• HABARI MPYA

  Jumamosi, Agosti 01, 2020

  NAHODHA CAMEROON KOMBE LA DUNIA 1990 AFARIKI DUNIA

  GWIJI wa Cameroon, Stephen Tataw amefariki dunia jana Julai 31, 2020 Jijini Yaounde baada ya kuugua kwa muda mfupi.
  Shirikisho la Soka Cameroon (FECAFOOT) limethibitisha kifo cha Tataw aliyeaga dunia akiwa ana umri wa miaka 57.
  Stephen Tataw anayeheshimika kama mmoja wa wachezaji bora zaidi kuwahi kutokea katika historia ya soka ya Cameroon, hadi kifo chake alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa FECAFOOT. 

  Moja ya matukio yake ya mwisho kuonekana hadharani ilikuwa ni kwenye upangwaji wa ratiba ya Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) Cameroon 2020 iliyofanyika Februari 17, mwaka huu Jijini Yaounde, ambako alikuwa akimsaida gwiji mwenzake, Salomon Olembe kuendesha droo hiyo.
  Tataw alikuwa Nahodha wa kikosi maarufu cha Cameroon miaka ya 1990, ‘Class of 1990’ ambacho kilipamba vichwa vya habari wakati wa Fainali za Kombe la Dunia 1990 nchini Italia baada ya kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Afrika kufika Robo Fainali ya michuano hiyo.
  Beki huyo wa kulia pia alikuwa Nahodha wa Simba Wasiofungika kwenye Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1994 nchini Marekani. 
  Mafanikio yake makubwa ni kushinda Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 1988 nchini Morocco. 
  Tataw alianzia kwenye klabu za Tonnere Yaounde na Olympic Mvolye za nyumbani kwao kabla ya kujiunga na Tosu Future mwaka 1995, akiweka rekodi ya kuwa Mwafrika wa kwanza kucheza soka ya kulipwa Japan.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NAHODHA CAMEROON KOMBE LA DUNIA 1990 AFARIKI DUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top