• HABARI MPYA

    Thursday, June 19, 2014

    BIN SLUM WAKAMATA TIMU YA TATU LIGI KUU, WAMWAGA MAMILIONI NDANDA YA MTWARA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KAMPUNI ya Bin Slum Tyres Limited, leo imesaini Mkataba wa udhamini na timu ya tatu ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Ndanda FC ya Mtwara.
    Bin Slum ambayo awali iliingia mikataba na Mbeya City ya Mbeya na Stand United ya Shinyanga, sasa inakuwa kampuni inayodhamini timu nyingi zaidi za Ligi Kuu, ikifuatiwa TBL, wanaozidhamini Simba na Yanga.
    Mkurugenzi wa Bin Slum Tyres, Nassor Bin Slum amesema katika Mkutano na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam kwamba, wameingia Mkataba wa mwaka mmoja na Ndanda wenye thamani ya Sh. Milioni 50.
    Mkurugenzi wa Bin Slum Tyres, Nassor Bin Slum kulia akitiliana saini mikataba ya udhamini na Katibu wa Ndanda FC, Edmund Kunyengana kushoto
    Wanabadilishana mikataba
    Ndoa mpya Ligi Kuu
    Makabidhiano ya jezi

    Bin Slum amesema kwamba katika Mkataba huo, Ndanda watavaa jezi zenye nembo ya matairi ya Vee Rubber kwa mbele pamoja na kuweka mabango ya bidhaa hizo kwenye mechi ao za nyumbani, Uwanja wa Nangwanda Sijaona.  
    Bins Slum amesema sababu za kuamua kuwekeza kwenye klabu hiyo mpya katika Ligi Kuu iliyopanda msimu huu, ni kuitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete aliyeagiza makampuni yasaidie na timu ndogo pia, badala ya kuelekeza nguvu kwa timu kubwa pekee, ambazo tayari zina vyanzo vya mapato.  
    Lakini Bin Slum amesema pia Mtwara ni mkoa mkubwa kibiashara ambako anaamini atanufaika kwa kuuza bidhaa zake kwa wingi. 
    Stand United pia wamepewa Mkataba wa Sh. Milioni kwa mwaka nao watavaa jezi zenye nembo ya matairi ya Double Star yanayosambazwa na kampuni ya Bin Slum katika mechi zake zote msimu wa 2014-2015.
    Aidha, mabango ya Double Star pia yatabandikwa katika mechi za Uwanja wa nyumbani, Kambarage mkoani Shinyanga za timu hiyo.
    Mbeya City ambao watavaa jezi zenye nembo ya betri za RB zinazosambazwa na Bin Slum pia, wao wamepewa Mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Sh. Milioni 360.
    Katibu Mkuu wa Ndanda FC, Edmund Kunyengana Njowoka amefurahia udhamini huo na kusema utakuwa chachu yao wao kufanya vizuri katika Ligi Kuu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BIN SLUM WAKAMATA TIMU YA TATU LIGI KUU, WAMWAGA MAMILIONI NDANDA YA MTWARA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top