• HABARI MPYA

  Monday, June 03, 2019

  SAMATTA APEWA MTAA KATIKA MOJA YA BARABARA KUBWA ZA MANISPAA YA TEMEKE

  Na Asha Said, DAR ES SALAAM
  MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameagiza moja ya mitaa ya Manispaa ya Temeke ipewe jina la Nahodha wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Mbwana Ally Samatta.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake mjini Dar es Salaam leo, Makonda amesemna kwamba uamuzi huo umetokana na na heshima kubwa ambayo taifa inaipata kutoka kwa mshambuliaji huyo wa klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji.
  “Kutokana na heshima kubwa tunayoipata kupitia kwa mchezaji Mbwana Samatta, tumeamua kuita moja ya Barabara za Wilaya ya Temeke jina la mchezaji huyo wa Genk,” amesema Makonda ambaye jana alikuwa mgeni rasmi katika mechi ya hisani aliyoindaa Samatta Uwanja wa taifa kwa kushirikiana na mwanamuziki Ally Kiba.

  Makonda alisema katika hafla ya kuutambulihsa mmoja wa mitaa ya Temeke kwa jina la Samatta kutakuwa na viongozi mbalimbali pamoja na wachezaji wenzake wa Taifa Stars na wengineo atakaowaalika.
  “Mchango wa Samatta katika Taifa hili kila mtu anautambua, hivyo nasi kama Mkoa tumeona moja ya Barabara kubwa zenye Lami na mataa itaitwa jina la Samatta,”alisema Makonda, mpenzi na shabiki mkubwa wa klabu ya Simba SC ya Dar es Salaam.
  Kupitia taasisi yao ya Sama Kiba Foundation, Samatta na Kiba walicheza baina mechi ya Hisani katika tamasha la Nifuate jana Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, maalum kuchangia miundombinu ya shuke za Msingi Dar es Salaam.
  Timu ya Samatta rafiki zake, ‘Team Samatta’ ikaibuka na ushindi wa 6-3 dhidi ya Team Kiba, huo ukiwa mwendelezo wa ubabe baada ya mwaka jana pia kushinda 4-2.
  Ni baada ya kuonyesha uwezo mkubwa katika mechi ya mwaka jana, Kiba akasajiliwa na Coastal Union ya Tanga na kuichezea mechi kadhaa za Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu. 
  Samatta amerejea nchini wiki mbili zilizopita akitoka kuipa Genk ubingwa wa Ligi Kuu ya Ubelgiji huku naye akishinda tuzo yake Mwanasoka Bora Mwafrika anayecheza Jupiler Pro League baada ya kumaliza na mabao 23 msimu huu.
  Kwa ujumla, Samatta mwenye umri wa miaka 26, ameifungia Genk mabao 62 katika mechi 156 za mashindano yote tangu amejiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Katika ligi ya Ubelgiji pekee amefunga mabao 47 katika mechi 123, kwenye Kombe la Ubelgiji amefunga mabao mawili katika mechi tisa na Europa League amefunga mabao 14 katika mechi 24.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAMATTA APEWA MTAA KATIKA MOJA YA BARABARA KUBWA ZA MANISPAA YA TEMEKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top