TANZANIA PRISONS YAICHAPA COASTAL UNION 2-1
WENYEJI, Tanzania Prisons wameibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
Mabao ya Tanzania Prisons yamefungwa na kiungo Ezekia Mwashilindi dakika ya 27 na winga Beno Khalfan Ngassa dakika ya 76, kabla ya kiungo Bakari Suleiman Msimu kuifungia bao la kufuatia machozi Coastal Union dakika ya 90.
Kwa ushindi huo, Tanzania Prisons inafikisha pointi 30 na kusogea nafasi ya 11, wakati Coastal Union inabaki na pointi zake 31 nafasi ya nane baada ya wote kucheza mechi 28.
Ligi Kuu inashirikisha timu 16 na mwisho wa msimu mbili zitashuka daraja, huku tayari Ken Gold yenye pointi 16 za mechi 23 imeshashuka daraja.
Timu nyingine mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana zenyewe katika mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu, wakati atakayetolewa atakwenda kucheza na timu ya Championship kujaribu tena kurudi Ligi Kubwa.
Kutoka Championship timu zilizopanda Ligi Kuu moja kwa moja na mabingwa, Mtibwa Sugar na washindi wa pili, Mbeya City — wakati Stand United na Geita Gold zitamenyana kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini kutafuta nafasi ya kucheza timu itakayoporomoka Ligi Kuu kujaribu tena kupanda.