• HABARI MPYA

  Sunday, July 07, 2019

  AZAM FC YAANZA VYEMA KAGAME, YAWAPIGA WENYEJI 1-0, RAYON YAILAZA 1-0 TP MAZEMBE

  Na Mwandishi Wetu, KIGALI
  MABINGWA watetezi, Azam FC wameanza vyema baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Mukura Victory katika mchezo wa Kundi B Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame Uwanja wa Huye mjini Butare.
  Asante kwa bao la kujifunga la Muniru Abdulrahman dakika ya 78 baada ya kazi nzuri ya mshambuliaji mpya, Iddi Suleiman ‘Nado’ aliyesajiliwa msimu huu kutoka Mbeya City ya nyumbani, Tanzania. 
  Mchezo mwingine wa kundi hilo, Bandari FC ililazimishwa sare ya 1-1 na KCCA ya Uganda Uwanja wa Huye. Abdallah Hassan alianza kuifungia Bandari dakika ya pili kabla ya Sadam Juma kuisawazishia KCCA dakika ya 61.
  Wachezaji wa Azam FC wakipongezana baada ya kupata bao lao pekee leo na chini ni kikosi kilichoanza  
   
  Wawakilishi wengine wa Tanzania, KMC wamelazimishwa sare ya 1-1 na Atlabara ya Sudan Kusini katika mchezo wa Kundi A Uwanja wa Nyamirambo mjini Kigali.
  Salim Aiyee alianza kuifungia KMC dakika ya 46 kabla ya Peter Sunday kuisawazishia Atlabara dakika ya 67.  Mchezo mwingine wa Kundi A, Rayon Sport iliichapa TP Mazembe 1-0, bao pekee la Jules Ulimwengu dakika ya nne Uwanja wa Nyamirambo.
  Michuano hiyo itaendelea kesho kwa mechi za Kundi C, Proline ya Uganda ikimenyana na Heegan ya Somalia Saa 8:00 mchana na Green Eagles ya Zambia dhidi ya wenyeji, APR Saa 10:00 jioni Uwanja wa Nyamirambo.
  Kutakuwa na mechi za Kundi D pia Uwanja wa Huye, KMKM ya Zanzibar na Port ya Djibouti Saa 8:00 mchana na Gor Mahia ya Kenya dhidi ya Manyema Union ya DRC Saa 10:00 jioni Uwanja wa Umuganda mjini Gisenyi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC YAANZA VYEMA KAGAME, YAWAPIGA WENYEJI 1-0, RAYON YAILAZA 1-0 TP MAZEMBE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top