• HABARI MPYA

    Saturday, August 08, 2020

    SIMBA YAMTAMBULISHA RASMI MORISSON, YANGA SC WASEMA WATACHUKUA HATUA ZA MFANO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imemtambulisha winga Mghana, Bernard Morisson kuwa mchezaji wake mpya, huku klabu yake, Yanga SC ikisema itachukua hatua za kisheria.
    Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Simba SC imeposti picha tatu za Morrison akiwa na jezi ya klabu hiyo akitia dole gumba na kusaini fomu na kuambatanisha maelezo; “MORRISON IS RED #NguvuMoja”.
    Hata hivyo, tofauti na taarifa nyingi za usajili wa klabu hiyo, zimekuwa zikisema mchezaji amesaini mkataba na wa muda gani – lakini hii ya leo imesema tu “Morrison ni Mwekundu”.
    Muda mfupi baadaye watani wao wa jadi, Yanga SC wakatoa barua pia kupitia ukurasa wao wa Instagram wakisema kwamba Morisson bado ni mchezaji wao na ana mkataba hadi mwaka 2022 hivyo watachukua hatua kali na za mfano. 
    Simba SC imeposti picha tatu za Morrison na kuambatanisha maelezo; “MORRISON IS RED #NguvuMoja”.

    “Uongozi unawataka wanachama na wapenzi wa Yanga kuwa watulivu, kwani Bernard Morisson ana mkataba na klabu yetu hadi 2022 na shauri baina yake na klabu bado lipio mikononi mwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Jumatatu litaendelea kusikilizwa,” imesema taarifa ya Yanga.
    Morrison alijiunga na Yanga SC Januari mwaka huu kama mchezaji huru kwa mkataba wa miezi sita, lakini baada ya mwanzo wake mzuri akifunga bao pekee la ushindi kwenye mechi dhidi ya watani, Simba SC Machi 8 Uwanja wa Taifa, sasa Mkapa ikaripotiwa ameongezwa mkataba wa miaka miwili.
    Siku chache baadaye Morrison akaibuka akidai Simba wanamshawishi kujiunga nao kwa ofa nzuri zaidi na Yanga SC ikawasilisha malalamiko TFF dhidi ya mahasimu wao kukiuka taratibu za usajili. 
    Morrison akagoma kusafiri na Yanga SC Kanda ya Ziwa kabla ya kuibuka kwa taarifa anataka kuondoka kufuata ofa nzuri Uarabuni katika klabu ambayo hata hivyo hakuitaja.
    Tangu hapo mahusiano ya Yanga na mchezaji huyo yakazidi kuwa mabovu kiasi cha kuripotiwa hadi kumshikia kisu Meneja wa klabu, Abeid Mziba kambini, ingawa aliendelea kuitumikia klabu.  
    Morrison akafungua kesi TFF kupinga mkataba wa hadi 2022 akida yeye ana mkataba wa miezi sita tu ambao umemalizika Julai. TFF ilimuamuru Morrison kurejea kazini Yanga wakati shauri lake linaendelea kusikilizwa.
    Julai 12, mwaka huu Morrison akaondoka moja kwa moja baada ya kufanyiwa mabadiliko katika mchezo dhidi ya Simba SC Uwanja wa Taifa nafasi yake ikichukuliwa na Mnyarwanda Patrick Sibomana dakika ya 64 katika mchezo wa Nusu Fainali Kombe la TFF, maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC). 
    Tangu siku hiyo, Yanga ikachapwa mabao 4-1 Mghana huyo akicheza chini ya kiwango – hajaonekana tena kwenye kambi ya timu hiyo iliyomaliza Ligi Kuu katika nafasi ya pili nyuma ya mahasimu wao hao wa jadi, Smba SC.
    Morrison mwenye umri wa miaka 27, awali aliibukia klabu ya Heart of Lions mwaka 2013, kabla ya kuhamia Ashanti Gold mwaka 2015, zote za kwao Ghana.
    Mwaka 2016 alijiunga na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambako alidumu hadi 2018 alipohamia Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
    Mwaka 2019, Morrison aliyezaliwa mjini Mankessim, Ghana alirejea DRC kujiunga na DC Motema Pembe ambako alicheza kwa nusu msimu na kurejea kwao Ghana kabla ya kusajilwa Yanga SC Januari mwaka huu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA YAMTAMBULISHA RASMI MORISSON, YANGA SC WASEMA WATACHUKUA HATUA ZA MFANO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top