• HABARI MPYA

  Jumatatu, Oktoba 19, 2020

  ZAMALEK NAO WABISHA HODI FAINALI LIGI YA MABINGWA AFRIKA

  VIGOGO wa Misri, Zamalek wamebisha hodi Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Raja Club Athletic waliotawazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Morocco, maarufu kama Botola Pro hivi karibuni.
  Na aliyewazimisha Raja ni Mmorocco mwenzao, Achraf Bencharki aliyerejea Uwanja wa Mohamed V Jijini Casablanca na kufunga bao pekee katika mchezo huo wa Nusu Fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa usiku wa kuamkia leo.
  Mchezaji huyo wa zamani wa Wydad Club Athletic alifunga bao hilo pekee dakika ya 18 akimalizia pasi ya Ahmed Sayed 'Zizo' na sasa The White Knights watahitaji kwenda kuulinda ushindi huo mwembamba kwenye mchezo wa marudiano Uwanja wa Kimataifa wa Cairo Jumamosi ijayo ili waende fainali.

  Huo unakuwa ushindi wa pili wa Zamalek dhidi ya Raja kwenye mechi tatu za michuano ya klabu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
  Kwa Raja, hicho ni kipigo cha pili tu katika mechi 23 za Ligi ya Mabingwa Afrika walizocheza nyumbani, wakati Zamalek waliingia kwenye mchezo huo wakiwa na rekodi ya kushinda mechi moja tu ugenini katika mechi 13.
  Ushindi wa Zamalek umeendeleza wikiendi nzuri kwa timu za Misri Jijini Casablanca baada ya Al Ahly nayo kuifunga Wydad 2-0 katika Nusu Fainali nyingine ya kwanza Jumamosi na sasa mahasimu hao wa Jiji la Cairo wanaweza kukutana wenyewe kwenye fainali kama watazitoa timu za Morocco.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ZAMALEK NAO WABISHA HODI FAINALI LIGI YA MABINGWA AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top