• HABARI MPYA

  Friday, June 07, 2019

  MKUDE, AJIBU NA KAPOMBE WAACHWA KIKOSI CHA TAIFA STARS KINACHOKWENDA MISRI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BEKI wa Simba SC, Shomari Kapombe na viungo Jonas Mkude, wote wa Simba na Ibrahimu Ajibu wa Yanga wameenguliwa kwenye kikosi cha  timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars kinachoondoka leo kwenda Misri kwa kambi ya mwisho ya kujiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zikazofanyika baadaye mwezi huu nchini Misri. 
  Wengine walioenguliwa ni Kennedy Wilson wa Singida United, Ally Ally wa KMC, Khamis Khamis wa Kagera Sugar na Ayoub Lyanga wa Coastal Unon ya Tanga.
  Taifa Stars inaondoka na wachezaji 32 kwenda kambini mjini Alexandria, Misri baada ya kuchujwa saba na kati ya hao ni 23 tu watashiriki AFCON.

  Kiungo Jonas Mkude (katikati) ameachwa kikosi cha Taifa Stars kinachoondoka leo kwenda Misri kushiriki AFCON 

  Wachezaji wengine wataendelea kubaki kambini kwa maandalizi ya michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.
  Kikosi cha kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike kitaanza na mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji wa AFCON, Misri Juni 13, mwaka huu Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria.
  Baada ya hapo Taifa Stars itacheza mechi zake tatu za Kundi C mfululizo ikianza na Senegal Juni 23, Kenya Juni 27 na kumaliza na Algeria Julai 1 kuangalia matokeo yake kama yataipeleka hatua ya mtoano.  
  Kikosi cha Taifa Stars kinachoondoka kinaundwa na makipa; Aishi Manula (Simba SC), Metacha Mnata (Mbao FC), Suleiman Salula (Malindi SC) na Aaron Lulambo (Tanzania Prisons).
  Mabeki; Claryo Boniface (U20), Hassan Kessy (Nkana FC, Zambia), Vincent Philipo (Mbao FC), Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni (Simba SC), Kelvin Yondan, Gardiel Michael (Yanga SC), Abdi Banda (Baroka FC, Afrika Kusini), Ally Mtoni (Lipuli FC), David Mwantika na Aggrey Morris (Azam FC).
  Viungo ni Feisal Salum, Himid Mao (Petrojet, Misri), Frank Domayo, Mudathir Yahya (Azam FC), Shiza Kichuya (ENNPI, Misri), Simon Msuva (Difaa Hassan El-Jadidi Morocco), Farid Mussa (Tenerife, Hispania) na Freddy Tangalu (Lipuli FC).
  Washambuliaji ni Yahya Zayd (Ismailia, Misri), Shaaban Iddi Chilunda (Tenerife, Hispania), Rashid Mandawa (BDF, Botswana), Miraj Athumani (Lipuli FC), Kelvin John (Serengeti Boys), Adi Yussuf (Solihull Moors, England), John Bocco (Simba SC), Thomas Ulimwengu (JS Saoura, ALgeria) na Nahodha Mbwana Samatta (KRC Genk, Ubelgiji).  
  Mbali na Taifa Stars kupangwa Kundi C AFCON 2019 pamoja na jirani zao, Kenya, Algeria na Senegal – wenyeji, Misri wapo Kundi A pamoja na na Zimbabwe, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Kundi B linaundwa na Burundi, Madagascar, Guinea na Nigeria, Kundi D linaundwa na Namibia, Afrika Kusini, Ivory Coast na Morocco, wakati Kundi E kuna Angola, Mauritania, Mali na Tunisia na Kundi F ni Guinea Bessau, Benin, Ghana na mabingwa watetezi, Cameroon. 
  Taifa Stars imefuzu AFCON ya mwaka huu baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi L kwa pointi zake nane, nyuma ya jirani zao wa Afrika Mashariki, Uganda walioongoza kwa pointi zao 13 wakizipiku Lesotho iliyomaliza na pointi sita na Cape Verde pointi tano.    
  Mwaka huu, Tanzania itashiriki AFCON kwa mara ya pili tu kihistoria baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria ambako ilipangwa Kundi A pamoja na wenyeji, Nigeria, Misri na Ivory Coast na kushika mkia.
  Mwaka 1980 ilifungwa mechi mbili, 3-1 na Nigeria na 2-1 na Misri kabla ya kutoa sare ya 1-1 na Ivory Coast na kuishia Raundi ya kwanza tu, wakati timu nane tu zinashiriki michuano hiyo.   
  Michuano itaanza Juni 21 hadi Julai 19 na Taifa Stars itachezea mechi zake Uwanja wa Juni 30 na Al Salam mjini Cairo.
  Na katika CHAN, Taifa Stars itaanzia nyumbani dhidi ya Sudan Julai 26 kabla ya kurudiana Agosti 2 na ikifuzu mtihani huo itamenyana na mshindi kati ya Kenya na Burundi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MKUDE, AJIBU NA KAPOMBE WAACHWA KIKOSI CHA TAIFA STARS KINACHOKWENDA MISRI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top