• HABARI MPYA

  Friday, September 06, 2019

  YANGA WAISHITAKI BODI YA LIGI SERIKALINI KWA KUMFUNGIA ZAHERA KWA KOSA LA KUVAA PENSI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  UONGOZI wa Yanga SC umepeleka malalamiko kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ukipinga uamuzi wa Bodi ya Ligi kumfungia kocha Mwinyi Zahera mechi tatu kutokana na shutuma za upendeleo alizotoa kwa Bodi hiyo baada ya mchezo kati ya Yanga dhidi ya Ruvu Shooting
  Katika mchezo huo wa kwanza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu, kocha Zahera alilalamikia hatua ya Bodi ya Ligi kukataa kusogeza mbele kwa siku mbili mechi dhidi ya Ruvu Shooting hasa ikizingatiwa Yanga ilipaswa kusafiri kutoka Botswana
  “Yanga tulicheza Botswana Agosti 24 na tukasafiri kurejea nchini usiku wa kuamkia Agosti 26, wachezaji walipumzika siku moja tu kabla ya kushuka tena dimbani,” amesema Makamu Mwenyekiti wa Yanga SC, Mwakalebela.

  Mwakalebela ambaye ni Katibu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ameongeza kwamba kwa kosa analodaiwa kufanya Zahera adhabu ya kumfungia kocha mechi tatu ni kubwa, pengine faini ingetosha na kwa sababu hiyo wamekwishaiandikia barua Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo kulalamikia adhabu hizo.
  “Pamoja na adhabu hiyo, Kocha wetu alipigwa faini ya kulipa laki tano kutokana na mavazi aliyovaa kwenye mchezo huo.  Hata hivyo wengi tumeshangazwa na uamuzi huo kwani pamoja na adhabu kumkumba yeye, kocha msaidizi wa Ruvu Shooting naye hakuwa na mavazi rasmi lakini hakuadhibiwa,”alisema.
  Mwakalebela amesema hawaoni kama Bodi ya ligi imemtendea haki Zahera kwa kumfungia kocha mechi tatu, wakati wangeweza kumpiga faini tu aendelee kufundisha timu. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA WAISHITAKI BODI YA LIGI SERIKALINI KWA KUMFUNGIA ZAHERA KWA KOSA LA KUVAA PENSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top