• HABARI MPYA

    Sunday, February 09, 2014

    SEIF MAGARI ASEMA MANENO HAYO, HUWEZI AMINI NI YEYE, BUSARA TUPU MWANZO MWISHO...AMALIZIA NA KUWAPELEKA YANGA CHAMAZI KUISHANGILIA AZAM

    Na Prince Akbar, Dar es Salaam
    MWENYEKITI wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa ya klabu ya Yanga SC, Seif Ahmed ‘Magari’ ametoa shukrani za dhati kwa wale wote waliofanikisha maandalizi ya mchezo wao wa jana wa kwanza wa Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Komorozine ya Comoro.
    Yanga SC jana ilitanguliza mguu mmoja Raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kufuatia ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Komorozine ya Comoro jioni hii katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali, Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Asanteni; Seif Magari akiwa na Emmanuel Okwi

    Washambuliaji Mrisho Khalfan Ngassa alifunga mabao matatu, Mrundi Didier Kavumbangu mawili, Mganda Hamisi Kiiza moja na lingine beki Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’.
    Kwa ushindi huo, Yanga sasa inahitaji sare au kufungwa si zaidi ya mabao 6-0 katika mchezo wa marudiano wiki mbili zijazo ugenini ili kusonga mbele, ambako itakutana na Al Ahly ya Misri.
    Seif Magari amesema anawashukuru wale wote waliotoa ushirikiano kwao hadi kufanikisha kwa mechi hiyo ambayo iliisha kwa salama, amani na furaha ya ushindi.
    Aidha, Seif amewashukuru mashabiki waliojitokeza na kuishangilia timu hiyo, kwani kitaalamu shabiki ni mchezaji wa 12, hivyo anaamini walichangia kwa kiasi kikubwa ushindi huo.
    Seif amewataka mashabiki kuendelea kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu yao katika mechi zijazo za ligi na michuano ya Afrika. Amewashukuru pia mashabiki wa wapinzani wao wa jadi, Simba SC kwa kujitokeza kwenye mchezo wa jana na kusema huo ni moyo wa kizalendo, kwani ushindi wa Yanga jana umeipa sifa Tanzania kwa ujumla.
    Shukrani zaidi Seif amezipeleka kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya rais wake, Jamal Malinzi kwa ushirikiano mkubwa walioipa klabu hiyo hadi kufanikisha maandalizi ya mchezo huo na akaomba jambo hilo liendelee.
    “Kwa kweli tunashukuru sana, namshukuru Malinzi na TFF yake kwa ushirikiano waliotupa. Nawashukuru wote ambao kwa namna moja au nyingine walifanikisha maandalizi ya mchezo huu, hapo kuna jeshi la Pilisi, Vyombo vya Habari, Kamati za Ulinzi na Usalama na wadau mbalimbali. Tunawashukuru sana,”alisema milionea huyo maarufu muuza magari ya kisasa nchini.
    Seif amewataka wapenzi wa Yanga kwenda kuisapoti Azam FC leo katika mchezo wao wa kwanza wa Raundi ya Awali, Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Ferroviario de Beira ya Msumbiji Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    “Tuonyeshe moyo wa kizalendo kwa kwenda kuisapoti Azam, Chamazi si mbali, nakumbuka kuna wakati ilitokea dharula Simba na Yanga zikawa zinachezea mechi zao Uwanja wa Chamazi, na mashabiki walikuwa wanakwenda kwa wingi, hivyo ninaomba sana twendeni tukaisapoti Azam,”alisema Seif Magari. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SEIF MAGARI ASEMA MANENO HAYO, HUWEZI AMINI NI YEYE, BUSARA TUPU MWANZO MWISHO...AMALIZIA NA KUWAPELEKA YANGA CHAMAZI KUISHANGILIA AZAM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top