Na Patrick Kahemele, Rabat
AZAM FC ipo mjini Rabat ikijiandaa kukabiliana na wenyeji AS FAR Rabat katika mechi ya hatua ya 16 bora, Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kulazimishwa sware ya bila kufungana nyumbani, Dar es Salaam wiki iliyopita.
Azam FC imetua hapa na wachezaji 23, benchi lote la ufundi isipokuwa, Ibrahim Shikanda pekee aliye masomoni Nairobi na uongozi karibu wote na kwa pamoja kama timu Azam FC ina dhamira ya kuifunga na kuitoa AS FAR.
Kuna sababu sita, ambazo zinaifanya Azam FC iamini na kujiamini kuwa inaweza kushinda kwenye mechi hiyo ya Jumamosi, ambazo ni maandalizi bora, wachezaji wazuri, uongozi Mzuri, benchi bora la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Muingereza Stewart Hall, mipango mizuri na dhamira ya kupata mafanikio.
Katika makala haya, itakayowajia katika sehemu tatu, nitachambua vipengele vilivyoaninishwa hapa chini.
![]() |
| Kocha Mkuu wa Azam, Stewart Hall kulia akiwafuatilia wapinzani wake jana wakicheza mechi ya Ligi ya Morocco. Kushoto Msaidizi wake, Kali Ongala. |
MAANDALIZI MAZURI:
Timu za Tanzania kwa miaka mingi zimekuwa zikishiriki mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na CAF, kwa Azam FC hii ni mara yake ya kwanza kupata nafasi hii. Lakini unaweza kuona tofauti kubwa ya maandalizi kati ya Azam FC na timu nyingi za Tanzania.
Na tofauti hiyo ndiyo inaifanya Azam FC hadi sasa kuweza kucheza mechi tano za mashindano ya Afrika bila kupoteza hata mmoja.
Azam FC baada ya kujua kuwa itawakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa, iliamua kufanya juhudi za makusudi za kujiandaa kwa kiwango cha mashindano hayo yanayoandaliwa na CAF.
Azam FC ilifanya ziara na kucheza mechi nane za kimataifa za kirafiki nje ya ardhi ya Tanzania, ilikwenda Kinshasa nchini DRC, ambako ilishiriki na kutwaa Kombe la Hisani9 nchini hujo Desemba mwaka jana.
Baadaye ilikwenda kushiri na kutwaa Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar kabla ya kusafiri tena hadi Nairobi, Kenya ambako ilipata nafasi ya kucheza mechi nyingine tatu.
Lengo la ziara hizo ilikuwa ni kuwapa ukomavu na uzoefu vijana wake ili wanapokuwa kwenye mashindano ya CAF hasa wanapocheza mechi za ugenini wasiwe na hofu. Hakika matunda ya ziara hizo tunayaona sasa,kwani Azam FC imeshinda ugenini mechi zake zote mbili za awali hadi sasa.
Maadalizi ya Azam FC kwenye mashindano haya pia yalihusisha utafutwaji na usajili wa wachezaji wenye viwango vya kuweza kucheza na kuisaidia timu, uboreshwaji wa kambi ya mazoezi ya Chamazi mapema kwa ajili ya kambi ya nyumbani, ununuzi wa vifaa bora vya mazoezi na kadhalika.
![]() |
| Wachezaji wakiwa mazoezini jana Rabat |
UWEZO WA WACHEZAJI:
Timu ni wachezaji, bila ya wachezaji bora wenye nidhamu, viwango bora na malengo ni sawa na bure. Azam FC ililitambua hilo mapema na haikukurupuka kusaka wachezaji kwa mkupuo, usajili wa wachezaji kwa ajili ya mashindano ya CAF ulifanyika kwa umakini kwa muda mrefu huku klabu ikijiwekea malengo ya kuwa na kikosi bora kitakochoweza kupambana na kuvifunga vigogo vya soka la Afrika.
Leo ukiwaangalia wachezaji 25 wa Azam FC waliosajiliwa kwenye mashindano ya CAF utaungana nami kuwa ni wachezaji sahihi kwa mashindano haya.
Wachezaji wa Azam FC wana nidhamu na vipaji vya hali ya juu. Wote wana viwango vya kuweza kuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na kuanza kwenye kikosi cha kwanza. Hapa nitazungumzia sifa za wachezaji wa eneo la ulinzi tu kwa ufupi na katika sehemu ijayo, nitaelezea sifa za wachezaji wa kiungo na baadaye kumalizia na washambuliaji.
MWADINI ALLY; Ni kipa chaguo la kwanza la kikosi cha timu ya taifa ya Zanzibar na sehemu ya kudumu ya kikosi cha Taifa Stars. Ana uzoefu mkubwa wa michezo ya kimataifa akiiongoza Zanzibar kushika nafasi ya tatu mara mbili kwenye mashindano ya CECAFA Challenge.
Ni kipa hodari ambaye Azam FC inajivunia kuwa naye
AISHI MANULA; Utasemaje juu ya kipaji cha kijana huyu kutoka Mji Kasoro Bahari, Morogoro? Wengi wanamfananisha na kipa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania na klabu za Reading ya England, Coastal Union ya Tanga na Simba SC ya Dar es Salaam, Mwameja Mohammed Mwameja.
