NASSOR IDRISA ‘FATHER’ KIGOGO MPYA BODI YA LIGI, MWAYELA KAIMU CEO

MWENYEKITI wa klabu ya Azam FC, Nassor Idrisa ‘Father’ ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kukaimu nafasi ya Stephen Mnguto aliyejiuzulu.
Aidha, Meneja wa Fedha wa TPLB, Ibrahim Mwayela ameteuliwa kukaimu nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo kufuatia kusimamishwa kwa Almasi Kasongo.
Kwa mujibu wa barua kwenda kwa klabu, viongozi hao wawili ndio watakaoiongoza Bodi hiyo kabla ya uchaguzi wa viongozi wapya Agosti mwaka huu.
Pamoja na kuwa Mwenyekiti wa Azam FC, Father pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo – na anakuwa kiongozi wa pili wa Azam FC kuwa kiongozi Mkuu wa TPLB baada ya Shiekh Said Mohamed (sasa marehemu).

Nassor Idrisa ‘Father’ (kulia) akiwa na Wakurugenzi wa Azam FC, Abubakar Bakhresa (kushoto) na Yusuph Bakhresa (katikati).
Mnguto alijiuzulu Juni 13 siku ambayo pia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitoa taarifa ya kumsimamisha kazi Kasongo, ambayo inatafsiriwa na kutii matakwa manne ya klabu Yanga ambayo ni kujiuzulu kwa Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo na Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao — na la nne ambalo ni la muda mrefu, iundwe Bodi mpya Huru ya Ligi.
Yanga ilitoa masharti hayo na ikishurtisha yatimizwe ndio wacheze mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara dhidi ya mahasimu, Simba ambao sasa umepangwa kufanyika Juni 25 Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Na hatua hiyo ilifuatia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk, Samia Suluhu Hassan kukutana na kuzungumza na viongozi wa Simba na Yanga Ikulu, Chamwino Jijini Dodoma, kabla ya TPLB kutoa taarifa ya kuusogeza mchezo huo kutoka Juni 15 hadi 25.
Awali mchezo huo ulipangwa kufanyika Machi 8 hapo hapo Uwanja wa Mkapa – lakini TPLB ikaufuta kufuatia Simba kutishia kutoingiza timu ikidai kuzuiwa kufanya mazoezi Machi 7, siku moja kabla ya mechi kwa mujibu wa kanuni.
Bodi ya Ligi ilitangaza rasmi kuuahirisha mchezo huo mchana wa Machi 8, lakini Yanga wakikwenda uwanjani na kufanya mazoezi kabla ya kuondoka na baadaye kufungua kesi Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS).
Hata hivyo, CAS ilikataa kusikiliza kesi ya Yanga kutaka ipewe ushindi na kuagiza irejeshe malalamiko yake kwenye mamlaka za nchini.

Nassor Idrisa ‘Father’ (kulia) akiwa na Mkurugenzi wa Azam FC, Omar Bakhresa (kushoto).
Wakati wa sakata hilo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ilikutana na viongozi wa klabu zote, Bodi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ingawa haikuwahi kutoa majibu yoyote juu ya mkutano huo uliohudhuriwa pia na viongozi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Yanga ilikwenda mbali na kutishia kususia hata mechi nyingine mbili za kumalizia msimu dhidi ya Tanzania Prisons na Dodoma Jiji pamoja na kujitoa kwenye Ligi ya msimu ujao wapo matakwa yao matatu Kati ya manne hayatatimizwa.
Kwa ujumla uliibuka mgogoro mkubwa baina ya Yanga na TFF – kwani klabu hiyo ilitishia pia kutocheza Fainali ya Kombe la TFF, michuano inayodhaminiwa na Benki ya CRDB msimu huu hadi itakapolipwa Fedha zake za zawadi za msimu uliopita.
Fainali ya Kombe la CRDB imepangwa kufanyika Juni 28 Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar – Yanga ikikutana na Singida Black Stars.
TFF kwa upande wao walisema ndio wanaidai Yanga na fedha hizo wamekata kufidia madeni hayo.
TFF iliomba kukutana na viongozi wa Yanga kujadili madeni yao ili kinachobaki wapewe, lakini uongozi wa klabu ulikataa na kusema hautaki kikao isipokuwa fedha zao ziingizwe kwenye akaunti yao.