• HABARI MPYA

  Sunday, June 02, 2019

  MECHI ZA PLAY-OFF PAMBA NA KAGERA, GEITA GOLD NA MWADUI FC SASA KUCHEZWA KESHO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MECHI za kwanza za mchujo wa kuwania kupanda na kubaki Ligi Kuu ya Tanzania Bara zilizokuwa zifanyika leo Kanda ya Ziwa zimeahirishwa hadi kesho.
  Mechi hizo ni baina ya Pamba SC na Kagera Sugar ya Bukoba iliyopangwa kufanyika Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza na Geota Gold Mine dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga Uwanja wa Nyankumbu, Geita.   
  Hata hivyo, Azam Media Limited walioombwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kuonyesha mechi zote nne za nyumbani na ugenini baina ya Kagera Sugar na Mwadui FC zilizoangukia kwenye Play-Off kutoka Ligi Kuu na Pamba na Geita zinazowania kupanda kutoka Daraja la Kwanza wameshindwa kufanya hivyo leo.


  Taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliyotolewa na Afisa Habari na Mawasiliano, Cliford Mario Ndimbo imesema kwamba mechi hizo zimesogezwa mbele hadi kesho kutokana na sababu za kiusalama. 
  Ndimbo amesema mechi zote, zikiwemo za marudiano zitakazochezwa Juni 8 zitaoneshwa moja kwa moja ( live ) na kituo cha televisheni cha Azam TV. 
  "Usalama wa magari ya Azam TV ulikuwa mdogo kutokana na baadhi ya washabiki kutishia kuvunja vioo wakipinga mechi hizo kuoneshwa. Kwa mujibu wa Kanuni za Ligi, haki za matangazo ya televisheni ni mali ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)," amesema Ndimbo.
  Afisa Habari huyo ameonya timu itakayozuia mechi yake kuonyeshwa, itahesabika kuwa haikufika uwanjani, hivyo itachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni. 
  "Viongozi wa timu husika waepuke kutoa matamko ambayo ni kinyume na kanuni za mpira wa miguu. Kwa watakaokwenda kinyume watachukuliwa hatua za kinidhamu na kimaadili," amesema Ndimbo.
  Kwa upande wao Azam nao wametoa taarifa isemayo; “Mpendwa mteja wetu, tumelazimika kuondoa magari ya matangazo katika viwanja viwili vya Geita & Nyamagana baada ya kutokea sintofahamu na vurugu juu ya urushwaji live wa mechi mbili za FDL Play-Off,” imesema taarifa ya Azam Media leo na kuongeza;
  “Awali, Azam Media Ltd iliombwa na TPLB kusaidia kuonyesha live mechi hizo ili kudhibiti vitendo vya hujuma, Azam TV ilikubali ombi hilo na kufanya maandalizi yote ikiwa ni pamoja na kusafirisha magari ya matangazo mpaka viwanja husika kwa kuzingatia umuhimu wa ombi la TPLB,”.
  “Msimamo wa Azam Media Ltd ni kutenda haki na usawa kwa ama kuonesha mechi zote nne au kuacha kabisa kuonesha mechi hizo.. Baada ya Azam Media Ltd kuondoa magari yetu na kuanza safari kurudi DSM, tumepokea ombi jipya toka TPLB kuwa mechi hizo hazitafanyika leo na wametuomba tubakie na kuzionesha tena hapo kesho.,”.
  Azam Media Ltd imekubali ombi hilo kwa maana hiyo mchezo kati ya Pamba na Kagera utaruka Kwenye chaneli ya Azam Sports 2 hapo kesho saa 10 jioni na mchezo kati ya Geita Gold na Mwadui FC utaruka Azam Sports HD kesho saa 10 jioni,” wamesema Azam Tv.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MECHI ZA PLAY-OFF PAMBA NA KAGERA, GEITA GOLD NA MWADUI FC SASA KUCHEZWA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top