GOR MAHIA WATAKA KUIPELEKA MASHEMEJI DERBY HOME BAY

KLABU ya Gor Mahia inatazama uwezekano wa kuhamishia mechi na mahasimu wao, ‘Mashemeji Derby’ dhidi ya AFC Leopards Uwanja wa Raila Odinga uliopo Homa Bay baada ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kupendekeza tarehe mpya ya mchezo huo ambayo ni kati ya Jumapili ya Juni 1 na Jumatatu ya Juni 2.
Awali mchezo huo ulipangwa kuchezwa mwanzoni mwa Mei, lakini ukaahirishwa kwa sababu ya ukosefu wa Uwanja unaofaa baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuishauri FKF dhidi ya kutotumia Uwanja wa Kasarani, ambao kwa sasa unafanyiwa ukarabati kwa ili michuano ya CHAN.
Gor Mahia walitaka kuuhamishia mchezo huo Uwanja wa Ulinzi Sports Complex, ambao hata hivyo uwezo wake wa kuingiza watazamaji ni mdogo, mashabiki 8,000 – hivyo wakaomba wapewe muda Zaidi wapate Uwanja mpya.
Gor Mahia walifikiria pia kuupeleka mchezo huo Uwanja wa Kimataifa wa Nyayo, lakini nao pia unafanyiwa ukarabati na hata mashindano ya Riadha yamehamishiwa Ulinzi Sports Complex.
Uwanja wa Homa Bay uliopo eneo la Luo Nyanza, ni ngome ya Gor Mahia na klabu hiyo inafurahia uungwaji mkono mkubwa katika eneo hilo.