TANZANIA imefanikiwa kwenda Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17(AFCON U17) baada ya ushindi wa penalti 4-3 kufuatia sare ya kufungana mabao 3-3 na Algeria jioni ya leo Pitch 11 ya Uwanja wa Mohammed VI Football Academy Jijini Sale Kaskazini Magharibi mwa Morocco.
Mabao ya Serengeti Boys yamefungwa na washambuliaji wake tegemeo, Dissmas Shida Athanas mawili dakika ya 25 na 61 na Luqman Ally Mbalasalu dakika ya 45’+8, wakati ya Algeria yamefungwa na winga wa kushoto, Mouhammad Valmy mawili naye dakika ya nne na 40 na beki wa kati, Noam Benramdane dakika ya 65.
Katika mikwaju ya penalty walioifungia Tanzania ni Razack Mbegelendi, Erick Lupuga, Luqman Mbalasalu na Hassan Kizinga na walioifungia Algeria ni Ilyes Mekkaoui, Khalid Touali na Ayoub Dahmas huku Noam Benramdane na Mouhamed Valmy wakikosa.
Unakuwa mwaka mzuri kwa Serengeti Boys kwa Tanzania katika ushiriki wake wa michuano ya U17 ya wavulana, ikiweka rekodi nyingine ya kwenda Nusu Fainali baada ya kuvuka hatua ya makundi kwa mara ya kwanza sambamba na kufuzu Kombe la Dunia.
Mafanikio hayo yanakuja Tanzania ikishiriki kwa kwa mara ya tatu AFCON U17 baada ya mwaka 2017 nchini Gabon na 2019 nyumbani, Tanzania ambako mara zote walitolewa katika hatua ya makundi.



.png)
0 comments:
Post a Comment