• HABARI MPYA

  Friday, October 04, 2019

  SAMATTA ANAFAA KUWA MCHEZAJI BORA WA MUDA WOTE TANZANIA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  “Mbwana Amekuwa juu ya kiwango kuliko sisi, kwa sababu anacheza katika wakati wa hivi sasa na ni mchezaji ambaye nafikiri anaitia Tanzania katika nuru ya mpira,”.
  Hayo ni maneno ya Mtanzania wa kwanza kucheza soka ya kulipwa Ulaya, Sunday Manara akimzungumzia Nahodha wa timu ya taifa, Mbwana Ally Samatta.
  Sunday Manara ambaye alifungua milango ya Watanzania kucheza Ulaya baada ya kusajiliwa na klabu ya Heracles ya Uholanzi mwaka 1978 na kudumu hadi 1980, alisema hayo katika mahojiano na mwandishi wa makala haya kwenye kipindi cha Sports Am, ambacho hurushwa hewani kila Jumamosi na Jumapili kupitia chaneli ya Azam Sports 2.

  Mbwana Samatta ndiye mchezaji anayeiweka Tanzania katika nuru ya soka kwa sasa

  Samatta ndiye lulu ya Tanzania katika soka kwa sasa akiwa anachezea klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji ambako tayari amekwishaanza kupewa Unahodha wa timu. 
  Baada ya kufanya vizuri barani Afrika ikiwemo kushinda mataji ya Ligi za nchi mbili, Tanzania akiwa na Simba SC na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akiwa na TP Mazembe aliyoiwezesha pia kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika 2015, Mbwana akahamishia cheche zake Ulaya.  
  Na hiyo ni baada ya kucheza Klabu Bingwa ya Dunia ya FIFA nchini Japan mwaka 2015 na kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika baada ya kuwa mfungaji bora wa Lig ya Mabingwa barani humo mwaka huo.
  Msimu uliopita Samatta pamoja na kucheza Kombe la UEFA akiwa Mtanzania wa pili kucheza michuano ya Ulaya baada ya Kassim Manara aliyecheza Kombe la Washindi akiwa na Austria Klagenfurt, pia aliiwezesha KRC Genk kutwaa mataji mawili Ubelgiji, ubingwa wa Ligi na Super Cup.
  Na ndiyo msimu ambao naye alikaribia kuwa mfungaji bora wa Ligi ya Ubelgiji baada ya kumaliza nafas ya pili hivyo kushinda tuzo ya Kiatu cha Ebony, yaani Mchezaji Bora wa Afrika katika Ligi ya Ubelgiji.
  Na msimu huu, Samatta ameweka rekodi mpya kabisa, kuwa Mtanzania wa kwanza siyo tu kucheza bali na kufunga bao katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
  Chini ya Unahodha wa Samatta, Genk iliokota pointi yake ya kwanza juzi kwenye Ligi ya Mabingwa baada sare ya 0-0 na Napoli nyumbani kufuatia kufungwa 6-2 na Salzburg nchini Austria katika mchezo wa kwanza wa Kundi E.

  Mbwana Samatta wakati anashinda tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika

  Samatta mwenye umri wa miaka 26 alicheza mechi zote hizo mwanzo hadi mwosho na pia alifungua akaunti yake ya mabao kwenye michuano hiyo kwa kufunga bao 1-0 wakipigwa 6-2 na Salzburg.
  Kwa ujumla, Samatta amecheza mechi 166 kwenye mashindano yote tangu ajiunge na KRC Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akiwa amefunga mabao 68 jumla.
  Katika ligi ya Ubelgiji pekee amecheza mechi 130 na kufunga mabao 52, kwenye Kombe la Ubelgiji amecheza mechi tisa na kufunga mabao mawili, katika Super Cup mechi moja na Europa League mechi 24 na mabao 14. 
  Pamoja na kuiwezesha Tanzania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Juni mwaka huu nchini Misri, ikiwa mara ya pili tu kihistoria tangu mwaka 1980 – Mbwana Ally Samatta anastahili kupewa heshima ya Mchezaji Bora wa Muda wote Tanzania.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAMATTA ANAFAA KUWA MCHEZAJI BORA WA MUDA WOTE TANZANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top