WIZARA YAIRUHUSU SIMBA KUFANYA MAZOEZI MKAPA KESHO KUJIANDAA NA ‘DERBY’ JUMAPILI

KLABU ya Simba imepokea barua rasmi kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ikiuhusiwa kufanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kesho kuelekea mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara Jumapili dhidi ya mahasimu, Yanga Jumamosi.
Kwa mujibu wa barua hiyo iliyosainiwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Boniface Tamba kwa niaba ya Katibu wa Wizara hiyo – Simba ndio walioanza kuiandikia wizara kuomba ruhusa ya kufanya mazoezi siku moja kabla ya mechi; “Wizara haina kipingamizi na timu kufanya mazoezi ya mwisho kabla ya mechi kwa mujibu wa kanuni,” imesema barua hiyo na kuongeza;
“Wizara inapenda kusistiza kwamba itaendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi wa vilabu vyote nchini wanaoomba kutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa na vingine vyote vilivyopo chini ya Wizara bila ya kukwamisha kwa namna yoyote matumizi ya viwanja hivyo,”.

Barua hii inatoka siku moja baada ya Simba SC kusema kwamba itapeleka kikosi chake Uwanja wa Mkapa Jumapili kwa ajili ya mchezo huo na haitakuwa tayari kucheza mechi hiyo tarehe nyingine tofauti na Juni 15.
Na tangu jana Bodi ya Ligi imekuwa ikisistiza inaendelea na maandalizi ya mchezo huo, ingawa wenyeji wa mechi hiyo, Yanga nao wamesistiza hawatocheza hata baada ya kikao na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) Jumanne Jijini Dar es Salaam.
Awali mchezo huo ulipangwa kufanyika Machi 8 hapo hapo Uwanja wa Mkapa – lakini TPLB ikaufuta kufuatia Simba kutishia kutoingiza timu ikidai kuzuiwa kufanya mazoezi Machi 7, siku moja kabla ya mechi kwa mujibu wa kanuni.
Bodi ya Ligi ilitangaza rasmi kuuahirisha mchezo huo mchana wa Machi 8, lakini Yanga wakikwenda uwanjani na kufanya mazoezi kabla ya kuondoka na baadaye kufungua kesi Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS).
Hata hivyo CAS ilikataa kusikiliza kesi ya Yanga kutaka ipewe ushindi na kuagiza irejeshe malalamiko yake kwenye mamlaka za nchini. Wakati wa sakata hilo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ilikutana na viongozi wa klabu zote, Bodi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ingawa haikuwahi kutoa majibu yoyote juu ya mkutano huo uliohudhuriwa pia na viongozi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Yanga imekwenda mbali na kutishia kususia hata mechi nyingine mbili za kumalizia msimu dhidi ya Tanzania Prisons na Dodoma Jiji pamoja na kujitoa kwenye Ligi ya msimu ujao wapo matakwa yao matatu Kati ya manne hayatatimizwa.
Matakwa hayo ni Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ijiuzulu, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Almasi Kasongo ajiuzulu, Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao naye ajiuzulu — na la nne ambalo ni la muda mrefu nyundo mpya wa Bodi Huru ya Ligi.
Kwa ujumla Yanga wapo katika mgogoro mkubwa na TFF kwa sasa – kwani tayari wametishia pia kutocheza Kombe la TFF, michuano inayodhaminiwa na Benki ya CRDB msimu huu hadi itakapolipwa Fedha zake za zawadi za msimu uliopita.
Fainali ya Kombe la CRDB imepangwa kufanyika Juni 28 Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar – Yanga ikikutana na Singida Black Stars.
TFF kwa upande wao wanasema ndio wanaidai Yanga na fedha hizo wamekata kufidia madeni hayo.
TFF iliomba kukutana na viongozi wa Yanga kujadili madeni yao ili kinachobaki wapewe, lakini uongozi wa klabu ulikataa na kusema hautaki kikao isipokuwa fedha zao ziingizwe kwenye akaunti yao.