakini msimu huu amerejea na kuwafanya Wekundu wa Msimbazi wafufue ubabe wao.
    Mapema tu kabla ya mechi hiyo, Kaseja alisema, Yanga hawawezi kuifunga Simba yeye akiwa langoni - na hilo limetimia, je, kwa nini asijiite ni kiboko ya Yanga?


    Mgosi ajisafisha Msimbazi
    SIMBA walikuwa wamekwishapoteza imani na Mussa Hassan Mgosi - kwamba ni mchezaji ambaye hawezi kuifunga Yanga hata akibaki anatazamana na nyavu, lakini kwa bao lake pekee lililoipa timu hiyo ushindi leo, bila shaka amejisafisha mbele ya viongozi, wanachama na wapenzi wa timu hiyo.Katika mchezo wa kwanza baina ya Simba na Yanga, Oktoba 26, mwaka jana, Mgosi alikosa mabao mawili ya wazi, siku ambayo, Yanga iliibuka na ushindi wa 1-0 kwa bao pekee la Ben Mwalala.
    Wakati mchezo wa marudiano unawadia Aprili 19, mwaka huu, Mgosi alikuwa ana mwaliko wa kwenda kufanya majaribio katika klabu ya Mahindra United ya India, hivyo Simba kwa kujua kwamba hata akibakia hawezi kuifunga Yanga, uongozi ulimruhusu kwenda India.
    Lakini huko mambo hayakumwendea vizuri Mgosi, akarejea Simba na hatimaye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu baina ya miamba hiyo, alikuwa uwanjani na alichokifanya aliwadhihirishia yote ya nyuma yalikuwa bahati mbaya.
    Hii ni mara ya pili kwa Mgosi kuifunga Yanga tangu ajiunge na Simba mwaka 2005, akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro. Mara ya kwanza ilikuwa ni kwenye Kombe la Tusker Julai 2, mwaka 2005 wakati Simba ilipoibuka na ushindi wa 2-0 kwenye fainali.
    Siku hiyo Mgosi alichokifanya ni kushindilia msumari wa moto kwenye jeneza la Yanga kwa kufunga bao la pili dakika ya 72, kufuatia Emmanuel Gabriel kufunga la kwanza dakika ya 60.

    Banka: Si nilisema, Yanga wamefulia


    KIUNGO Mohamed Banka, leo baada ya mchezo huo, alikumbusha kauli yake aliyoitoa kwamba; Yanga watake wasitake watafungwa Oktoba 31, mwaka huu, kwani hicho ndicho kilitokea.
    Akizungumza na DIMBA, Banka alisema kwamba alijua utakuwa mchezo mgumu, lakini kitu ushindi kwa timu yake Simba alikiona mapema mno.
    “Nilijua utakuwa mchezo mgumu, lakini kitu ushindi kwetu nilijua lazima kipo, tulipata upinzani mkali uwanjani, lakini mwishowe timu bora ilitoka kifua mbele,” alisema Banka.
    Banka, ambaye huu ni msimu wake wa tatu Simba, tangu ajiunge nayo akitokea Yanga, jana aling’ara licha ya kukabiliwa na upinzani mkali wa viungo vijana wadogo kama Athumani Iddi, Kiggi Makassy, Nurdin Bakari na mkongwe Abdi Kassim.
    Wakati anaachwa Yanga, moja ya sababu zilikuwa ni kwamba alitaka fedha nyingi za usajili wake, uwezo wake unaelekea kufikia mwisho, lakini alipotua kwa Wekundu wa Msimbazi, amekuwa kama amezaliwa upya.


    Arsenal yapeta England

    ARSENAL leo iliibuka kidedea kwenye Ligi Kuu ya England, baada ya kuichapa Tottenham Hotspurs mabao 3-0, katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Emirates, London.
    Ushindi huo, umeifanya Arsenal itimize pointi 25, baada ya kucheza mechi 11, hivyo kupanda kileleni kwa muda ikiipiku Chelsea, iliyokuwa ikiongoza Ligi hiyo kwa pointi zake 24. Hata hivyo, Chelsea ilikuwa inamenyana na Bolton jana, mchezo ambao ikishinda inabakia kileleni.
    Hadi mapumziko Arsenal ilikuwa mbele kwa mabao 2-0, yaliyotiwa kimiani na Robin Van Persie dakika ya 42 na Cesc Fabregas dakika ya 43.
    Arsenal ilipata bao lake la pili dakika ya 60, mfungaji akiwa ni Van Persie tena, ambaye jana alikuwa mwiba mchungu kwa ngome ya Spurs.
    Kikosi cha Arsenal kilikuwa; Almunia, Sagna, Vermaelen, Gallas, Clichy, Diaby, Fabregas, Song, Arshavin/Eboue, Van Persie/Ramsey na Bendtner/Eduardo.
    Tottenham; Gomes, Bassong, Corluka, King, Assou-Ekotto, Bentley, Huddlestone/Bale, Jenas, Palacios, Keane/Pavlyuchenko na Crouchyellow.



    Kaizer Chiefs, Orlando hakuna mbabe

    JOHANNESBURG, Afrika Kusini
    WAPINZANI wa jadi nchini Afrika Kusini, Kaizer Chiefs na Orlando Pirates, leo wametoka sare ya bila kufungana katika mchezo wa Ligi Kuu ya nchi hiyo, uliofanyika kwenye Uwanja Loftus Versfeld, wenye uwezo wa kumeza mashabiki 94,700.
    Katika mchezo huo, kila timu iliumiliki mpira kwa asilimia 50, Kaizer ikilenga mashuti nane langoni mwa Pirates, kucheza faulo tisa, kupata kona tatu na kuokoa hatari mbili, huku wachezaji wake wawili wakipewa kadi za njano.
    Pirates yenyewe ililenga mashuti matano langoni kwa Kaizer, kucheza faulo saba, kupata kona tatu, kuotea mara moja, kuokoa hatari tano langoni mwao na mchezaji wake mmoja kupewa kadi ya njano.
    Kaizer itaijutia nafasi waliyopata dakika ya 90, wakati Siphiwe Tshabalala alipopiga shuti kwa guu lake la kushoto kutoka umbali wa mita 25, lakini likagonga mwamba.
    Pirates nayo ilipata nafasi dakika hiyo hiyo, baada ya Langu Sweswe wa Kaizer Chiefs kumchezea rafu Thembinkosi Fanteni, lakini Lucky Lekgwathi alipokwenda kupiga adhabu ndogo, haikuwa na madhara.
    Kikosi cha Kaizer kilikuwa Bartman, Tau, Jambo, Rooi, Dladla, Letsholonyane, Nale, Nengomasha, Sweswe, Tshabalala na Motaung Jnr.
    Pirates: Josephs, Jele, Lekgwathi, Thwala, Mahamutsa, Gumbi, Jali, Mabalane, Mashego, Mbuyane na Modise.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MGOSI AIUA YANGA, SIMBA POINTI 30... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top