• HABARI MPYA

    Thursday, June 19, 2014

    IVORY COAST YALALA 2-1, COLOMBIA WATINGA 16 BORA KOMBE LA DUNIA

    IVORY COAST imejiweka mguu nje, ndani kusonga Raundi ya Pili ya Kombe la Dunia baada ya kufungwa mabao 2-1 na Colombia jioni hii katika mchezo wa Kundi C Uwanja wa Brasilia, Brazil.
    Matokeo hayo yanaifanya Ivory Coast ibaki nafasi ya pili kwa pointi zake tatu baada ya mechi mbili, wakati Colombia inapanda kileleni kwa pointi zake sita na kujihakikishia kutinga 16 Bora moja kwa moja.
    Ivory Coast sasa watalazimika kuifunga Ugiriki katika mchezo wake wa mwisho wa kundi hilo ili kusonga mbele. 
    Colombia ilipata bao lake la kwanza dakika ya 64, mfungaji James Rodriguez aliyeunganisha kona ya Cuadrado.
    Mkongwe Didier Drogba akimuacha chini beki wa Colombia katika mchezo ambao Ivory Coast ililala 2-1 

    Wakati Tembo wanatafuta bao la kusawazisha kwa nguvu zote, shambulizi la kushitukiza liliipa Colombia bao la pili dakika ya 70. Mpira wa adhabu uliopigwa na Yaya Toure uligonga ukuta wa timu hiyo Amerika Kusini na Colombia wakaanzisha shambulizi la haraka.Serey Die alipoteza mpira katikati ya Uwanja na kuwapa nafasi Colombia kufanya shambulizi la kushitukiza kupita kwa Gutierrez, ambaye alimpatia pasi nzuri Juan Quintero aliyemtungua kiulaini kipa Boukacar Barry. 
    Ivory Coast haikukata tamaa hata baada ya kuwa nyuma kwa 2-0 na iliongeza umakini, ikianza kulinda lango na kushambulia kwa ujanja zaidi. Hali hiyo iliwasaidia kupata bao la kufutia machozi dakika ya 74, mfungaji Gervinho ambaye aliwachambua mabeki wa Colombia kabla ya kufumua shuti lililotinga nyavuni.
    Still in with a shot: Gervinho pulled one back for the Elephants after a fine run
    Gervinho akiwatoka mabeki wa Colombia kabla ya kuifungia Ivory Coast bao la pili

    Ivory Coast ilipata uhai zaidi baada ya bao hilo na kusukuma mashambulizi mengi langoni mwa Colombia, lakini bahati haikuwa yao, wakaishia kukosa mabao ya wazi.
    Colombia: Ospina, Armero/Arias dk72, Yepes, Zapata, Zuniga, Sanchez Moreno, Aguilar/Mejia dk78, Ibarbo/Quintero dk53, Rodriguez, Cuadrado na Gutierrez.
    Ivory Coast: Barry, Boka, Bamba, Zokora, Aurier, Die/Bolly dk73, Tiote, Gervinho, Yaya Toure, Gradel/Kalou dk67 na Bony/Drogba dk60.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: IVORY COAST YALALA 2-1, COLOMBIA WATINGA 16 BORA KOMBE LA DUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top