• HABARI MPYA

    Sunday, July 07, 2019

    MWAKYEMBE: NINA IMANI NA KOCHA AMUNIKE KUENDELEA KUFANYA VIZURI NA TAIFA STARS

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Dk. Harrison George Mwakyembe amesema kwamba ana imani kubwa na kocha wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mnigeria Emmanuel Amunike kuendelea kufanya vizuri na timu hiyo.
    Akizungumza na waandishi wa Habari jana baada ya kukutana na kw mazungumzo na Amunike katika hotel ya Protea Courtyard mjini Dar es Salaam, Mwakyembe amesema kwamba kinachohitajika ni swala la muda tu, kwani Mnigeria huyo amemueleza mipango mikubwa ya kiufundi aliyonayo kwa Taifa Stars ili iweze kufanya vizuri katika mashindano yajayo.

    Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Dk. Harrison Mwakyembe (kulia) akizungumza pembeni ya kocha wa Taifa Stars, Mnigeria Emmanuel Amunike jana

    Mwakyembe amsema kwamba Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2019 zinazoendelea nchini Misri zimebeba uzito wa kipekee kwa nchi ya Tanzania baada ya kukaa nje kwa miaka 39 na kufuzu kushiriki katika mashindano hayo ambayo Taifa Stars imetupwa nje baada ya kufungwa mechi zote tatu za Kundi C dhidi ya Senegal, Algeria na Kenya.
    “Ndugu waandishi wa Habari kwanza kabisa niseme tu kwamba, nimefurahi sana kukutana na kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania, ambapo lengo la kukutana naye ni kunieleza kilichotokea kule nchini Misri katika mashindano ya Afcon ambayo tumeshiriki baada ya miaka 39 kupita, mashindano haya yamebeba uzito wa kipekee kwa nchi yetu, na niseme tu kwamba nina imani kubwa sana na kocha Amunike kuendelea kufanya vizuri na timu yetu, nimeongea naye mambo mengi sana kuhusu mashindano, na tumeona kama Wizara tumpe muda zaidi kwa mipango mizuri ya kiufundi aliyonayo kwa Timu ya Taifa hili iweze kufanya vizuri katika mashindano yajayo,”.
    “Mimi nimefurahi sana kukaa na mwalimu, na yeye pia amefurahi kukaa na Serikali, ili tujuwe mwenzetu maoni yake ni nini kuhusu timu ya Taifa, tufanyaje kujipanga hili kesho, kesho kutwa turejee tena Afcon lakini safari hii tukirejea kila mtu awe na wasiwasi kuwa hii sio timu nzuri kukutana nayo, ametupa mfano mzuri sana, kwamba Uganda mwaka 2015 iliposhiriki mara mwisho haikufanya vizuri hata kidogo, lakini wenzetu wakarudi wakaanza kuyafanyia kazi mapungufu katika mchezo wao, badala ya kukaa mwaka mzima mnalumbana na kunyoosheana vidole, mapungufu kwenye timu ya kiufundi na sisi kwa upande wetu yamejitokeza sana, mengi sitayasema kwa sababu ni mambo ambayo tutakaa na vyombo vinavyohusika, lakini cha msingi tunafurahi sana mwalimu ana moyo chanya kwamba tunaweza, tumeonyesha watanzania kwamba tunaweza, lakini kiufundi inatakiwa na sisi tujiongeze,” alisema Mheshimiwa Mwakyembe.
    Aidha Mheshimiwa Mwakyembe amesema Kocha Amunike amependekeza mazoezi zaidi kwa wachezaji wa Timu ya Taifa pamoja na kucheza mechi za kirafiki kimataifa mara Tatu kwa Mwaka hili kuweza kupata uzoefu zaidi katika mashindano ya kimataifa.
    “Tatizo lililojitokeza ambalo mwalimu anadhani linaweza kutatuliwa ni mazoezi kwa timu ya Taifa, kwamba angalau mara tatu timu ya Taifa kila mwaka ikawa na mechi za kirafiki, wanaitwa leo wanacheza na Zambia , na Afrika Kusini, tumewakaribisha pengine Spain wanakuja na kuangalia mbuga za wanyama, tunajenga imani ya wachezaji wetu, kwenye mashindano haya yaliyopita tumeona kuna wakati wachezaji wetu walikosa kujiamini, unaona mchezo kadri unavyoendelea ndio sasa hata pasi za uwakika ndio zinapigwa, kwa hiyo ni kujiamini lakini vijana wa Tanzania walicheza vizuri sanaa,” alisema Mwakyembe.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWAKYEMBE: NINA IMANI NA KOCHA AMUNIKE KUENDELEA KUFANYA VIZURI NA TAIFA STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top