![]() |
| Baadhi ya wachezaji wa Stars walio na timu Marakech, Mrisho Ngassa kushoto na Zahor Pazi kulia |
TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imetua mjini Marrakech, Morocco leo- Juni 3 mwaka huu tayari kwa mechi ya Kundi C kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia dhidi ya wenyeji Morocco itakayochezwa Jumamosi- Juni 8 mwaka huu.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imefikia hoteli ya Pullman ambayo pia ilikaa timu ya Ivory Coast ilipokuja kucheza na Morocco. Kikosi hicho kina wachezaji 21 wakati Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu watawasili kesho- Juni 4 mwaka huu saa 8 mchana wakitokea Maputo, Msumbiji ambapo timu yao ya TP Mazembe ilikuwa na mechi ya Kombe la Shirikisho.
Stars imetua hapa ikitokea Ethiopia, ambako iliweka kambi ya wiki moja kwa ajili ya mchezo wa kirafiki ulio katika kalenda ya FIFA jana dhidi ya Sudan kwenye Uwanja wa Addis Ababa.
Katika mchezo huo, Stars ilitoka sare ya bila kufungana na Sudan ikicheza bila washambuliaji wake wake wawili nyota, Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta ambao walikuwa wanaichezea klabu yao, TP Mazembe ya DRC katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Washambualiji wa Stars akina Khamis Mcha ‘Vialli’, Mrisho Ngasa na Amri Kiemba wakiongozwa na John Bocco jana walilitia msukosuko mara kwa mara lango la Sudan ambalo lilikuwa chini ya beki wa kati Nadir Eltayeb ambaye alifanya kazi ya ziada dakika ya 72 kuokoa mpira uliokuwa ukielekea wavuni.
Stars katika mechi hiyo iliwakilishwa na Juma Kaseja, Nadir Haroub/Vincent Barnabas, Shomari Kapombe, Kelvin Yondani, Aggrey Morris, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Salum Abubakar, John Bocco/Haroun Chanongo, Amri Kiemba/Khamis Mcha na Simon Msuva/Athuman Iddi ‘Chuji’. Kocha Kim Poulsen amesema kikosi chake kinaendelea na mazoezi vizuri na kitaimarika zaidi baada ya Samatta na Ulimwengu kujiunga na wenzao kesho huu mjini Marrakech.
Mechi kati ya Stars na Morocco itachezwa kuanzia saa 3 usiku kwa saa za Morocco ambapo nyumbani Tanzania itakuwa ni saa 5 usiku.



.png)