CAF YAUHAMISHIA ZANZIBAR MCHEZO WA MARUDIANO SIMBA NA BERKANE

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limeagiza mchezo wa marudiano wa Fainali ya Kombe la Shirikisho baina ya Simba na RSB Berkane uhamishiwe Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Kwa mujibu wa barua ya CAF jana iliyosainiwa na Katibu wa Bodi hiyo ya kandanda barani, Mkongo mwenye Uraia wa Uswisi pia, Veron Mosengo-Omba sababu za mabadiliko hayo ni Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao upo katika marekebisho wakati huu kutokuwa tayari kwa mchezo huo Mei 25.
Barua hiyo ya Mosengo-Omba iliyoelekezwa kwa Katibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imesema kwamba taarifa za kina na za Kitaalamu za wakaguzi wa CAF zinaonyesha Uwanja huo hautakuwa tayari kwa matumizi ya mchezo huo mkubwa wiki ijayo, hususan kutokana na tatizo kubwa la Pitch yake na mvua zinazoendelea hivi sasa Dar es Salaam.
Mechi ya kwanza ya Fainali ya Kombe la Shirikisho itachezwa Jumamosi kuanzia Saa 4:00 usiku Uwanja wa Manispaa ya Berkane nchini Morocco.