• HABARI MPYA

  Tuesday, June 04, 2019

  YANGA SC YAREJESHWA MICHUANO YA AFRIKA, KUCHEZA LIGI YA MABINGWA MSIMU UJAO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limethibitisha Tanzania kuingiza na timu nne katika mashindano ya klabu barani kwa msimu wa 2019/2020.
  Taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) leo imesema kwamba timu mbili zitashiriki katika Ligi ya Mabingwa na nyingine mbili zitashiriki Kombe la Shirikisho.
  Nafasi hiyo kwa Tanzania imekuja baada ya kuwa katika nafasi 12 bora kwenye viwango vya ubora vya CAF.
  Kwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu zilizofanyiwa marekebisho na Kamati ya Utendaji baada ya kupatikana nafasi nne (4) timu za Tanzania zitakazowakilisha kwenye mashindano hayo ni Simba na Young Africans, maarufu Yanga Ligi ya Mabingwa (CAF CL),Azam FC na KMC Kombe la Shirikisho (CAF CC).

  KMC atawakilisha Kombe la Shirikisho kwa mujibu wa Kanuni hiyo ambayo inatamka kama timu iliyomaliza nafasi ya 3 itakua ndio bingwa wa Kombe la FA basi mshindi wa 4 anapata nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho kwasababu bingwa wa FA anaiwakilisha nchi kwenye mashindano hayo.
  Tayari CAF imefungua dirisha kwa Mashirikisho kusajili timu kupitia mtandao wa CMS.
  Mwisho wa usajili ni Juni 30,2019 ambapo TFF inatakiwa iwe imesajili timu zitakazoshiriki kwenye mashindano ya Kimataifa msimu wa 2019/2020.
  Rais wa TFF Wallace Karia amezitaka klabu zilizopat nafasi kusajili kwa umakini na kujiandaa kwa Mashindano ya CAF ili kutopoteza nafasi ya kuingiza timu nne katika mashindano ya CAF.
  Wakati huo huo: Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limeialika klabu ya Yanga kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame Julai mwaka huu nchini Rwanda.
  Maana yake, Tanzania itakuwa na timu tatu kwenye michuano hiyo, Azam FC kama mabingwa watetezi, Simba bingwa wa nchi na Yanga waalikwa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YAREJESHWA MICHUANO YA AFRIKA, KUCHEZA LIGI YA MABINGWA MSIMU UJAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top