• HABARI MPYA

  Jumatatu, Mei 24, 2021

  NI RAJA NA PYRAMIDS TENA NUSU FAINALI KOMBE LA SHIRIKISHO

  WENYEJI, Raja Athletic wamefanikiwa kutinga Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa 4-0 dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini katika mchezo wa marudiano wa Robo Fainali jana Uwanja wa Mohamed V Jijini Casablanca, Morocco.
  Pongezi kwa nyota wa kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Ben Malango Ngita aliyefunga mabao mawili dakika ya sita na 36, wakati mabao mengine yalifungwa na washambuliaji wenzake, Wamorocco Mahmoud Benhalib dakika ya 22 na Soufiane Rahimi dakika ya 31.
  Kwa matokeo hayo, Raja Casablanca wanakwenda Nusu Fainali kwa ushindi wa jumla wa 5-1 baada ya sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza wiki iliyopita Jijini Johannesburg, Afrika Kusini na sasa itakutana na Pyramids ya Misri, mechi ya kwanza ikichezwa Cairo Juni 20 na Casablanca Juni 27.


  Ikumbukwe Raja na Pyramids zilikuwa pamoja Kundi D na Nkana FC ya Zambia na Namungo ya Tanzania. Katika mechi zilizozikutanisha timu hizo, Raja ilishinda zote, 3-0 Casablanca na 2-0 Cairo.
  Pyramids imeitoa Enyimba ya Nigeria kwa jumla ya mabao 5-2 baada ya sare ya 1-1 ugenini na ushindi wa 4-1 nyumbani, wakati Cotonsport ya Cameroon iliwatoa wenyeji, Jaraaf kwa bao la ugenini baada ya ushindi wa 1-0 nyumbani na kufungwa 2-1 jana Uwanja wa Lat Dior mjini Thies, Senegal na JS Kabylie ya Algeria imeitoa CS Sfaxien ya Tunisia kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya sare ya 1-1 ugenini na ushindi wa 1-0 nyumbani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NI RAJA NA PYRAMIDS TENA NUSU FAINALI KOMBE LA SHIRIKISHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top