AISHI MANULA ASAFIRI NA SIMBA SC ZANZIBAR MECHI NA BERKANE

KIPA Aishi Salum Manula amesafiri na kikosi cha Simba kwenda Zanzibar kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo wa marudiano wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RSB Berkane ya Morocco Jumapili.
Katika mchezo huo utakaoanza Saa 10:00 jioni Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Simba inatakiwa kushinda 3-0 ili kutwaa taji hilo au ishinde 2-0 na bingwa apatikane kwa mikwaju ya penalti.
Aishi hakusafiri na timu katika mchezo wa kwanza Simba ikifungwa 2-0 Jumamosi iliyopita (Mei 17, 2025) Uwanja wa Manispaa ya Berkane mjini Berkane nchini Morocco.
Mabao ya RSB Berkane yalifungwa na kiungo Msenegal, Mamadou Lamine Camara dakika ya nane na mshambuliaji Oussama Lamlaoui la pili dakika ya 14.
Tayari CAF imesema bingwa wa Kombe la Shirikisho atapewa Kombe jipya kama ilivyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika, ambayo yatazinduliwa kesho katika ofisi za wadhamini wakuu, TotalEnergies Jijini Johannesburg, Afrika Kusini – Hafla itakayoanza Saa 12:00 jioni na kuhudhuriwa na magwiji wa soka barani Afrika.