MBAPPE AWA MCHEZAJI BORA WA MSIMU REAL MADRID

MSHAMBULIAJI wa KImataifa wa Ufaransa, Kylian Mbappé (26) ameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu wa Real Madrid ya Hispania kufuatia mwanzo mzuri katika msimu wake wa kwanza akifunga jumla ya mabao 42 kwenye mashind ao yote sambamba na pasi nne za mabao ya wengine katika mechi 55 alizocheza.
“Ni furaha na wakati mzuri kwangu. Ningependa kuwashukuru wana Madridista wote walionipigia kura. Ulikuwa msimu wangu wa kwanza nchini Hispania, uzoefu mpya kama mchezaji na kama mtu, na nina furaha sana kuwa hapa,” Alisema Mbappe baada ya kushinda Tuzo hiyo.
Mbappé anafuata nyayo za Jude Bellingham (21) na Vinicius Jr. (24), ambao nao walishinda Tuzo hiyo misimu miwili iliyotangulia na sasa anaelekeza ngugu zake katika michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia ya FIFA, michuano itakayofanyika mwezi Juni nchini Marekani – Los Blancos wakiwa wamepangwa Kundi H pamoja na Al-Hilal, Pachuca na Red Bull Salzburg.
Mbappe amekuwa Mfungaji Bora wa La Liga kwa mabao yake 31, ingawa Real Madrid imevuliwa ubingwa kwa kumaliza nafasi ya pili, nyuma ya Barcelona.
Mbappe anakuwa mchezaji wa kwanza wa Ufaransa kuwa Mfungaji Bora wa La Liga tangu Karim Benzema (37) alipofanya hivyo akiwa na Real Madrid pia msimu wa 2021-22.
Kabla ya Klabu Bingwa ya Dunia ya FIFA, Mbappé anatarajiwa kuiongoza Les Bleus katika Nusu Fainali ya michuano ya UEFA Nations League dhidi ya Hispania wiki ijayo – hayo yakiwa marudiano ya Nusu Fainali ya Euro 2024, ambayo La Roja ilishinda 2-1.