PSG NA REAL MADRID ZAGONGANA SOKONI KUSAKA SAINI YA BEKI WA LIVERPOOL
KLABU za PSG na Real Madrid zinapigana vikumbo kuwania saini ya beki wa kati wa Liverpool, Mfaransa Ibrahima Konaté mwenye asili ya Mali.
Pamoja na mawindo hayo ya vigogo hao wa Ulaya, lakini mkataba wa Konaté ambaye wazazi wake wanatokea Mali utamalizika mwaka 2026.
Milan Skriniar, ambaye kwa sasa yuko kwa mkopo Fenerbahçe, anatarajiwa kuondoka PSG kabisa mwishoni mwa msimu huu, jambo ambalo limesababisha klabu hiyo kuanza kusaka mbadala wake kuimarisha safu ya ulinzi.
Dalili za PSG kuvutiwa na Konaté zilianza Februari mwaka huu iliporipotiwa kwamba PSG walikuwa wakimfuatilia kwa karibu, na kuzua mazungumzo ya uwezekano wa kurejea katika mji wake.
Beki huyo mzaliwa wa Paris alipitia akademi ya Paris FC kabla ya kuwenda Ujerumenia kujiunga na RB Leipzig iliyomkuza na sasa anaaminika kuwa miongoni mwa walengwa wakuu wa PSG majira haya ya joto.