RONALDO AIPELEKA URENO FAINALI LIGI YA MATAIFA ULAYA

MWANASOKA bora wa dunia wa zamani, Cristiano Ronaldo jana aliifungia bao la ushindi Ureno ikitoka nyuma na kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya wenyeji, Ujerumani katika mchezo wa Nusu Fainali wa LIgi ya Mataifa ya Ulaya ya UEFA Uwanja wa Allianz Arena Jijini Munich.
Winga wa Juventus, Francisco Conceicao alifuga bao la kwanza la Ureno dakika ya 63, kabla ya Ronaldo anayechezea Al-Nassr ya Saudi Arabia kufunga la ushindi dakika tano baadaye kufuatia kiungo mshambuliaji wa Bayer Leverkursen, Florian Wirtz anayetakiwa na Liverpool kuanza kuifungia Ujerumani dakika ya 48.
Lilikuwa bao la 137 anaifungia timu yake ya taifa, Ronaldo mwenye umri wa miaka 40 sasa katika jumla ya mechi 220 alizocheza hadi jana, ambazo zote ni rekodi za dunia.
Mara ya mwisho Ureno kuifunga Ujerumani ilikuwa ni miaka 25 iliyopita kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Ulaya, Euro 2000 kabkla ya kufungwa mechi tano mfululizo zilizofuata huku Ronaldo akicheza mechi zote hizo.
Kwa ushindi wa jana, Ureno inaingia Fainali ya michuano hiyo iliyoanzishwa mwaka 2019 na itakutana na ama bingwa wa mwaka 2021, Ufaransa au bingwa wa mwaka 2023, Hispania Jumapili hapo hapo Munich.
Ujerumani itawania nafasi ya tatu na timu itakayofungwa kwenye Nusu Fainali ya pili leo kati ya Ufaransa na Hispania kuanzia Saa 3:00 usiku Uwanja wa MHPArena Jijijni Stuttgart. Mechi ya mshindi wa tatu pia itachezwa hapo hapo MHPArena.
Wakati Ureno itakuwa inawania taji la pili baada ya kuweka rekodi ya kuwa mabingwa wa kwanza wa michuano hiyo mwaka 2019 – Ujerumani watajaribu kurejesha heshima angalau tangu walipofungwa 1-0 na Urusi kwenye Fainali ya walipotwaa Kombe la Mabara la FIFA mwaka 2017.