“SAFINA”
“NGANO
“UNGA
“UNGA
“WATER”
HABARI MOTOMOTOHABARI ZA NYUMBANI

SIMBA SC YAAMBULIA SARE 1-1 ZANZIBAR, RSB BERKANE WAONDOKA NA KOMBE

NDOTO za Simba SC kutwaa Kombe la Shirikisho Afrika hazikutimia leo baada ya kutoa sare ya kufungana bao 1-1 na Renaissance Sportive de Berkane ya Morocco katika mchezo wa marudiano wa Fainali Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Matokeo hayo yanamaanisha RSB Berkane wanatwaa taji la CAF Confederation Cup kwa ushindi wa jumla wa 3-1 kufuatia kushinda mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza Jumamosi iliyopita Uwanja wa Manispaa ya Berkane mjini Berkane.

Katika mchezo wa leo Simba SC walitangulia kwa bao la Mzambia, Joshua Mutale Budo dakika ya 17 akimalizia pasi ya winga mwenzake, Mkongo Elie Mpanzu Kibisawala – kabla ya kiungo wa Kimataifa wa Mali, Soumaila Sidibe kuisawazishia RSB Berkane dakika ya 90’+3.

Refa Dahane Beida wa Mauritania alimtoa kwa kadi nyekundu kiungo Yusuph Ally Kagoma dakika ya 50 kufuatia kumuonyesha kadi ya pili ya njano kwa kucheza rafu.

Mshambuliaji Mganda, Steven Dese Mukwala aliunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu wa kiungo Muivory Coast, Jean Charles Ahoua dakika ya 76 na kufunga – licha ya refa kukubali bao hilo, lakini akabatilisha maamuzi yake baada ya msaada wa Marudio ya Picha za Video (VAR) kufuatia kughasiwa na wachezaji wa RSB Berkane.

Hii inakuwa mara ya tatu kwa RSB Berkane kutwaa CAF Confederation Cup baada ya mwaka 2020 na 2022, mwaka ambao pia walitwaa taji la CAF Super Cup.

Kwa Simba SC imekuwa mara ya pili wanamalizia nyumbani Fainali za CAF na kushindwa kutwaa taji baada ya mwaka 1993 pia kufungwa 2-0 na Stella Adjame ya Ivory Coast Uwanja wa Taifa, sasa Uhuru Jijini Dar es Salaam kufuatia kutoa sare ya bila mabao awali Jijini Abidjan.

Kwa ujumla hii inakuwa mara ya tatu kwa timu za Tanzania kufika Fainali na kushindwa kutwaa Kombe, kwani na Yanga SC ilifika Fainali Kombe la Shirikisho mwaka juzi, 2023 nayo ilipoteza taji kwa kuruhusu mabao nyumbani baada ya sare ya jumla ya 2-2, ikifungwa 2-1 Dar es Salaam na kushinda 1-0 Algeria dhidi ya USM Alger.

Pamoja na kupewa Kombe jipya, RSB Berkane wanapatiwa kitita cha Dola za Kimarekani Milioni 2, huku washindi wa pili, Simba SC wakipata Dola Milioni 1.

Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Mousa Camara, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’/ Valentin Nouma dk84, Che Malone Fondoh/ Leonel Ateba dk84, Chamou Karaboue, Fabrice Ngoma, Yusuph Kagoma, Jean Charles Ahoua, Steven Mukwala, Joshua Mutale/Kibu Dennis dk71 na Elly Mpanzu.

ZAWADI ZA KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA

NAFASIZAWADI YA FEDHA
BingwaUS$2,000,000
Mshindi wa PiliUS$1,000,000
Nusu FanaliUS$750,000
Robo FainaliUS$550,000
Mshindi wa tatu wa KundiUS$400,000
Mshindi wa Nne wa KundiUS$400,000

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button