![]() |
| Miraj kulia akimshuhudia baba yake mkubwa, Edward Hizza akimsainia. Kushoto ni kaimu Mwenyekiti wa Simba SC, Joseph Itang'are 'Kinesi' |
BEKI chipukizi wa kushoto wa Simba SC, Miraj Adam amekamilisha idadi ya wachezaji chipukizi waliopandishwa kutoka kikosi cha pili kusaini mikataba ya kuchezea kikosi cha kwanza.
Miraj mwenye umri wa miaka 17, ambaye ameonyesha uwezo mkubwa akichezea kikosi cha kwanza cha Simba SC msimu huu, amesainiwa na baba yake mkubwa, Edward Hizza jioni ya leo, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa sheria za mikataba, kijana aliye chini ya umri wa miaka 18 atasainiwa na wazazi au walezi wake rasmi, hivyo mshambuliaji huyo wa zamani wa Pamba FC ya Mwanza amemsainia mtoto wa ndugu yake.
Makinda wengine waliosainiwa Simba SC kutoka timu B, ni kipa Abuu Hashimu, Ramadhani Kipalamoto, William Lucian ‘Gallas’, Hassan Hatibu, Said Ndemla, Ramadhani Singano ‘Messi’, Haroun Chanongo, Rashid Ismail, Edward Christopher, Jonas Mkude na Hassan Isihaka.
Pamoja na kupandisha makinda hao, Simba SC katika kikosi chake cha msimu ujao imeonekana kuelekeza nguvu kwa wachezaji wenye umri mdogo zaidi.
Kwani imesajili chipukizi watatu kutoka timu za vijana za taifa, Twaha Shekuwe ‘Messi’ wa Coastal Union, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ wa Mtibwa Sugar na Zahor Pazi wa Azam FC aliyekuwa anachezea JKT Ruvu kwa mkopo. Wachezaji wengine waliosajiliwa Simba SC ni kipa Andrew Ntalla kutoka Kagera Sugar na beki Mganda, Samuel Ssenkoom kutoka URA ya Uganda, ambao wote hawazidi umri wa miaka 25.
Simba SC pia iko mbioni kumsajili kiungo mshambuliaji wa Uganda, Moses Oloya, mwenye umri wa miaka 20, anayecheza soka ya kulipwa Vietnam.
Simba SC imepania kujiimarisha baada ya msimu mbaya uliopita, ikipoteza ubingwa wa Ligi Kuu mikononi mwa wapinzani wao wa jadi, Yanga SC na kukosa hata nafasi ya pili, ikizidiwa kete na Azam FC.



.png)