PSG WAICHAPA INTER MILAN 5-0 NA KUTWAA TAJI LA LIGI YA MABINGWA ULAYA
TIMU ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa usiku wa jana imefanikiwa kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Inter Milan ya Italia katika mchezo wa Fainali Uwanja wa Allianz Arena Jijini Munich nchini Ujerumani.
Mabao ya PSG yalifungwa na beki Mmorocco, mzaliwa wa Hispania Achraf Hakimi Mouh dakika ya 12,washambuliaji Mfaransa, mwenye asili ya Ivory Coast, Désiré Nonka-Maho Doué mawili dakika ya 20 na 63, Khvicha Kvaratskhelia wa Georgia dakika ya 73 na kiungo Senny Mayulu mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) dakika ya 86.
Unakuwa msimu mzuri zaidi kwa PSG wakiukamilisha kwa kutwaa jumla ya mataji matatu na Ligi ya Ufaransa, Kombe la Ufaransa na UEFA Champions League katika usiku ambao mshambuliaji chipukizi wa umri wa miaka 19, Désiré Doué alijipambanua kwenye ulimwengu wa soka kwa mabao yake mawili aliyofunga.
Nani angemuhitaji Lionel Messi, Neymar na Kylian Mbappé wakati yupo Doue? PSG wanayo majibu ya hilo baada ya hatimaye kukamilisha muda mrefu wa kusubiri kutwaa taji la kwanza la Ligi ya Mabingwa Ulaya wakiw ana kikosi chenye nyota chipukizi kuliko kile kilichokuwa kinaundwa na wachezaji ghali nyota.
Ushindi huo unamfanya Kocha wa PSG, Luis Enrique awe Kocha wa pili tu kihistoria kutwaa mataji matatu na timu mbili tofauti baada ya Mspaniola mwenzake, Pep Guardiola.
SAFARI YA PSG HADI KUSHINDA TAJI
HATUA YA LEAGUE:
W4 D1 L3 F14 A9 (Nafasi ya 15)
HATUA YA MTOANO PLAY-OFF:
Brest 10-0 agg (3-0 a, 7-0 h)
HATUA 16 BORA:
Liverpool 1-1 agg, aet, 4-1pens (0-1 h, 1-0 a)
ROBO FAINALI:
Aston Villa 5-4 agg (3-1 h, 2-3 a)
NUSU FAINALI:
Arsenal 3-1 agg (1-0 a, 2-1 h)
FAINALI:
Inter 5-0
VINARA WA TIMU
MFUNGAJJI BORA:
Ousmane Dembélé (Mabao 8)
MTOA ZA ASSISTS NYINGI:
Ousmane Dembélé (Mabao 6)
ALIYECHEZA ENEO KUBWA:
João Neves (Kilomita 184.3)
ALIYEKUWA NA KASI ZAIDI:
Achraf Hakimi (Kilomita 36.9 kwa Saa)
ALIYECHEZA DAKIKA NYINGI:
Willian Pacho (1,542)
ALIYFUNGA POINTI NYINGI ZA FANTASY:
Achraf Hakimi (125)