TFF NA YANGA NGOMA BADO MBICHI KABISA


Yanga imegoma kucheza Fainali ya Kombe la TFF, michuano inayodhaminiwa na Benki ya CRDB msimu huu hadi itakapolipwa Fedha zake za zawadi za msimu uliopita.
Fainali ya Kombe la CRDB imepangwa kufanyika Juni 28 Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar – Yanga ikikutana na Singida Black Stars.
Afisa Habari wa Yanga SC, Ally Shaaban Kamwe aliwaambia Waandishi wa Habari juzi kwamba hatua hiyo inafuatia kuvumilia kwa muda mrefu kusubiri kupatiwa zawadi yao.
Baada ya tamko hilo la Yanga, mapema jana wadhamini wa Kombe la TFF, Benki ya CRDB walitoa taarifa ikisema zawadi za bingwa na mashindano ya msimu uliopita kwa ujumla walikabidhi kwa bodi hiyo ya kandanda nchini.
Nao TFF jana mchana wakajibu wakisema hawajaipa Yanga fedha za zawadi za msimu uiopita kwa sababu klabu hiyo iliomba kwa maandishi wakatwe fedha hizo kwa malipo ya madeni yao mbalimbali.
Jana hiyo hiyo Yanga wakajibu tena wakisema kwa misimu yote mitatu ya nyuma ya ushindi wao wa Kombe la TFF tangu wakati wa udhamini wa Azam Media Limited haijalipwa fedha za zawadi.
Kiini cha mgogoro wa Yanga na TFF ni mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara dhidi ya watani wao, Simba SC uliopangwa kufanyika Jumapili wiki hii kuanzia Saa 11:00 jioni Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Yanga imegoma kucheza mechi hiyo hadi matakwa yao matatu kati ya manne yatakapofanyiwa kazi – ambayo ni Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi pamoja ijiuzulu, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Almasi Kasongo ajiuzulu,Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao naye ajiuzulu — na la nne ambalo ni la muda mrefu nyundo mpya wa Bodi Huru ya Ligi.
Awali mchezo huo ulipangwa kufanyika Machi 8 hapo hapo Uwanja wa Mkapa — lakini TPLB ikaufuta kufuatia Simba kutishia kutoingiza timu ikidai kuzuiwa kufanya mazoezi Machi 7, siku moja kabla ya mechi kwa mujibu wa kanuni.
Bodi ya Ligi ilitangaza rasmi kuuahirisha mchezo huo mchana wa Machi 8, lakini Yanga walikwenda uwanjani na kufanya mazoezi kabla ya kuondoka na baadaye kufungua kesi Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa ya Michezo (CAS).
Hata hivyo CAS ilikataa kusikiliza kesi ya Yanga kutaka ipewe ushindi na kuagiza irejeshe malalamiko yake kwenye mamlaka za nchini.
Wakati wa sakata hilo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ilikutana na viongozi wa klabu zote, Bodi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ingawa haikuwahi kutoa majibu yoyote juu ya mkutano huo uliohudhuriwa pia na viongozi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Pamoja na kususia mchezo huo, Yanga imekazia kama matakwa hayo matatu ya kujiuzulu kwa viongozi hao hawatacheza na mechi nyingine mbili za mwisho za Ligi na msimu ujao hawatashiriki ligi pia.