• HABARI MPYA

  Monday, June 03, 2019

  MAKONDA AMZAWADIA MANULA SH MILIONI 10 KWA KUDAKA VIZURI DHIDI YA MAZEMBE LUBUMBASHI

  Na Asha Said, DAR ES SALAAM
  MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amemzawadia kitita cha Sh. Milioni 10 kipa wa Simba SC, Aishi Manula kwa kufunga udakaji wake mzuri kwenye mechi ya marudiano ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Simba ikichapwa 4-1 na wenyeji, Tout Puissant Mazembe mjini Lubumbashi Aprili 13 mwaka huu.
  Makonda amemkabidhi Manula kitita hicho leo ofisini kwake mjini ikiwa ni kutekeleza ahadi aliyoitoa wiki iliyopita katika sherehe za tuzo za Mo Simba hoteli ya Hyatt Regency, Dar es Salaam.
  Siku hiyo, Makonda alisema atamzawadia Manula Sh. Milioni 10 kwa udakaji wake mzuri kwenye mechi ya mwisho ya Simba michuano ya Afrika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Sh, Milioni 1 kila mchezaji aliyeshinda tuzo. 
  Na leo pamoja na kumkabidhi Manula Sh. Milioni 10, lakini akamkabidhi kila mchezaji aliyeshinda tuzo Alhamisi iliyopita Sh. Milioni 1.
  Waliopewa fedha hizo ni mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere aliyeshinda tuzo za Mchezaji Bora na Mfungaji Bora, Erasto Edward Nyoni aliyeshinda tuzo mbili pia, Mchezaji Bora wa Wachezaji na Beki Bora na Mghana James Kotei aliyeshinda tuzo ya Kiungo Bora.
  Wengine ni Nahodha John Bocco aliyeshinda tuzo ya Mshambuliaji Bora, kiungo Mzambia Clatous Chama aliyeshindia tuzo ya Goli Bora, Rashid Juma aliyeshinda Tuzo ya Mchezaji Bora Mdogo wa Mwaka na Mwanahamisi Omary Shaluwa ‘Gaucho’ aliyeshinda Tuzo ya Mchezaji Bora Mwanamke.
  Mshindi mwingine usiku huo wa Mei 30 ni mfadhili wa zamani wa klabu hiyo, Azim Dewji ameshinda Tuzo ya Heshima baada ya kuiwezesha klabu kufika fainali ya Kombe la CAF 1993 – ambaye kwa kuwa si mchezaji hayumo kwenye ‘Neema ya Makonda’.


  Tuzo za Mo Simba zinafanyika kwa mwaka wa pili mfululizo tangu zianzishwe na Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Mohammed Dewji. 
  Aidha, Makonda alisema Juni 15 atakwenda katika hafla maalum ya Yanga SC ‘Kubwa Kuliko’ ukumbi wa Diamond Jubilee kuchangia kama Mkuu wa Mkoa kwani ni wajibu wake kushirikiana na kila timu ya mkoa huo.                                               
  "Juni 15 nikiwa na baadhi ya wadau tutakwenda katika hafla ya kuichangia Yanga, nami nitachangia kwa sababu napenda maendeleo ya mkoa wangu, ikiwa ni pamoja kupata mapato wakati timu hizi kubwa zikishiriki michuano ya Kimataifa,”alisema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAKONDA AMZAWADIA MANULA SH MILIONI 10 KWA KUDAKA VIZURI DHIDI YA MAZEMBE LUBUMBASHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top