AZIZ KI ATOKEA BENCHI WYDAD IKIKANDWA 2-0 NA MAN CITY

ALIYEKUWA kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki alitokea benchi kipindi cha pili usiku wa jana timu yake mpya, Wydad Athletic ya Morocco ikichapwa mabao 2-0 na Manchester City ya England katika mchezo wa Kundi G Kombe la Klabu Bingwa ya Dunia Uwanja wa Lincoln Financial Field, Philadelphia, Marekani.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Ramon Abatti wa Brazil — Aziz Ki akiyejiunga na Wydad Aprili mwaka huu baada ya misimu mitatu ya kuwa Yanga, aliingia dakika ya 84 kuchukua nafasi ya kiungo wa Kimataifa wa Afrika Kusini, Thembinkosi Christopher ‘Nyoso’.
Mbele ya mashabiki 37,446 waliofurika Lincoln Financial Field — mabao ya Man City yalifungwa na kiungo Philip Walter Foden wa England dakika ya pili na winga Mbelgiji, Jérémy Baffour Doku dakika ya 42.
Kiungo mshambuliaji Mtanzania, Suleiman Abdallah Mwalimu alisalia benchi muda wote wa mchezo akiishuhudia Wydad yake ikianza michuano hiyo ya FIFA.

Mechi nyingine ya Kundi hilo, Juventus ya Italia iliitandika ya Falme za Kiarabu (UAE) mabao 5-0 Uwanja wa Uwanja wa Audi Field, Washington, D.C.
Mabao ya Kibibi Kizee cha Turin yamefungwa na Kolo Muani dakika ya 11′ na 45+4, Conceição dakika ya 21 na 58 na Yıldız dakika ya 31.
Nayo Real Madrid ya Hispania ikalazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Al-Hilal ya Saudi Arabia katika mchezo wa Kundi H Uwanja wa Hard Rock, Miami Gardens.
Mbele ya mashabiki 62,415 katika mchezo uliochezeshwa na refa Facundo Tello wa Argentina — mshambuliaji chipukizi wa miaka 21, Gonzalo García Torres alianza kuifungia Real Madrid dakika ya 34, kabla ya kiungo Mreno, Rúben Diogo da Silva Neves kuisawazishia Al-Hilal dakika ya 41.
Mechi nyingine ya Kundi H, Red Bull Salzburg ya Austria iliichapa Pachuca ya Mexico mabao 2-1 Uwanja wa TQL Stadium, Cincinnati.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Mualgeria, Mustapha Ghorbal mabao ya Red Bull Salzburg yalifungwa na kiungo Muisrael, Oscar Gloukh dakika ya 42 na mshambuliaji wa Austria Karim Onisiwo mwenye asili ya Nigeria dakika ya 76′, huku la Pachuca likifungwa na Bryan González dakika ya 56.