• HABARI MPYA

  Sunday, July 07, 2019

  KAGERA SUGAR YAENDELEA KUJISUKA UPYA, YASAJILI KIUNGO MKABAJI KUTOKA BURUNDI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIUNGO mkabaji Moussa Hadji Mosi amejiunga na Kagera Sugar ya Bukoba kutoka Leslierres ya Ligi Kuu ya kwao, Burundi. 
  Mosi anakuwa mchezaji wa kwanza mpya wa kigeni kusajiliwa na Kagera Sugar na wa tisa jumla katika dirisha hili kusaini timu hiyo inayomilikiwa na kiwanda cha sukari.
  Wengine ni Yussuph Mhilu kutoka Yanga SC aliyecheza kwa mkopo Ndanda FC msimu uliopita, Zawadi Mauya kutoka Lipuli FC, Ally Shomari kutoka Mtibwa Sugar, Abdallah Seseme kutoka Mwadui FC,  Awesu Ally Awesu kutoka Singida United, Erick Kyaruzi, Frank Ikobela, wote kutoka Mbeya City ya Mbeya na  Evarist Mjwahuki kutoka Mbao FC ya Mwanza.

  Kiungo mkabaji, Moussa Hadji Mosi (kulia) amejiunga na Kagera Sugar kutoka Leslierres ya Burundi 

  Kagera Sugar imepania kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao baada ya kunusurika kushuka Daraja msimu uliopita.
  Ikumbukwe Kagera Sugar na Mwadui FC zilinusurika kushuka daraja baada ya kubaki Ligi Kuu ya Tanzania Bara kupitia mechi zao Play-Off dhidi ya Pamba SC na Geita Gold Mine za Daraja la Kwanza. 
  Mabao ya Ally Ramadhani dakika ya 51 na Japhet Makalayi dakika ya 59 yaliipa Kagera Sugar ushindi wa 2-0 dhidi ya Pamba SC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba Juni 9 baada ya timu hizo kutoka sare ya kwenye mchezo wa kwanza Juni 3 Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza.
  Na hiyo ni baada ya Kagera Sugar kumaliza nafasi ya 18 katika Ligi Kuu, nyuma ya Mwadui FC iliyomaliza nafasi ya 17 ambayo iliitoa Geita Gold katika mechi ya mchujo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAGERA SUGAR YAENDELEA KUJISUKA UPYA, YASAJILI KIUNGO MKABAJI KUTOKA BURUNDI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top