SULEIMAN MWALIMU AREJEA WYDAD ATHLETIC TAYARI KWA KLABU BINGWA YA DUNIA

KIUNGO mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Suleiman Mwalimu Abdallah ‘Gomez’ ameondoka kwa jana usiku Jijini Bloemfontein kwa gari kwenda Johannesburg kuunganisha usafiri wa ndege kurejea Morocco kujiunga na klabu yake, Wydad Athletic tayari kwa safari ya Marekani kwenye michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia ya FIFA.
Mwalimu alikuwa Afrika Kusini kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ambacho juzi kilicheza mechi ya kirafiki ya Kimataifa na wenyeji, Bafana Bafana ambayo ilimalizika kwa sare ya bila mabao Uwanja wa Peter Mokaba Jijinin Polokwane.
Na juzi usiku akasafiri na Taifa Stars kwenda Bloemfontein kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Kundi C Kombe la Mataifa ya Kusini mwa Afrika (COSAFA) ambao walifungwa 1-0 na Madagascar Uwanja wa Toyota Free States.
Lakini Mwalimu hakucheza baada ya kuumia katika mazoezi ya awali kufuatia kuumia jicho baada ya kugongana na mwenzake wakati akipiga kichwa, hivyo kuondolewa kwenye kikosi cha kwanza nafasi yake ikichukuliwa na Alphonce Mabula Msanga anayechezea Shamakhi FK ya Azebairjani.

Katika Klabu Bingwa ya Dunia ya FIFA inayotarajiwa kuanza Juni 14 hadi Julai 13, Wydad imepangwa Kundi G pamoja na Manchester City ya England, wababe wa Italia Juventus na Al Ain ya Falme za Kiarabu (UAE).