ERIK TEN HAG ALIYETIMULIWA MAN UNITED ATUA BAYER LEVERKUSEN

KLABU ya Bayer Leverkusen imemtambulisha Mholanzi Erik ten Hag kuwa kocha wake mpya akichukua nafasi ya Mspaniola, Xabi Alonso aliyetimkia Real Madrid ya kwao.
Ten Hag, ambaye amewahi Akufundisha Bayern Munich II kati ya mwaka 2013 na 2015 alikuwa hana kazi tangu atimuliwe na Manchester United Oktoba mwaka jana kwa matokeo mabaya.
Leverkusen walimaliza katika nafasi ya pili katika Bundesliga msimu huu, lakini bado wanajivunia kikosi kilichowasaidia kushinda taji hilo bila kupoteza mechi msimu uliotangulia, 2023-2024.
Ten Hag, 55, alikaa kwa zaidi ya misimu miwili Old Trafford kabla ya kufutwa kazi huku kukiwa na matokeo mabaya miezi mitano tu baada ya kushinda Kombe la FA – ingawa hata baada ya kuondoka kwake Man United imeendelea kusuasua.
Mrithi wake Ruben Amorim amefanikiwa kushinda mechi saba pekee za Ligi Kuu ya England na kumaliza katika nafasi ya 15, ingawa ameifikisha Fainali ya Europa League ambako walifungwa na Tottenham Hotspur.
Kabla ya kujiunga na United, Ten Hag alishinda mataji matatu ya Eredivisie nchini Uholanzi akiwa na Ajax na kuiongoza timu hiyo kutinga Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2018- 2019.