• HABARI MPYA

    Friday, October 11, 2019

    MCHEZAJI WA KAGERA SUGAR ALIYEMPIGA MATEKE AJIBU MECHI NA SIMBA BUKOBA APEWA ONYO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BEKI wa Kagera Sugar ya Bukoba, Zawadi Mauya amepewa onyo kwa kitendo chake cha kumpiga mateke kiungo wa Simba SC, Ibrahim Ajibu kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara baina ya timu hizo Septemba 26, mwaka huu Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. 
    Hatua hiyo imechukuliwa katika kikao cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kilichofanyika Oktoba 7, mwaka huu kupitia mwenendo na matukio mbalimbali ya ligi hiyo.
    Katika mechi hiyo namba 40 ambako Simba SC iliibuka na ushindi wa 2-0, Mauya alionekana kumpiga mateke Ajibu akijaribu kumdhoofisha ili ampokonye mpira na TPLB imesema adhabu dhidi yake ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
    Naye Mwamuzi wa mchezo huo Emmanuel Mwandembwa amepewa Onyo kwa kumuonesha Mauya kadi ya njano badala ya nyekundu kwa kitendo chake ambacho kilikuwa cha makusudi na kujirudia.
    Mechi namba 19: Coastal Union 2 v KMC 0- Klabu ya KMC imetozwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na timu yake kutoingia vyumbani wakati wa mapumziko katika mechi hiyo iliyochezwa Septemba 13, 2019 katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. 
    Hatua hiyo imechukuliwa katika kikao cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kilichofanyika Oktoba 7, mwaka huu kupitia mwenendo na matukio mbalimbali ya ligi hiyo.
    Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
    Mechi namba 24: Alliance FC 1 v Biashara United 1- Klabu ya Alliance imetozwa faini ya jumla ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na vurugu za washabiki wake pamoja na kufanya vitendo vinavyoashiria imani za ushirikina katika mechi hiyo iliyofanyika Septemba 20, 2019 Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
    Nayo klabu ya Biashara United imetozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kufanya vitendo vinavyoashiria imani ya ushirikiana wakati ikiingia uwanjani. Adhabu zote ni kwa mujibu wa Kanuni ya 43(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
    Mechi namba 41: Singida United 0 v Alliance FC 2- Klabu ya Alliance imetozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kumweka kwenye benchi la ufundi Meneja ambaye hakutambulishwa katika kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) wakati wa mechi hiyo iliyofanyika Septemba 28, 2019 Uwanja wa Namfua mjini Singida. 
    Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
    Mechi namba 44: Lipuli FC 2 v Tanzania Prisons 2- Klabu ya Tanzania Prisons imetozwa faini ya sh. 3,000,000 (milioni tatu) kutokana na basi lililobeba wachezaji wa timu hiyo kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi katika mechi hiyo iliyofanyika Septemba 29, 2019 Uwanja wa Samora mjini Iringa. Adhabu imezingatia Kanuni ya 14(49) kuhusu Taratibu za Mchezo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MCHEZAJI WA KAGERA SUGAR ALIYEMPIGA MATEKE AJIBU MECHI NA SIMBA BUKOBA APEWA ONYO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top