• HABARI MPYA

    Friday, October 04, 2019

    MCHEZAJI NA KOCHA BORA WA LIGI KUU SEPTEMBA WOTE SIMBA SC, NI MADENGE NA AUSSEMS

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa Simba ya Dar es Salaam, Miraji Athumani ‘Madenge’ amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Septemba wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2019/20, huku Patrick Aussems pia wa Simba akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.
    Miraji na Aussems walitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzao walioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo ya VPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na mapendekezo kutoka kwa makocha waliopo viwanja mbalimbali, ambavyo ligi hiyo inachezwa msimu huu. 
    Hiyo inakuwa mara ya pili mfululizo Simba SC kutoa Mchezaji Bora wa Mwezi, baada ya Mnyarwanda mzaliwa wa Uganda, Meddie Kagere kuwa Mchezaji Bora wa Agosti.  
    Miraji Athumani ‘Madenge’ wa Simba SC ndiye Mchezaji Bora wa Lgi Kuu kwa mwezi Septemba

    Kwa mwezi huo wa Septemba, Simba ilicheza michezo mitatu na kushinda yote ikiifunga Mtibwa Sugar mabao 2-1, Kagera Sugar mabao 3-0 na Biashara United mabao 2-0, ambapo Miraji alikuwa na kiwango kizuri uwanjani kwa mwezi huo akichangia kwa asilimia kubwa mafanikio hayo ya Simba ikiwa ni pamoja na kufunga mabao mawili na kutoa pasi za mabao mawili. 
    Miraji anayefahamika pia kwa jina la utani Shevchenko au Sheva, aliwashinda Kagere aliyetoa mchango mkubwa pia katika mafanikio ya Simba ikiwa ni pamoja na kufunga mabao manne. 
    Mchezaji mwingine aliyeingia fainali alikuwa Ismail Kada wa Prisons aliyeonesha kiwango kizuri na kutoa mchango katika michezo ambayo Prisons  ilicheza ikishinda miwili, sare mmoja, ambapo iliifunga Ruvu Shooting mabao 2-1, Mtibwa Sugar mabao 3-1 na kutoka sare na Lipuli mabao 2-2.
    Kwa kutwaa tuzo hiyo, Miraji atazawadiwa kikombe na Tsh. 1,000,000 (milioni moja) kutoka Vodacom. Vilevile atapata Kisimbusi  kutoka Azam TV.
    Kwa upande wa Aussems aliwashinda Mohammed Rishard wa Prisons na Abdallah Mohammed ‘Baresi’ wa JKT Tanzania, ambapo Aussems aliongoza timu yake kupata ushindi katika michezo mitatu, kati ya hiyo mmoja nyumbani dhidi ya Mtibwa Sugar na miwili ugenini mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar na mabao 2-0 dhidi ya Biashara United. Simba imemaliza mwezi ikiwa nafasi ya kwanza. 
    Rishard aliingia hatua ya fainali baada ya kuiongoza Prisons kushinda michezo miwili na kutoa sare mmoja, ambapo ilishinda nyumbani mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting, kisha ikashinda ugenini mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa na ikatoka sare ugenini na Lipuli ya mabao 2-2, wakati Baresi aliingoza JKT Tanzania kushinda michezo miwili, sare moja na kupoteza mmoja.
    JKT Tanzania ilifungwa ugenini bao 1-0 na Lipuli,  ikatoka 0-0 nyumbani na Mtibwa Sugar,  ikashinda bao 1-0 ugenini dhidi ya Biashara United na pia ikapata ushindi ugenini kama huo dhidi ya Kagera Sugar. Mwezi uliopita, Kocha Bora wa Ligi Kuu alikuwa ni Salum Mayanga wa Ruvu Shooting.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MCHEZAJI NA KOCHA BORA WA LIGI KUU SEPTEMBA WOTE SIMBA SC, NI MADENGE NA AUSSEMS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top