• HABARI MPYA

    Tuesday, November 05, 2019

    AVEVA NA KABURU WAACHIWA BAADA YA KUTIMIZA MASHARTI YA DHAMANA MAHAKAMANI LEO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu mjini Dar es Salaam leo imewaachia kwa dhamana aliyekuwa rais wa klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ baada ya kutimiza masharti ya dhamana.
    Wawili hao walitakiwa kuwa na wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh milioni 30  kila mmoja pamoja na kuwa na vitambulisho vya taifa.
    Majira ya saa  sita mchana, Kaburu pamoja na wadhamini wake walisaini fomu ya mahakama na kuachiwa huru huku Aveva akiwa anapatiwa huduma ya kwanza baada ya hali yake kiafya kuonekana kutokuwa nzuri.
    Kaburu aliondoka mahakamani hapo akiwa ndani ya gari ndogo aina ya subaru yenye namba ya usajili T854 DGB.
    Aveva na Kaburu wameachiwa kwa dhamana baada ya vuta nikuvute vute kati ya upande wa mashitaka na utetezi kuhusu dhamana ya washitakiwa hao, lakini Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ametupilia mbali mapingamizi ya upande wa mashitaka ya kupinga dhamana baada ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi kesi hiyo isiendelee hadi Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi.

    Akisoma uamuzi huo, Hakimu Simba amesema kukata rufaa kwa upande wa mashitaka hakuondoi maamuzi ya mahakama na kwamba rufaa waliyokata itakaposikilizwa na kutolewa maamuzi ndio inaweza kufuta maamuzi ya mahakama ya chini.
    Ameongeza kuwa,  kitendo cha serikali kukata rufaa kupitia mawakili wake hakuzuii washitakiwa kupewa dhamana hivyo maombi yao yanatupiliwa mbali.
    Baada ya kutoa maamuzi hayo, Wakili wa Serikali Mkuu, Shadrack Kimaro akisaidiana na Pendo Temu alidai kuwa anaomba kujitoa katika kesi hiyo.
    Hata hivyo, Hakimu Simba aliwaeleza kuwa anaandika kwenye kumbukumbu za mahakama kwamba wamejitoa wenyewe na kuongeza kuwa sio kila wanachotaka upande wa mashitaka ni lazima kiwe hivyo na kuonya wasibishane na mahakama.
    Baada ya kueleza hayo, mawakili hao wa serikali walisimama na kutoka nje ya chumba cha mahakama kwa hasira na Hakimu Simba aliwataka washitakiwa hao kuwa na wadhamini wawili na wasaini bondi ya Sh milioni 30. Kesi hiyo imahirishwa hadi Novemba 12, mwaka huu kwa ajili ya utetezi.
    Mbali na washitakiwa hao, wengine ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hansppope wamekutwa na kesi ya kujibu katika mashitaka saba na kuondolewa mashitaka mawili ya utakatishaji fedha.
    Katika mashitaka ya kwanza,  Aveva na Kaburu wanadaiwa kula njama ya kutenda kosa la matumizi mabaya ya madaraka.
    Inadaiwa Aveva na Kaburu wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kuandaa fomu ya kuhamisha fedha Dola za Marekani 300,000 kutoka kwenye akaunti ya Simba iliyoko benki ya CRDB Azikiwe kwenda kwenye akaunti binafsi ya Aveva iliyoko benki ya Barclays.
    Aveva na Kaburu pia kwa pamoja wanadaiwa kughushi nyaraka iliyokuwa ikionyesha Simba inalipa mkopo wa Dola za Marekani 300,000 kwa Aveva kitu ambacho sio kweli.
    Aveva anadaiwa katika benki ya CRDB anadaiwa kutoa nyaraka ya uongo ikionesha Simba wanalipa mkopo wa Dola za Marekani 300,000
    Aveva anadaiwa kuwa katika Benki ya Baclays Mikocheni alijipatia Dola za Marekani 187,817 wakati akijua zimetokana na kughushi.
    Kaburu anadaiwa kumsaidia Aveva kujipatia Dola za Marekani 187,817 kutoka kwenye akaunti ya Simba wakiwa wanajua fedha hizo zimetokana na zao la kughushi. 
    Aveva, Kaburu na Hans Poppe wanadaiwa kughushi hati ya malipo ya kibiashara wakionesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zina thamani ya Dola za Marekani 40,577 huku wakijua kwamba siyo kweli
    Katika mashitaka ya nane, Aveva anadaiwa kuwasilisha hati ya malipo ya kibiashara ya uongo  kwa Levison Kasulwa  kwa madhumuni ya kuonesha kwamba Simba wamenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Marekani 40,577
    Aveva, Kaburu na Hanspope wanadaiwa kuwasilisha nyaraka za uongo kuonesha kuwa Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Marekani 40,577.
    Aveva na Kaburu walioingia madarakani Juni 30, mwaka 2014, hawakufanikiwa kumalizia muda wao wa uongozi Simba SC kufuatia kuwekwa rumande katika gereza la Keko tangu Juni 29, mwaka 2017 kwa tuhuma za kesi inayowakabili sasa mahakamani.
    Julai 1, mwaka huo, viongozi waliobaki katika Kamati ya Utendaji, Wajumbe Iddi Kajuna, Said Tully, Collins Frisch, Ally Suru na Jasmine Badour waliteua watu wa kukaimu nafasi za Aveva na Kaburu.
    Hao ni Mjumbe ni Mteule wa Kamati ya Utendaji, Salum Abdallah ‘Try Again’ aliyeteuliwa Kukaimu Urais na Kajuna Umakamu ambao walifanikiwa kuitisha uchaguzi mwingine Novemba 5, mwaka 2018 uliofanyika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere mjini Dar es Salaam, Swedi Nkwabi akishinda Uenyekiti.

    Hata hivyo, Septemba 14, mwaka huu Mkwabi ameamua kujiuzulu wadhifa huo miezi 10 na ushei tu tangu achaguliwe akisema sababu ya kuchukua uamuzi huo ni kwamba mambo si shwari ndani ya klabu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AVEVA NA KABURU WAACHIWA BAADA YA KUTIMIZA MASHARTI YA DHAMANA MAHAKAMANI LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top