• HABARI MPYA

    Thursday, June 04, 2020

    YANGA SC KUMENYANA NA KMC KATIKA MCHEZO WA KIRAFIKI JUMAPILI KUJIANDAA KUIVAA MWADUI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KATIKA kujiandaa na mchezo wake wa kiporo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Mwadui FC Juni 13 Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga – Yanga SC itakuwa na mchezo wa kirafiki dhidi ya KMC Jumapili Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
    Yanga inataka kuutumia mchezo huo kujua hali halisi ya kikosi chake kabla ya kumenyana na Mwadui FC huko Shinyanga wiki ijayo na baadaye JKT Tanzania Dar es Salaam.
    Wiki iliyopita Bodi ya Ligi ilitoa ratiba ya mechi za viporo za Ligi na siku moja baada ya Yanga kumenyana na Mwadui, mabingwa watetezi, Simba SC watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting Juni 14 Uwanja wa Taifa.


    Mechi nyingine ya Juni 13 ni kati ya Coastal Union na Namungo FC Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga, wakati Juni 14, Azam FC nao watakuwa wenyeji wa Mbao FC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na Juni 17, Yanga SC watakuwa wageni wa JKT Tanzania Uwanja wa Taifa.
    Baada ya kukamilisha mechi hizo za viporo, rasmi Ligi Kuu itaanza Juni 20 na kufikia tamati Julai 26, mwaka huu baada ya kusimama tangu Machi 17, mwaka huu kwa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa maambukizi ya virusi vya corona duniani kote.  
    Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa pointi zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.
    Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.
    Wakati huo huo Yanga leo imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Transit Camp kwenye mchezo wa kirafiki Uwanja wa Chuo cha Sheria, Oysterbay Jijini Dar es Salaam, mabao yake yakifungwa na Feisal Salum kwa penalti, Bernard Morrison na mtokea benchi Mrisho Ngassa.
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Farouk Shikalo, Paul Godfrey/Juma Abdul, Jaffar Mohammed, Kelvin Yondan, Lamine Moro, Said Juma 'Makapu', Haruna Niyonzima/Deus Kaseke, Feisal Salum 'Fei Toto'/Abdulaziz Makame, Ditram Nchimbi/David Molinga, Bernard Morrison/Yikpe Gislain na Mapinduzi Balama/Mrisho Ngassa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC KUMENYANA NA KMC KATIKA MCHEZO WA KIRAFIKI JUMAPILI KUJIANDAA KUIVAA MWADUI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top