Aishi anajiamini, ana umbo zuri na kipaji kikubwa cha kulinda lango. Ndiyo maana haishangazi kwa nini yeye ni kipa namba moja wa timu za vijana za taifa na chaguo namba tatu la Taifa Stars ya kocha Mdenmark, Kim Poulsen mbele ya makipa wazoefu wanaocheza Ligi Kuu kila siku.
HIMID MAO; Ana umri wa miaka 20 tu, lakini ni mkongwe ndani ya kikosi cha Azam FC, Himid ni kiungo mwenye sifa za kukaba ambaye sasa anacheza kama beki wa kulia wa Azam FC. Hakuna aliyeshangaa jina lake lilipoitwa na Kim Poulsen kuwa sehemu ya wachezaji 30 bora nchini wanaonyemelea nafasi za walio timu ya taifa kwa sasa. Himid Mao aliibukia kwenye mashindano ya Copa Coca Cola na baadaye kuwa Nahonda wa kikosi cha vijana wa umri wa chini ya miaka 20.
Tangu kocha wa zamani wa Azam FC, Mbrazil Itamar Amorim ampe nafasi kwenye kikosi cha kwanza akitokea Azam Academy, Himid ameendelea kufanya vizuri hadi sasa, pamoja na kuhamishwa kutoka kiungo hadi beki wa kulia.
WAZIRI SALUM; Huenda ndiye mchezaji mwenye kipaji kikubwa cha kumiliki mpira kuliko wachezaji wote nchini Tanzania kwa sasa.
Waziri Salum, naye yumo kwenye daftari la kocha Kim Poulsen na ni mwanachama wa kudumu wa kikosi cha Zanzibar Heroes. Mguu wake wa kushoto ni kama mkono wa paka, kwani unaweza kufanya lolote na mpira. Ana mbinu za kukaba, ana krosi za hatari na chenga za maudhi. Ni hazina kubwa ya Azam FC na taifa la Tanzania kwa ujumla.
JOACKINS ATUDO; Ni beki bora wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) msimu uliopita, ambaye alitua Azam FC wakati wa dirisha dogo la usajili nchini, Desemba mwaka jana ili kuimarisha ukuta wa Azam FC kwa ajili ya mashindano haya.
Tangu atue Azam FC, Atudo amethibitisha kuwa waliomchagua kuwa beki bora Kenya, hawakukosea.
Wakati Azam inaomba maoni yake kocha wa zamani wa Kenya, Harambee Stars, James Nandwa kabla ya kumsajili Atudo, alisema; “Ukiwa na beki kama Atudo, unapata vitu viwili, kwanza uongozi ndani ya Uwanja na pili beki mwenye kipaji, nguvu, kimo na kujitolea,”.
Hakika kila kocha angependa kuwa na Atudo kwenye kikosi chake.
Kwa Tanzania, tayari amejijengea umaarufu mkubwa kutokana na soka yake maridadi na maarifa ya hali ya juu ukabaji, uzuiaji na uongozaji wa safu ya ulinzi kwa jumla. Pia hupanda kusaidia mashambulizi na kufunga, akiunganisha mipira mirefu kutoka poembeni hususan ya kona.
LUCKSON KAKOLAKI; Labda ndiye mchezaji mwenye busara zaidi kwenye kikosi cha Azam FC, kiasi kwamba wachezaji wenzake wanamuheshimu na kumkubali kama kaka.
Busara hizi za nje ya Uwanja pia unaweza kuziona ndani ya Uwanja, kwani Luckson amekuwa mhimili mkuu kwa Azam FC hasa pale eneo la ulinzi linapokabiliwa na majeruhi. Kiwango chake cha uchezaji kimekuwa cha uhakika wakati wote na hili alilithibitisha kwenye mechi ya awali dhidi ya AS FAR, alipoingia katika dakika ya sita kuchukua nafasi ya Atudo aliyeumia bega na akamudu kucheza kwa ustadi mkubwa. Luckson ni mchezaji mmojawapo, ambaye tunaweza kusema ana damu ya bluu (yaani ana damu yenye rangi ya Azam FC).
DAVID MWANTIKA; Tanzania tumejaaliwa kuwa na mabeki wazuri, lakini hatujawahi kuwa na beki wa kiwango cha David Mwantika tangu kuondoka kwenye ramani ya soka kwa Boniface Pawasa.
![]() |
| Add caption |
Mwantika hapitiki kwa namna yoyote ile. Mwantika ana nguvu za asili na mwili uliojengeka vema kimichezo. Wenyewe Wanyakyusa wanamuita Bedui kwa jina la utani. Mwantika ana kasi ya upepo na amekuwa maarufu ndani ya wachezaji wa Tanzania tangu yupo Prisons ya Mbeya, ambako vyombo vya habari nchini havikumbaini na kumpa sifa zake.
Lakini ukikutana na washambuliaji wa Ligi Kuu, watakuambia kuwa beki wanayemuogopa zaidi nchini ni David. Juzi Kim Poulsen amemjumuisha kwenye kikosi chake B na bila shaka wala wasiwasi, Mwantika atavuka kwenye kikosi cha Young Taifa Stars na kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha Taifa Stars muda si mrefu.
USIKOSE; Sehemu zijazo za mfululizo wa makala haya, yanayoandikwa na Patrick Kahemele, Meneja wa Azam FC, yaliyobeba sababu sita za Azam FC kuing’oa FAR Rabat Afrika.










.png)