• HABARI MPYA

    Saturday, July 06, 2019

    BEKI MGHANA, DANIEL AMOAH AONGEZA MKATABA WA MIAKA MITATU AZAM FC HADI 2022

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BEKI kisiki Mghana, Daniel Amoah ameongeza mkataba mpya wa miaka mitatu kuendelea kuitumikia Azam FC.
    Mkataba huo mpya utamfanya Amoah, kuendelea kusalia ndani ya viunga vya Azam Complex hadi mwaka 2022.
    Amoah aliyejiunga na Azam FC miaka mitatu iliyopita kutoka Medeama SC ya kwao, Ghana anaungana na Mghana mwenzake, Yakubu Mohammed kuongeza mkataba katika klabu hiyo.
    Maana yake msimu ujao Azam FC itakuwa na wachezaji watatu tu kutoka Ghana, mwingine ni kipa Razack Abalora baada ya kuachwa kiungo mshambuliaji, Enock-Atta Agyei aliyesajiliwa pamoja na Amoah kutoka Medeama mwaka 2017.
    Kwa sasa kikosi cha Azam FC kipo mjini Kigali nchini Rwanda kwa ajili ya kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la kagame iliyoanza leo.

    Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat' akibadilishana mikataba na Daniel Amoah baada ya kusaini 

    Mabingwa hao watetezi wa michuano hiyo, Azam FC wamepangwa Kundi B pamoja na wenyeji, Mukura Victory, KCCA ya Uganda na Bandari ya Kenya.
    Kundi A linaundwa na wenyeji, Rayon Sports, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Atlabara ya Sudan Kusini na KMC ya Dar es Salaam.
    Kundi C linaundwa na wenyeji wengine, APR, Green Eagles ya Zambia, Proline ya Uganda na Heegan ya Somalia wakati Kundi D kuna DC Motema Pembe ya DRC, Gor Mahia ya Kenya, Port ya Djibouti na KMKM ya Zanzibar. 
    Azam FC wanawania kutwaa taji la tatu mfululizo la Kombe la Kagame katika michuano ya mwaka huu, baada ya awali kulichukua mara mbili mfululizo nyumbani, Tanzania.
    Mwaka 2015 walibeba taji hilo kwa mara ya kwanza baada ya kuifunga Gor Mahia ya Kenya 2-0 katika fainali Agosti 2 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, mabao ya John Bocco dakika ya 17 na Kipre Herman Tchetche dakika ya 64.
    Wakatetea taji hilo Julai 13 mwaka jana Dar es Salaam baada ya kuifunga Simba SC 2-1, mabao yake yakifungwa na mshambuliaji Shaaban Iddi Chilunda dakika ya 33 na beki Aggrey Moris dakika ya 69, huku la Wekundu wa Msimbazi likifungwa na Kagere Meddie dakika ya 63.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BEKI MGHANA, DANIEL AMOAH AONGEZA MKATABA WA MIAKA MITATU AZAM FC HADI 2022 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top